Kutumia Lotion au Mafuta Ambayo Ingredient Yake Ina Alcholol

 

SWALI:

 

Assalam Alaykum, poleni sana kwa kazi kubwa mnayoifanya ya kuipeleka mbele Dini ya ALLAAH kwa njia ya internet. Nawaombea dua Allaah awalipe kila la kheri na awaepushe na kila la shari - AMEEN. Kwenye perfume nyingi na hata lotion ukisoma zile ingredients zake utakuta kuna percentage fulani ya alcohol. Naomba ufafanuzi wa hili katika sheria ya Dini yetu tukufu ya kiislam, hasa ukizingatia kuwa sisi wanaume tumeruhusiwa kujipamba kwa manukato.

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa du'aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Atutakabalie hizo du'aa na Atuzidishie uwezo wa kuelimishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn

Maulamaa wamekhitilafiana kidogo katika mas-ala haya kuhusu vitu vinavyolevya ikiwa vinatumiwa katika mwili ni najisi au sio najisi. Ikhtilaafu hizo zimerejewa kutokana na ilivyofahamika kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala):

 

((يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُواْ إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالأَنصَابُ وَالأَزْلاَمُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ))

  ((إِنَّمَا يُرِيدُ الشَّيْطَانُ أَن يُوقِعَ بَيْنَكُمُ الْعَدَاوَةَ وَالْبَغْضَاء فِي الْخَمْرِ وَالْمَيْسِرِ وَيَصُدَّكُمْ عَن ذِكْرِ اللّهِ وَعَنِ الصَّلاَةِ فَهَلْ أَنتُم مُّنتَهُونَ))   

 

((Enyi mlioamini! Bila ya shaka ulevi, na kamari, na kuabudu masanamu, na kupiga ramli, ni uchafu katika kazi ya shaytwaan. Basi jiepusheni navyo, ili mpate kufanikiwa))

 

((Hakika shaytwaan anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Allaah na kuswali. Basi je, mmeacha?)) [Al-Maaidah: 90-91]

Waliosema kuwa ni haifai kutumia ni kutokana na kauli ((…basi jiepusheni navyo..)) hivyo ni kuepukana navyo katika hali zote ikiwa ni kunywa au kutumia katika ngozi au kwa utumiaji wowote mwingine.

Ama rai nyingine ni kwamba inafaa kwa sababu kauli ya Allaah katika hizo Aayah ((...shaytwaan anataka kutia kati yenu uadui na chuki kwa ulevi na kamari, na akuzuieni kumkumbuka Allaah na kuswali. Basi je, mmeacha?)) Imefahamika kuwa hapa imekusudiwa kuharamishwa kunywa pekee kwa sababu kujipaka katika ngozi hakumleweshi mtu na kumtoa katika fahamu zake au kuzibadilisha  na hivyo hakupeleki katika uadui, chuki n.k.

Rai iliyo sahihi kabisa ni kwamba imeruhusiwa kutumia manukato au vipodezo venye alkoholi katika mwili ikiwa asilimia ya alkoholi ni ndogo. Lakini ikiwa asilimia ya alikoholi ni kubwa basi haifai kutumia isipokuwa panapohitajika kama katika kusafisha vidonda n.k.  

Hivyo manukato yanayotumiwa kawaida na watu hayana ubaya lakini ni vizuri zaidi kutumia manukato ambayo yanajulikana kuwa hayana alkoholi kama manukato ya ambari, 'uud, miski n.k.

Soma pia Swali na Jibu lifautalo:

 Je, Manukato Ni Halaal?

 Na Allaah Anajua zaidi

Share