Tahiyyatul-Masjid Swalaah Za Sunnah Wakati Imaam Anahutubia

Tahiyyatul-Masjid Swalah Za Sunnah Wakati Imaam Anahutubia

  

www.alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 

Assalam Alaikum Warahmatulah Wabarakatuhu.

 

Ama Baad, Ndugu zangu wa Alhidaya ninaswali nataka kuwauliza na In Shaa Allaah atawawezesha kulijibu.

 

 

Nilienda msikitini siku ya Ijumaa, Imamu mmoja aliyekuwa akihutubu akasema kuwa ni vibaya kuswali sunnah kama imamu ashaanza kutoa khutba kwa sababu mawaidha ni kama swala na mtu akiswali na huku imamu yuwatoa mawaidha atakuwa anaswali swala ndani ya swala, je hivi ni kweli, naomba msaada kutoka kwenu maana alinichanganya kwa sababu nishazoea kuswali sunnah ninapoingia msikitini.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Ifahamike kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuwekea Sunnah ya Tahiyyatul Masjid (kuuamkua Msikiti) pindi Muislamu anapoingia Msikitini na kabla ya kukaa.  

 

Swalaah hii yaweza kuswaliwa hata wakati uliokatazwa kuswaliwa Sunnah nyinginezo, unaweza kuiswali hata baada ya Swalaah ya Alfajiri mpaka jua lichomozapo, wakati wa zawali na baada ya Swalaah ya Alasiri.

 

 

Mwanzo si sawa kabisa maneno aliyosema Imaam wako kuwa mawaidha ni kama Swalaah. Hivi ni vitu viwili tofauti kabisa wala havifanani wala kulingana. Mawaidha ni mawaidha na Swalaah ni Swalaah. Mtu akiwa anatoa mawaidha anaweza kumsemesha mtu mwengine msikilizaji hata kumuuliza swali lakini katika Swalaah haifai.

 

Na kuwa maneno yake si sahihi hebu tusikilize maneno ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Jaabir (Radhwiya Allaahu 'anhuma) amesema: Aliingia mtu siku ya Ijumaa na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anahutubu, akamuuliza: "Je, umeswali?" Akasema: "Hapana". Akasema (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): "Swali rakaa mbili" [al-Bukhaariy na Muslim].

 

Na katika lafdhi nyingine: "Simama uswali rakaa mbili na uzifanye nyepesi".

 

Hata kama mtu ameingia akaketi chini inapendeza asimame na kuswali rakaa mbili hata ikiwa Imaam anahutubu na aifanye hiyo Swalaah nyepesi (asiirefushe).

 

Hivyo, ndugu ni juu yako kuendelea na Swalaah hiyo ya Tahiyyatul Masjid hata kama umechelewa na Imaam anahutubu. Pia ni jukumu lako kumfahamisha Imaam Hadiyth hii iliyo sahihi kuhusu hilo.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share