Ameanza Ujenzi Wa Swadaqatun-Jaariyah Kwa Ajili Ya Mzazi Aliyefariki Kisha Akamalizia Mtu Mwengine Atataqabaliwa?

 

SWALI:

 

NAULIZA SWALI LANGU KUHUSU SADAKATUL JAARIYA.

 

MFANO MIMI NIMEMTOLEA MZEE WANGU ALIYEKWISHA KUFARIKI DUNIA VIFAA VYA KUJENGEA MSIKITI AU CHUO KWA AJILI YA SADAKATUL JAARIYA.  NA BAADA YA MUDA KAMA MIAKA MITATU (3) AKATOKEA MFADHILI MKUBWA KUJENGA MSIKITI HUO AU CHUO HICHO, NA IKABIDI KUVUNJWA WOTE, NA AKAANZA KUCHIMBA MSINGI MPYA NA KUTUMIA VIFAA VYENGINE KABISA BILA YA VILE VYA ZAMANI JE!!! HAPO ILE SADAKA YA MWANZO ILIYOTOLEWA PENGINE KWA KUCHANGIWA NA WENGI ITAENDELEA AU ITAKATIKA. NAOMBA KUFAHAMISHWA.

 


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri. Tufahamu kuwa hakuna amali inayofanywa kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka ikapotea bure. Kila amali inazawidiwa na Allaah Aliyetukuka kwa nia njema na ikhlasi. Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Hakika vitendo huzingatiwa kwa nia, na kwa hakika kila mtu atalipwa kwa nia yake" (al-Jama'ah, yaani Ahmad, al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaa'iy, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah).

 

Kwa ajili ya nia hiyo hata kama shughuli hiyo ya ujenzi haikumalizika bado thawabu utapata kwa juhudi na nia yako njema.

 

Kuhusu hili Hadiyth ya Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) iko wazi kabisa pale alipotuambia:

 

"Hakika Allaah Ameandika mambo mema na mabaya, kisha Ameyafafanua hayo kwa kusema kwamba mwenye kukusudia jambo jema na asilifanye Allaah Atamuandikia Kwake jema kamili" (al-Bukhaariy na Muslim).

 

Kwa hiyo, thawabu zako zipo kamili bila ya upungufu wala kasoro.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:  

 

‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share