Hukmu Ya Kutazama Uchi Na Kulala Uchi Je, Kunaruhusiwa?
Hukmu Ya Kutazama Uchi Na Kulala Uchi Je, Kunaruhusiwa?
SWALI:
Assalam alaykum
Ninapenda kuuliza kwamba, hivi inaruhusiwa kujiangalia kwenye huku (sehemu za siri) ukiwa naked hasa mathalan baada ya kuoga? Na vilevile vipi kuhusu kulala naked kwenye chumba chako peke yako inaruhusiwa?
JIBU:
AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu kujitazama uchi na kulala uchi chumbani peke yako.
Hakika Uislamu una muongozo wake kuhusu mambo yote ya maisha yetu. Yapo mambo ambayo yanaruhusiwa katika Uislamu mbali na kuwa ni bora kutoyaendea.
Katika hayo ni kutazama uchi wako kukiwa na haja ya kufanya hivyo. Mfano ni kuwa baada ya kuoga unataka kuhakikisha kama umesafisha sehemu hizo za siri vyema, au ukiwa unajipaka mafuta n.k. Bila ya kuwa na sababu yoyote inakuwa si muruwa kujitazama.
Ama kulala uchi ukiwa peke yako, hakuna dalili kuwa imekatazwa. Lakini kufanya hivyo sio jambo jema, kwani huenda yakakukuta mauti katika hali hiyo ikawa aibu kwako watu watakapokukuta katika hali hiyo. Binaadamu anapaswa kujikirimu na kujiweka katika stara wakati wote. Na kujisitiri ni sifa ya wenye kuona hayaa, na kuona haya ni katika tabia njema iliyoamrishwa katika Uislamu na dalili ya iymaan:
عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رَضِيَ اللَّهُ عَنْهُ عَنْ النَّبِيِّ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ قَالَ ((الْإِيمَانُ بِضْعٌ وَسِتُّونَ شُعْبَةً وَالْحَيَاءُ شُعْبَةٌ مِنْ الْإِيمَانِ)) متفق عليه
Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: ((Iymaan ina matawi 63, na hayaa ni tawi la Iymaan)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Na asiyeona hayaa huenda akafanya lolote lile bila kujali:
عن أبي مَسْعُودٍ عُقْبَةَ بن عمرو الأَنْصَارِيّ البَدْرِيّ رضي اللهُ عنه قال : قالَ رسُولُ الله صلى الله عليه وسلم: ((إِنَّ مما أَدْرَكَ النَّاسُ مِنْ كَلامِ النُّبُوَّةِ الأولَى: إِذا لمْ تَسْتَحِ فاصْنَعْ ما شِئْتَ)) رَوَاهُ الْبُخَارِيُّ
Kutoka kwa Abu Mas'uwd 'Uqbah Ibn 'Amr Al-Answaariy Al-Badriy (Radhiya Allaahu 'anhu) ambaye amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kasema: Katika maneno ambayo watu waliyapata kutoka kwa Rusuli wa mwanzo (waliotangulia) ni: "Ikiwa huna hayaa basi fanya utakalo" [Al-Bukhaariy]
Ama ukiwa uko na mkeo hakuna tatizo lolote ukiwa na hakika hakuna mtoto au mtu mwengine ataingia katika chumba hicho na kukukuta katika hali hiyo.
Na Allaah Anajua zaidi