Jimai: Kuzini Mchana Wa Ramadhwaan Na Usiku Wake Nini Hukmu Yake?
SWALI:
Kwanza natanguliza shukran zangu kwa mafunzo makubwa tunayopata katika jarida hili.
Swali langu najua kuzini ni dhambi kubwa, na ijapotokea mtu akazini aidha mchana wa ramadhani au usiku ni nini hukmu yake, na kuna tafauti yoyote baina ya mchana na usiku, katika tendo hilo katika mwezi huu. Natanguliza shukrani zangu.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihiwasallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Shukrani kwa swali lako zuri na kuwa umefahamu kuwa kuzini ni miongoni mwa madhambi makubwa. Hivyo, ndani ya Ramadhaan au nje yake Muislamu anafaa ajiweke mbali na kitendo hicho. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatuhimiza hata tusikaribie seuze kukifanya kitendo chenyewe. Allaah Aliyetukuka Anatuambia:
“Wala msikaribie uzinzi. Hakika huo ni uchafu na njia mbaya” (17: 32).
Adhabu yake pia ni kali kwa kufanya kitendo hicho kwani Allaah Aliyetukuka Anatuambia:
“Mzinifu mwanamke na mzinifu mwanamume, mtandikeni kila mmoja katika wao bakora mia. Wala isikushikeni huruma kwa ajili yao katika hukumu ya Allaah, ikiwa nyinyi mnamuamini Allaah na Siku ya Mwisho. Na lishuhudie adhabu yao kundi la Waumini” (24: 2).
Tufahamu kuwa hii ni adhabu kwa wanaofanya hivyo ikiwa hawajaoa au kuolewa.
Ipo nadharia miongoni mwetu kuwa zinaa haifai wakati wa Ramadhaan tu ikiwa ni usiku au mchana lakini hiyo ni nadharia potofu kama tulivyoonyesha hapo juu.
Ama ikiwa atazini usiku wa Ramadhaan atapata dhambi kubwa kwa kufanya kitendo hicho katika mwezi huo mtukufu. Kinachotakikana kufanya kwa sababu hakuna sheria ya Kiislamu katika nchi unayoishi na hata ulimwenguni leo hii, basi itabidi ufanye toba ya kweli kweli ili Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala)Akusamehe kosa hilo lako. Pia uwe umeweka moyoni kuwa lau kungekuwa na dola ya Kiislamu basi ningejipeleka kutwaharishwa na makosa hayo ya zinaa kwa kupewa adhabu inayostahiki kwa wazinifu.
Kitu ambacho unatakiwa kufanya kwa sasa ni kujuta kwa kitendo hicho ulichofanya, kujiondoa katika maasiya na kuazimia kutorudia tena uchafu huo. Pia unatakiwa kuongeza mambo mema, kutaka msamaha kutoka kwa Allaah na kurudi kwako katika njia njema na nzuri ya Allaah Aliyetukuka.
Ama ukifanya zinaa wakati wa mchana ya Ramadhaan basi umefanya makosa mawili makubwa sana. Ili upate msamaha kutoka kwa Allaah Aliyetukuka unatakiwa ufanye yale ya toba tuliyoyataja hapo juu. Mbali na hilo unatakiwa utoe kafara. Kafara ya hilo ni kumwacha mtumwa huru, ukitoweza basi ufunge miezi miwili mfululizo na ukitoweza ulishe masikini sitini. Hii ndiyo kafara ya kulala na mke wako wa halali na ndio kafara ya aliyezini vilevile ila kwa aliyezini kuna adhabu nyingineyo ya wazinifu kama kungekuwa kunafuatwa sheria ya Kiislam duniani.
Na Allaah Anajua zaidi