Mazungumzo Ya Nabii Musa Na Al-Khidhwr Katika Suratul-Kahf
Mazungumzo Ya Nabii Musa Na Al-Khidhwr Katika Suwrah Al-Kahf
SWALI:
Mimi Ningependa Kuuliza Suala Moja Tu. Katika Suwrah al-Kahf Kuna Masuala Ambayo Nabiy Muwsaa Alikuwa Anauliza Na Akipewa Majibu Na Yule Aliyefatana Nae. Tafadhali Naomba Ufafanuzi Wa Masuala Aliyokuwa Akiulizwa. Na Aliyemuuliza Ni Nani Yule?
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Hakika masuala hayo yanapatikana katika Suwrah Al-Kahf (18) ambayo Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametutaka tuwe tunaisoma kila Ijumaa ili tuepukane na fitina za Dajjaal. Masuala ambayo Nabiy Muwsaa (‘Alayhis-salaam) aliyomuuliza Khidhwr ni kama yafuatayo: Kwa nini akalitoboa jahazi, kumuua kijana asiye na hatia na kuusimamisha ukuta. Majibu ya masuala haya matatu yalikuwa:
أَمَّا السَّفِينَةُ فَكَانَتْ لِمَسَاكِينَ يَعْمَلُونَ فِي الْبَحْرِ فَأَرَدتُّ أَنْ أَعِيبَهَا وَكَانَ وَرَاءَهُم مَّلِكٌ يَأْخُذُ كُلَّ سَفِينَةٍ غَصْبًا ﴿٧٩﴾وَأَمَّا الْغُلَامُ فَكَانَ أَبَوَاهُ مُؤْمِنَيْنِ فَخَشِينَا أَن يُرْهِقَهُمَا طُغْيَانًا وَكُفْرًا ﴿٨٠﴾فَأَرَدْنَا أَن يُبْدِلَهُمَا رَبُّهُمَا خَيْرًا مِّنْهُ زَكَاةً وَأَقْرَبَ رُحْمًا ﴿٨١﴾وَأَمَّا الْجِدَارُ فَكَانَ لِغُلَامَيْنِ يَتِيمَيْنِ فِي الْمَدِينَةِ وَكَانَ تَحْتَهُ كَنزٌ لَّهُمَا وَكَانَ أَبُوهُمَا صَالِحًا فَأَرَادَ رَبُّكَ أَن يَبْلُغَا أَشُدَّهُمَا وَيَسْتَخْرِجَا كَنزَهُمَا رَحْمَةً مِّن رَّبِّكَ ۚ وَمَا فَعَلْتُهُ عَنْ أَمْرِي ۚ ذَٰلِكَ تَأْوِيلُ مَا لَمْ تَسْطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا ﴿٨٢﴾
Ama jahazi, ilikuwa ya masikini wanaofanya kazi baharini. Basi nikataka kuitia dosari kwani mbele yao alikuweko mfalme anayechukua kila jahazi kwa kupora. Na ama ghulamu, walikuwa wazazi wake wawili Waumini. Basi Tukakhofu asiwatie mashakani kwa upindukaji mipaka ya kuasi na kufuru. Tukakusudia Rabb wao Awabadilishie aliye bora zaidi kuliko yeye aliyetakasika na aliyekuwa karibu zaidi kihuruma. Na ama ukuta, ulikuwa ni wa ghulamu wawili mayatima katika mji ule, na kulikuweko chini yake hazina yao, na baba yao alikuwa mwema. Basi Rabb wako Alitaka wafikie umri wa kupevuka na watoe hazina yao; ni rahmah kutoka kwa Rabb wako. Na sikufanya hayo kwa amri yangu. Hiyo ni tafsiri ya hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavutia subira. [Al-Kahf: 79 – 82]
Aliyekuwa akimuuliza Nabii Muwsaa (‘Alayhis-salaam) ambaye ni Khidhwr wanazuoni wametofautiana kuhusu yeye alikuwa nani. Wengine wamesema kuwa alikuwa ni mja mwema kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa):
عَبْدًا مِّنْ عِبَادِنَا آتَيْنَاهُ رَحْمَةً مِّنْ عِندِنَ
Mja miongoni mwa waja Wetu (Khidhr), Tuliyempa rahmah kutoka Kwetu,.. [Al-Kahf: 65]
Na wengine wakasema kuwa alikuwa Nabii kwa kauli ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala):
..وَمَا فَعَلْتُهُ عَنْ أَمْرِي ۚ ذَٰلِكَ تَأْوِيلُ مَا لَمْ تَسْطِع عَّلَيْهِ صَبْرًا ﴿٨٢﴾
Na sikufanya hayo kwa amri yangu. Hiyo ni tafsiri ya hakika ya yale ambayo hukuweza kuyavutia subira. [Al-Kahf: 82]
Na Allaah Anajua zaidi