Nataka Kujua Matumizi Na Fadhila Za Suwrah Yaasiyn na Ayatul-Kursiy

 

Nataka Kujua Matumizi Na Fadhila Za  Suwrah Yaasiyn na Ayatul-Kursiy

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Nataka kujua matumizi na fadhila za Suwrah Yaasiyn na Ayatul Kursiy

 

Nina matumaini nitaafahamishwa vizuri nawatakia kila la kheri waislam wenzangu

   
 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Watu wanaifanyia vishindo Suwrah Yaasiyn na  wakabuni na kutumia Hadiyth dhaifu na ndipo limewafanya Waislamu kuipa nyongo Qur-aan nzima na wakawa wanaisoma Suwrah hii peke yake na nyingine chache. Hii ni kinyume na agizo la kuisoma Qur-aan pole pole na kidogo kidogo kuanzia Suwratul-Faatihah hadi An-Naas. Hadyith nyingi kuhusu fadhila za Suwrah hii ni dhaifu na za kuzushwa.

 

 

Miongoni mwa Hadiyth hizo kuhusu fadhila ya Suwrah hiyo ya Yaasiyn ni ile ya at-Tirmidhiy inayosema: “Kila kitu kina moyo wake, na moyo wa Qur-aan ni Yaasiyn. Atakayeisoma mara moja, Allaah Atamuandikia thawabu za kwamba ameisoma Qur-aan yote mara kumi.” Mwenyewe At-Tirmidhiy papo hapo alipoitaja alisema kuwa hii ni Hadiyth ngeni, yaani aina ya Hadiyth dhaifu.

 

Nyingine ni ile inayosema: “Kuisoma Yaasiyn kunampa msomaji alilolikusudia”. Hii ndiyo kabisa haina nguvu hata chembe wala tamko hili si la Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Ama Aayatul-Kursiy (2: 255) ni Aayah Tukufu kabisa kutokana na dalili.

 

Kutoka kwa ‘Abdullaahi bin Rabaah Al-Answaariy kutoka kwa ‘Ubayy bin Ka’ab ambaye amehadithia: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  amesema: “Yaa Abal-Mundhir! Hivi unajua ni Aayah gani ndani ya Kitabu cha Allaah kuwa ni adhimu kabisa?” Akasema: Nikasema: Allaah na Rasuli Wake ni wajuzi zaidi. “Yaa Abal-Mundhir! Hivi unajua ni Aayah gani ndani ya Kitabu cha Allaah kuwa ni adhimu kabisa?” Akasema: Nikasema: "Allaah, hapana mwabudiwa wa haki ila Yeye, Aliyehai daima, Msimamia kila kitu". (mpaka mwisho wa Aayah). Akasema Ubayy: Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)  akanipiga kifuani kisha akasema: “Wa-Allaahi upongezwe kwa ‘ilmu yako yaa Abal-Mundhir.” [Muslim] na katika mapokezi ya Ahmad imeendelea: “Naapa kwa Ambaye nafsi yangu imo Mikononi Mwake, Aayah hii ina ulimi na midomo miwili ambao inamtukuza Mfalme (Allaah) katika mguu wa Arsh.”  [Muslim (810), Swahiyh At-Targhiyb (1471)]

 

Anahimizwa kila Muislamu kuihifadhi na kuisoma nyakati nyingi kwani zimekuja Hadiyth nyingi juu ya fadhila zake. Miongoni mwa Hadiyth ni:

 

1-Kabla ya Kulala Kupata Hifadhi ya Shaytwaan:

 

Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kuisoma anapokuwa kitandani (kwa ajili ya kulala) hakika atakuwa katika hifadhi ya Allaah wala hatakaribiwa na shaytwaan mpaka kupambazuke” [al-Bukhaariy].

  

2-Kuisoma Asubuhi Na Jioni Kwa Ajili Ya Kinga;

 

“Atakayeisoma anapoamka asubuhi itamkinga na majini mpaka itakapofika jioni. Na atakayeisoma jioni atakingwa nao mpaka asubuhi.” [Al-Haakim (1/562) Taz. Swahiyh At-Targhiyb wat-Tarhiyb (1/273)]

 

Pia,

 

”Atakayezisoma mara tatu asubuhi na jioni  zitamtosheleza kwa kila kitu.” [Abuu Daawuwd (4/322) [5082], At-Tirmidhiy (5/567) [3575], Taz. Swahiyh At-Tirmidhiy (3/182)]

 

3-Kuisoma Kila Baada Ya Swalaah Kupata Kuingizwa Jannah:

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kuisoma baada ya kila Swalah hakitomzuia kuingia Jannah isipokuwa kifo”.  [Swahiyh Al-Jaami’ (5/339) [6464], na Silsilat Al-Ahaadiyth As-Swahiyhah (2/697) [972].

 

4-Ina Jina Tukufu Kabisa Ndani Yake Ambalo Unapoomba Hutakaqabaliwa:

 

Abuu Umaamah (Radhwiya Allaahu 'anhu)  amehadithia kwamba Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam)   amesema:  ”Jina Tukufu  kabisa la Allaah  Ambalo likiombewa kwalo Anaitikia limo katika Suwrah tatu; Al-Baqarah, Aal-‘Imraan, na Twaahaa’. [At-Tirmdhiy, Silsilah Asw-Swahiyhah (746)] Na mapokezi mengineyo yaliyothibitisha kuhusu Ismul-A’dhwam (Jina tukufu kabisa).

 

 

Na Hadiyth nyingine ni kule kufundishwa Abuu Hurayrah (Radhwiya-Allaahu ‘anhu) na shaytwaan kisha Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Amesema kweli japokuwa yeye ni muongo.” [Al-Bukhaariy na Muslim]     

 

Kwa hivyo hizi ni baadhi ya Hadiyth zinazoonyesha fadhila za Ayatul-Kursiy. Hakika itakuwa ni muhimu kwetu kuweza kuihifadhi na kuisoma kila wakati ambao umesuniwa kufanya hivyo ili tupate ulinzi na faida zake kutoka kwa Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)   

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share