Kupata Elimu Kwa Kutumia Uongo

SWALI:

 

Kama unaishi nchi za watu na unatumia jina na miaka ya uongo feki ukapata elimu ni haramu?


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kutumia uongo katika nchi za watu.

Uongo ni katika madhambi makubwa katika Uislamu na ni sifa ambayo Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema hawezi kuwa nayo Muislamu. Ni ajabu kuwa leo Waislamu leo tunaongoza katika kutumia majina na miaka feki ili tupate elimu na maslaha mengine katika nchi za ng’ambo.

 

Kufanya hivyo ni madhambi na itabidi Muislamu aliyefanya hilo arudi kwa Allaah Aliyetukuka kwa kuomba msamaha kwani Yeye ni Mwingi wa kusamehe. Elimu uliyopata tayari umeipata na huwezi kuirudisha, hivyo utabaki nayo na usome tena zaidi kwa njia ya halali angalau uweze kurekebisha yaliyopita.

 

Ikiwa ulifanya hivyo kwa kutokujua bila shaka utasamehewa na Allaah Aliyetukuka na ikiwa umefanya kwa elimu pia Allaah Aliyetukuka huenda Akakusamehe ikiwa utataka msamaha kisawa sawa na kikweli. Na usiache kuifuatlizia maovu hayo kwa mema kwa kuifanyia kazi elimu hiyo kuwasaidia Waislamu na kuunufaisha Waislamu huku ukikithirisha kuomba Maghfirah.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share