Janaba: Amelala Na Janaba Hadi Jua Likatoka Nini Hukmu Ya Swawm Yake?

SWALI:

Asalam aleikum

swali langu ni ikiwa mtu amelala  na janaba  mpaka jua likatoka  jee swaum inafaa amaitakuwa haifai  

shukranwa jazakum Allaah bil kher

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Tumewapa nasaha mara nyingi kuwa haipasi kufanya mchezo na amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) na Mjumbe Wake (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam). Amri za kufunga Swawm, kuitimiza ipasavyo, kwa wakati wake na ruhusa ya kufanya yote anayojizuia mja kwa wakati wake yanapaswa yote yatekelezwe bila ya kwenda kinyume au kudharau.

 

 

 

Swalah ya Alfajiri hata bila ya kuwa na Swawm inampasa Muislamu aitekeleze kwa wakati wake nao ni kuanzia Alfajiri hadi kabla ya jua kuchomoza. Sasa vipi Muislamu asiswali asubiri hadi jua lichomoze ndio atake kuswali? Huo utakuwa sio tena wakati wa Swalah hiyo, kwa hivyo utakuwa hukutimiza Swalah hiyo ya Alfajiri kamakamakama ilivyothibiti katika Hadiyth ifuatayo: kupitiwa na usingizi au kusahau ilivyowekewa muda wake maalumu. Isipokuwa tu ikiwa umefikwa na udhuru wa mambo yaliyoruhusu sheria

 

 

 

((من نسي صلاة أو نام عنها ، فكفارتها أن يصليها إذا ذكرها، لا كفارة لها إلا ذلك))  رواه مسلم 

 

 

 

((Atakayesahau Swalah au ikampita akiwa amelala basi kafara yake ni kuiswali atakapokumbuka, hakuna kafara isipokuwa hiyo)) [Muslim]

 

Ikiwa hali yako ilikuwa baina ya mambo hayo mawili; kulala au kusahau hizo mbili basi unatakiwa haraka ufanye ghuslu na uswali, na uendelee na Swawm yako. Na ikiwa umefanya makusudi basi unatakiwa uombe Tawbah kwa Mola wako na uazimie kutokurudia tena, na undelee na Swawm yako na itakuwa imesihi ila itakuwa imepunguka thawabu zake kwa dharau ya kutokutimiza amri.

 

 

 

Fahamu kuwa pamoja na kuwa umepewa udhuru wa kulala, lakini wewe na Mola wako ndio mnaojua nia haswa na ukweli wa kutoweza kwako kuamka, kwani kuna njia nyingi za kumwezesha mtu kuamka anapotaka, nazo ni kuweka alamu ya saa, kumuomba mtu amwamshe na njia zinginezo nyingi. Hivyo, hakikisha umetumia njia zote hizo ikiwa kweli unamcha Mola wako na unajali Dini yako.

 

 

 

Ingelikuwa umewahi kufanya ghuslu kabla ya jua kuchomoza basi kusingelikuwa na ubaya wowote kwani hivyo imeruhusiwa na hakuna dhambi kufanya hivyo. Dhambi ni kujiachia hadi jua lichomoze na kukosa kutimiza fardhi.

 

 

 

Ingia katika viungo vifuatavyo upate maelezo zaidi ya mas-ala haya:

 

 

 

 

 

Kulala Na Janaba Na Kuamka Na Swawm

 

Wakati Wa Mwisho Kukoga Janaba Katika Mwezi Wa Ramadhaan

 

Twaharah Ya Hedhi Kabla Ya Alfajiri Na Ghuslu (Josho) Baada Ya Alfajiri

 

 

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share