Thawabu Kusoma Tafsiyr Au Kusoma Qur-aan Kwa Kiarabu?
Thawabu Kusoma Tafsiyr Au Kusoma Qur-aan Kwa Kiarabu?
SWALI:
Asalaam aleykum,
Kwa jina la Allaah mwingi wa rehema, napenda kuuliza maswali yangu machache, In shaa Allaah niwe muulizaji mzuri.
Mimi ninapenda kusoma Qur-aan lakini niko mzito sana kusoma kiarabu kwa sababu hio nimenunua Msahafu wa tafsiri sasa nimekuwa najishuhulisha sana kusoma tafsiri na ule upande ulioandikwa kwa kiarabu huwa sisomi kabisa, pia najiona kwamba nafaidika sana nikisoma tafsiri kwa sababu nafahamu kilicho andikwa kuliko kusoma kiarabu ambacho huwa sifahamu kitu. sasa jee kufanya hivyo ni sawa au nalazimika kusoma kwa kiarabu? na kama ni sawa jee nitakuwa napata thawabu za kusoma Qur-aan kama wanaosoma kwa kiarabu?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukran ndugu yetu kwa maswali yako mazuri kuhusu mambo ya msingi katika Dini yetu tukufu. Insha’Allah nasi tutakujibu kwa mujibu wa misingi yetu ya Uislamu, na kwake Mola Mlezi tunataka usaidizi.
Mas-ala ya kusoma Qur-aan kwa Kiarabu imekuwa ni tatizo kubwa sana hasa kwa vijana wa leo. Hii yote inatokana na kutoona umuhimu wa kusoma Dini na kujikita katika kusoma masomo mengine ambayo tunaona ndio yanayotupatia hadhi katika jamii. Kusoma Qur-aan kupitia kwa tafsiri hata ikiwa ni ya Kiarabu haimpatii mtu huyo thawabu ikiwa ataisoma pekee bila ya kwanza kusoma ya asili yake nayo ni kwa Kiarabu Ni muhimu mtu aweze kusoma kwa Kiarabu na kisha ikiwa haelewi maana asome na tafsiri yake ambayo itampatia muelekeo na uongofu wa Dini yake. Hii ni kwa kuwa Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa Anatueleza:
وَرَتِّلِ الْقُرْآنَ تَرْتِيلًا
Au izidishe, na soma Qur-aan kwa kisomo cha utaratibu upasao... [Al-Muzammil: 4 ]
Sasa utasoma vipi kisomo cha sawa kwa kutumia lugha nyengine isiyokuwa ya asli. Na Rasuli wa Allah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
((من قرأ حرفاً من كتاب الله فله به حسنة،والحسنة بعشر أمثالها، لا أقول: ألم حرف، ولكن ألفحرف، ولام حرف، وميم حرف))
"Yeyote mwenye kusoma herufi katika kitabu cha Allah ataandikiwa mema, na mema moja ni sawa na kumi mfano wake. Sisemi الـم A.L.M. ni herufi, lakini Alif ni herufi na Laam ni herifi na Miim ni herufi" [at-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Sahiih].
Na tuelewe kuwa mtu aliye bora miongoni ni yule mwenye kujifunza Qur-aan kisha naye akaifunza
حديث عثمان رضي الله عنه : عن النبي صلى الله عليه وسلم قال: ((خيركم من تعلم القرآن وعلمه )) صحيح البخاري
Imetoka kwa 'Uthmaan (Radhwiya 'anhu) kwamba Nabiy Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi sallam kasema: "Mbora wenu ni yule mwenye kujifuna Qur'aan kisha (naye) akafundisha". [Al-Bukhariy]
Nasiha yetu kwako na kwa kaka na dada zetu mfano wako ni kuwa ima tuwe ni wenye kupata wasaa wa kujifunza kupitia kwa mwalimu ikiwa yupo karibu na hili ni jambo linalohimizwa sana. Na kujifunza Qur-aan ni rahisi sana haimchukui mtu zaidi ya miezi tatu ikiwa atafanya juhudi kubwa ataweza kuanza kusoma Qur-aan kisha pole pole ataweza kuendeleza mwendo wa kusoma haraka Insha Allaah.Kama ulivyosema unapata shida katika kusoma lakini usife moyo kwani kwa kufanya hivyo unapata thawabu mara mbili. Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) anasema:
"Yule ambaye kwamba anasoma Qur-aan naye ni mjuzi (hana shida aina yoyote) atakuwa pamoja na Malaika na Rusuli 'Alayhim-sallam na watiifu. Na yule ambaye kwamba anarudia pamoja na kuwa na shida katika kusoma basi atakuwa na ujira miwili". [ al-Bukhaariy, Muslim, Tirmidhy na Ibn Maajah kutoka kwa ‘Aishah (Radhwiya Allaahu 'anhaa)]
Huu ni uhimizo mkubwa ambao inatakiwa tuuzingatie.
Hivyo, jaribu usome kwa Kiarabu kiasi fulani hata kama ni kidogo na kisha usome tafsiri ili ipate kuleta taathira na mabadiliko katika mambo yetu. Na kama tunavyoelewa Qur-aan ndio inayotumika katika Swalah hivyo kuweza kutusaidia katika kujihimiza kusoma na hivyo kuweza kutekeleza nguzo hiyo bila shida aina yoyote.
Pia ni vyema hapa tuseme kuwa Qur-aan imeteremshwa ili kutubadilisha katika maisha yetu hivyo inatakiwa tusisome kama kasuku bali tuelewe kwa kusoma tafsiri ili tupate kuyafanyia kazi maagizo na makatazo yaliyomo ndani yake. Swahaba Radhwiya 'Allaahu 'amhum walikuwa wanachukua muda mrefu kuhifadhi Qur-aan kwa kuwa walikuwa baada ya kuchukua aayah 10 walikuwa hawachukui nyingine mpaka wahifadhi hizo na kuzifanyia kazi. Ndio Ibn ‘Umar Radhwiya Allaahu 'anhu alichukua miaka kumi kuihifadhi Suwrah Al-Baqarah [Maalik].
Kwa sababu ya nia yako nzuri na kujitahidi kusoma na kuyafanyia kazi yaliyomo katika Qur-aan Allaah Subhaanahu wa Ta'aalaa atakupatia ujira kwa hilo na akupatie kheri hapa duniani na kesho Aakhirah.
Na Allaah Anajua zaidi