03-Fatwa: Mtoto Ana Uwezo Mzuri Wa Kifedha Lakini Baba Anashikilia Kumtolea Zakaatul-Fitwr
Mtoto Wa Kiume Ana Uwezo Mzuri Wa Kifedha Lakini Baba
Anashikilia Kumtolea Zakaatul-Fitwr
SWALI:
Baadhi ya baba wanashikilia kuwatolea Zakaatul-Fitwr watoto wao wakiume ambao wana uwezo mzuri wa kifedha. Afanyeje mtoto?
JIBU:
AlhamduliLLaah,
Madamu mtoto anao uwezo, inampasa atoe mwenyewe Zakaatul-Fitwr. Ikiwa baba atamlipia Zakaatul-Fitwr hakuna ubaya khaswa ikiwa ni mazoea ya baba kuwatolea watoto wake Zakaatul-Fitwr kila mwaka japokuwa wameshakuwa wakubwa na wafanyakazi. Huenda akapenda kuendelea kufanya hivyo alivyozoea kabla na huenda ikamkasirisha baba ikiwa mwanawe atamwambia: "Usinilipie Zakaah". Hivyo mtoto ampe fursa baba yake kumlipia Zakaatul-Fitwr na pia mwenyewe ajitolee. Baadhi ya watu wanachukulia kwamba kuendelea kuwatolea watoto wao Zakaah ni kuendeleza kuambatana na watoto wake na dalili ya kwamba wao bado wako chini ya hifadhi na mas-uliya yake. Hivyo mtoto ampe baba yake fursa afanye kinachomfurahisha.
Na Allaah Anajua zaidi