Swalah Ya Tasbiyh Ni Swahiyh?

SWALI:

 

NDUGU ZANGU,

NAOMBA KUWAULIZA NISAIDIENI   TAFADHALI SALATI-TASBIYH   NI SAHIHI?   MTUME WETU (S.A.W.) ALIKUWA ANASALI? NA SISI TU SALI? PLZ PUT LIGHT ON THIS SUBJECT!

JAZAAKALLAHU KHEIR WASSALAAM

 

 

SWALI LA PILI:

 

Assalam Aleykum  
I've been receiving emails about Salatul Tasbih...Is there such a salat???? Please let me know so I can inform the others.

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Swalah hii ya Tasbiyh ina utata usahihi wake, na Maulamaa wakubwa wametofautiana kuhusu usahihi na udhaifu wake. Hata hivyo, wengi wamekubaliana kuwa Hadiyth yake ina kasoro na hivyo ni bora mtu kuiacha kuswali.

 

Kwanza tuitazame ilivyo Swalah yenyewe, kisha tutazame uchambuzi wa Wanachuoni kuhusu Hadiyth yake.

 

Swalah hiyo imeelezwa ni Rak'ah nne. Imeitwa hivyo kwa sababu kila moja ya Rak'ah zake unaleta Tasbiyh mara 75 ifuatayo: Subhaana-Allaahi wal HamduliLLaah wa Laa ilaaha illaa Allaahu wa Allaahu Akbar.

 

Imeelezwa katika Hadiyth hiyo kuwa inaswaliwa ifuatavyo, katika Rak'ah ya kwanza baada ya kusoma Suratul-Faatihah na Surah nyengine, unasoma hiyo Tasbiyh mara 15, kisha unarukuu na baada ya kuleta zile Tasbiyh tatu za kawaida utasoma hiyo Tasbiyh mara 10. Kisha unainuka katika iitidali utasoma hiyo Tasbiyh mara 10, kisha utasujudu. Baada zile Tasbiyh za kawaida utasoma hiyo Tasbiyh mara 10. Utasoma mara 10 tena katika kikao baina ya sijda mbili na katika sijda ya pili utaleta hizo Tasbiyh mara 10. Wakati wa kuinuka na katika kile kitako cha mapumziko utasoma Tasbiyh mara 10. Unafanya hivyo katika Rak'ah ya pili mpaka umalize Swalah hiyo.

 

Wanachuoni wachache waliosema kwamba Hadiyth hiyo ni Swahiyh wamechukulia Hadiyth iliyohusishwa na Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba alimwambiwa ami yake 'Abbaas:

 

"يَا عبَّاسُ يَا عَمَّاهُ!  أَلا أُعْطيكَ ، أَلا أَمْنَحُكَ ، أَلا أَحْبُوكَ  ، أَلا أَفْعَلُ بِكَ عَشْرَ خِصَالٍ ؟ إِذَا أَنْتَ فَعَلْتَ ذَلِكَ غَفَرَ اللهُ لَكَ ذَنْبَكَ : أَوَّلَهُ وَآخِرَهُ ، قَدِيمَهُ وَ حَديِثَهُ خَطَأَهُ وَعَمْدَهُ ، صَغِيرَهُ وَكَبِيَرهُ ، سِرَّهُ وَعَلانِيَتَهُ ، عَشْرَ خِصَالٍ : أَنْ تُصَلِّيَ أَرْبَعَ رَكَعَاتٍ تَقْرَأُ في كُلِّ رَكْعَةٍ فَاتِحَةَ الْكِتَابِ وَسُورَةً ، فَإِذَا فَرَغْتَ مِنَ الْقِرَاءَةِ في أَوَّلِ رَكْعَةٍ فَقُلْ وَأَنْتَ قَائِمٌ : سُبْحَانَ اللهِ وَالْحَمْدُ للهِ وَلا إِلهً إِلَّا اللهُ وَاللهُ أَكْبَرُ خَمْسَ عَشَرَةَ مَرَّةً ، ثُمَّ تَرْكَعُ فَتَقُولُهَا وَأَنْتَ رَاكِعٌ عَشَراً ، ثُمَّ تَرْفَعُ رَأْسَكَ مِنَ الرُّكُوعِ فَتَقُولُهَا عَشْراً ، ثُّمَ تَهْوِي سَاجِدَاً فَتَقُولُهَا وَأَنْتَ سَاجِدٌ عَشْراً ، ثُمَّ تَرْفَعُ رَأْسَكَ مِنَ السُّجُودِ فَتَقُولُهَا عَشْراً ، ثُمَّ تَسْجُدُ وَتُقُولُهَا عَشْراً ، ثُمَّ تَرْفَعُ رَأْسَكَ فَتَقُولُهَا عَشْراً ، فَذلِكَ خَمْسٌ وَسَبْعُونَ في كُلِّ رَكْعَةٍ ، تَفْعَلُ ذلِكَ في أَرْبَعِ رَكَعَاتٍ ، إِنْ اسْتَطَعْتَ أَنْ تُصَلِّيَهَا في كُلِّ يَوْمٍ مَرَّةً فَافْعَلْ ، فَإِنْ لَمْ تَسْتَطِعْ فَفِي كُلِّ جُمُعَةٍ مَرَّةً ، فَإِنْ لَمْ تَفْعَلْ فَفِي كُلِّ شَهْرٍ مَرَّةً ، فَإِنْ لَمْ تَفْعَلْ فَفِي كُلِّ سَنَةٍ مَرَّةً ، فَإِنْ لَمْ تَفْعَلْ فَفِي عُمُرِكَ مَرَّةً " رواه أبو داود  

 

"Ewe 'Abbaas, Ewe ami yangu! Je, nikupe, nikupe zawadi, nikupe zawadi kumi khaswa. Ukifanya nitakayokuambia hivi karibuni utapata faida kumi: Allaah Atakusamehe madhambi yako yote, ya mwanzo na ya mwisho, ya zamani na mapya, uliyofanya kimakosa na makusudi, makubwa na madogo, (uliyofanya) kwa siri na kwa dhahiri, kumi kwa ujumla. Uswali Rak’ah nne (za Swalah), katika Rak’ah ya kwanza usome Al-Faatiha na Suwrah. Kisha wakati bado umesimama usome: Subhaana-Allaah, wal-HamduliLLaah, wa laa ilaaha illa-Allaah, wa-Allaahu Akbar' mara 15. Kisha urukuu na usome hivyo mara 10, kisha unyanyue kichwa chako kutoka rukuu' usomea mara 10 wakati umesimama, kisha nenda kasujudu usema mara 10, kisha nyanyua kichwa chako kutoka sujuud ukiwa umekaa useme tena mara 10. Kisha unapokwenda kusujudu tena useme maneno hayo hayo mara 10, kisha unyanyue kichwa chako kutoka sujuud useme tena mara 10. Itajumlika kuwa zote ni Tasbiyh 75 katika Rak’ah moja. Ufanye hivyo katika Rak’ah zote nne. Ukiweza kufanya mara moja kwa siku fanya, usipoweza fanya mara moja kwa wiki, usipoweza fanya mara moja kwa mwezi, usipoweza fanya mara moja kwa mwaka, usipoweza fanya mara moja katika umri wako" [Abuu Daawuwd]

 

Hakika ni kuwa Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) hakuwahi kabisa kuswali Swalah hii katika maisha yake.

 

Hadiyth nyingi zilizokuja kueleza fadhila na ubora wa Swalah hii ima ni dhaifu, ngeni au zilizozuliwa.

 

Wanachuoni kama Ibn Hajar, As-Subkiy, Ibn Al-Mubaarak, Ibn Mandah, Az-Zarkashiy, At-Tirmidhy, Abur Daawuwd, Al-Bayhaqiy na Al-Albaaniy ambao wamesema baadhi ya riwaya zake ni Hasan au Swahiyh.

 

Lakini Wanachuoni wengi wakiwemo Imaam Ahmad na Imaam Al-Bukhaariy wameipinga na kusema ni Munkar na haifai, na wengine kama Shaykh Al-Islaam Ibn Taymiyyah, Ibn Al-Jawziy, Al-Mizzi, Imaam An-Nawawiy na wengineo wa karibuni kama Ibn Baaz, Ibn ‘Uthaymiyn wamechambua na kusema kuwa riwaya zake ni dhaifu na hivyo haziwezi kutumiwa kama hoja na kuifanyia kazi. Na wakasema hata mpangilio wa Swalah yenyewe unatofautiana na mpangilio wa Swalah za kawaida ambazo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alizotufundisha.

 

Jambo jingine ambalo linalotendeka ambalo halipasi ni kuwa Swalah hii inaswaliwa sana na watu zinapoingia siku kumi za mwisho za Ramadhwaan. Bali utakuta baadhi ya Misikiti ma-Imaam wanaiswalisha siku ya tarehe 27 ya Ramadhwaan. Kufanya hivyo ni bid'ah kwani hata kama Hadiyth ingekuwa ni Swahiyh, lakini haikutaja kuwa iswaliwe Ramadhwaan au inapoingia kumi la mwisho la Ramadhwaan. Kwani kutekeleza 'ibaadah kwa wakati maalumu au idadi maalumu bila ya kuweko na dalili huwa ni jambo la uzushi.

 

Hivyo Muislamu inampasa ajiepushe na uzushi kama huo.

Tumeona kwamba imetajwa iswaliwe ima mara moja kwa siku, au mara moja kwa wiki, au mara moja kwa mwezi au mara moja kwa mwaka au mara moja katika umri wa bin Aadam. Sasa vipi iwe mwezi wa Ramadhwaan tu ndio itekelezwe au inapoingia tu kumi la mwisho iwe ndio miongoni mwa 'ibaadah muhimu za kutekelezwa tena kwa kuswaliwa jamaa'ah?

 

Nasaha zetu ni kuwa ni bora tuache kuswali Swalah hiyo kwani zipo Swalah nyingine za Sunnah ambazo ni sahihi na zina fadhila kubwa sana kama Tahajjud, Dhuhaa, Witr na zile za kabla na baada ya Swalah za faradhi zilizohimizwa.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share