Nabii ‘Iysa Atakua Katika Kundi Gani Miongoni Mwa Makundi 72?
Nabii ‘Iysa Atakua Katika Kundi Gani Miongoni Mwa Makundi 72?
Swali:
Assalaam aleykum
Namshukuru Allah (s.w) Kupata Fursa Hii Kuwaluiza Swali Adhiwym.
Allaah (s.w) Amebainisha Wazi Katika Uislam Juu Ya Kushikamana Pamoja Na Akakataza Makundi. Leo Hii Kila Kukicha Kuna Makundi Yanazuka Mfano Shia, Kadiyani, Answar Sunna, Salafiya Jadiyd, Tabligh, N.k. Je Nabiy Iysa Akirudi Leo Atakua Kundi Gani?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Kwanza kabla hatujajibu swali lako, tunakukumbusha kuwa unapoandika jina la Allaah au Mtume, usifupishe mbele yake kwa kuweka (S.W.) au (S.A.W.) kama ilivyozoelekea na wengi, bali andika kwa kirefu maneno hayo bila ya kuyafupisha. Andika (Subhaanahu wa Ta'alaa) baada ya kumtaja Allaah, na andika Swalla Allaahu 'alayhi wa sallam) au (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) baada ya kumtaja Nabiy. Hivyo ndivyo inavyopaswa, na ndio heshima zaidi na utukufu na ndivyo inavyotamkwa na si kama inavyofupishwa na wengi kimazoea au kivivu. Pia hiyo ni ibada, na ibada inatakiwa ifanywe kwa namna iliyofundishwa na haifai kugeuza, kuongeza au kupunguza. Hali kadhalika swahaba walikuwa wakiandikiana barua na hakuna aliyekuwa akikatisha Salaam, wala kumswalia Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) wala kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) kwenye barua zao. Tuige na tufuate nyendo zao tusalimike.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kundi atakalokuwa Nabiy 'Iysa (‘alayhis-salaam). Tufahamu kuwa haya makundi yote ambayo yapo au yatakayotokea katika nyakati zinazokuja yameundwa na wanaadamu ambao wanapata na wanakosa. Katika hayo uliyoyataja miongoni mwa makundi, Qadiyani na Shia hayaingii katika makundi ya Kiislamu.
Soma maelezo zaidi hapa chini kuhusu Qadiyani (Ahmadiya) na Shia:
Uislamu wa kweli una kanuni na masharti ambayo yanamfanya mwenye kuyafuata kuwa Muislamu wa hakika. Kanuni kubwa ambayo ipo katika Qur-aan na Sunnah ni kuyafuata machimbiko hayo mawili katika kila hali. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:
فَإِن تَنَازَعْتُمْ فِي شَيْءٍ فَرُدُّوهُ إِلَى اللَّـهِ وَالرَّسُولِ إِن كُنتُمْ تُؤْمِنُونَ بِاللَّـهِ وَالْيَوْمِ الْآخِرِ ۚ ذَٰلِكَ خَيْرٌ وَأَحْسَنُ تَأْوِيلًا ﴿٥٩﴾
Mkizozana katika jambo basi lirudisheni kwa Allaah na Rasuli mkiwa mnamwamini Allaah na Siku ya Mwisho. Hivyo ni bora na matokeo mazuri zaidi. [An-Nisaa: 59]. Aayah hii iko wazi kabisa wala haihitaji maelezo ya ziada.
Tuelewe kuwa naye Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema katika Hijjatul Wadai':
"Mimi nimewaachia mambo mawili lau mtashikana nayo basi hamtapotea kabisa: Kitabu cha Allaah na Sunnah zangu" [al-Bukhaariy na Muslim]
Na akasema tena (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
"Hakika atakayeishi katika nyinyi ataona khitilafu nyingi, basi jilazimisheni na kufuata mwendo wangu (Sunnah yangu) na mwendo wa Makhalifa walioongoka, yashikeni kwa magego yenu mambo yao" [Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, Ahmad, Ibn Maajah na ad-Daarimiy].
Kwa hiyo, Nabiy 'Iysa (‘alayhis-salaam) atakaporudi atafuata misingi hii miwili mikubwa. Na dalili kuhusu hilo lipo, mojawapo ikiwa ni ile Hadiyth iliyosahihishwa na al-Albaaniy,
"Kisha utarudi tena Ukhalifa kwa misingi ya Makhalifa waongofu, kufuata mwendo wa Mtume".
Na ile Hadiyth nyingine inayotueleza:
"Hakutakosekana kuwa na kikundi katika Ummah wangu, wakipigana juu ya haki wakiwa washindi haki Siku ya Qiyaama… kisha 'Iysa bin Maryam atashuka, na Amiri wao (Waislamu) atasema: 'Njoo utuswalishe katika Swalah!' Atasema: 'Hapana, nyinyi ndio ma-Amiri juu ya kila mmoja kama heshima kutoka kwa Allaah kwa Ummah huu'" [Muslim].
Hivyo, Nabiy 'Iysa (‘alayhis-salaam) atasimama imara kusimamisha Qur-aan na Sunnah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Na Allaah Anajua zaidi