Swadaqah Inafaa Kumtolea Mama Yangu Aliyefariki?

Swadaqah Inafaa Kumtolea Mama Yangu Aliyefariki?

 www.alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Jirani yangu aliniuliza kuhusu mama yangu aliye fariki kama nimemtolea sadaka baada ya kufa mimi nikamjibu sikutoa sadaka yoyote, isipokua mimi nijuavyo kama ana deni inabidi nimlipie ikiwa deni hilo ni kwa binaadamu au kwa Allah na kama aliweka nadhiri kwa Allaah ya kufunga inabidi pia nimlipie kwa kufunga. Na zaidi na muombea dua yeye akanijibu haifai mtu akifiwa na mama yake inabidi amtolee sadaka ampelekee majuzuu na misahafu madrasa au msikitini sasa sijui uthibitisho wa hili.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Maiti ananufaika kwa yote yaliyopitishwa na Shariy’ah ya Kiislamu ima katika Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  na kwa mwongozo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Imepokewa na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kuwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Anapokufa mwana Aadam basi amali zake zote hukatika isipokuwa kwa mambo matatu: Swadaqah ya kuendelea, au elimu yenye manufaa au mtoto mwema anayemuombea” [Muslim].

 

Ukitazama kwa hakika mambo yote hayo ni katika juhudi alizofanya maiti kabla ya kufa kwake. Hivyo, ujira wake unamwendea akiwa kaburini mwake.

 

Pia maiti ananufaika kwa yafuatayo kama alivyotuashiria Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika kwa yanayomfuata Muumini kwa matendo na mambo mema baada ya mauti yake: Elimu aliyofundisha na kuieneza, mtoto mwema aliyemuacha, msahafu aliourithisha au Msikiti aliojenga, au nyumba kwa wapita njia aliyojenga, au swadaqah aliyoitoa kutoka katika mali yake katika hali yake ya afya na uhai wake. Zote hizo zinamfuata baada ya umauti wake” [Ibn Maajah na Ibn Khuzaymah, na Isnaad yake ni Hasan]

 

Hizi Hadiyth mbili zinatuonyesha mambo yanayomnufaisha Muislamu anapokufa kwa mambo aliyoyafanya akiwa hai.

 

Lakini zipo Hadiyth zinazotueleza kuwa mtoto anapomtolea mzazi wake aliyefariki swadaqah basi thawabu zinamfikia. Miongoni mwazo ni: Yupo mtu aliyemuuliza Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Hakika mamangu ameaga dunia, je itamfaa nikimtolea swadaqah?” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: “Ndio” [Al-Bukhaariy]

Imepokewa kuwa Sa‘ad bin ‘Ubaadah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) alisema: “Ee Rasuli wa Allaah! Hakika mamake Sa‘ad amekufa, je ni swadaqah ipi iliyo bora?” Akasema: “Maji”. Hivyo akachimba kisima akasema: “Cha mamake Sa‘ad” [Abu Daawuwd, at-Tirmidhiy, an-Nasaa’iy na Ibn Maajah].

 

Na katika Hadiyth nyengine alikuja mtu kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamuuliza: “Baba yangu amefariki na ameacha mali ambayo hakuusia chochote, je, nikitoa swadaqah mali hiyo atapata malipo kwayo?” Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akamjibu: “Ndio” [Muslim].

 

Hivyo yako mambo kadhaa ambayo yanamfaa maiti mojawapo ikiwa ni kumtolea swadaqah na pia kumuombea du’aa.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:  

 

‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

Share