Inafaa Kufunga Swiyaam Na Kuswali Kwa Ajili Ya Aliyefariki?
Inafaa Kufunga Swiyaam Na Kuswali Kwa Ajili Ya Aliyefariki?
SWALI:
A.alaykum naomba kuulza mtu anaweza kumfungia na kusali kwa ajili y mtu aliyekufaa
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kuswali au kufunga Swawm kwa ajili ya maiti kutegemea thawabu zimfikie ni jambo lisilo katika Shariy’ah kwa sababu Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Anasema:
وَأَن لَّيْسَ لِلْإِنسَانِ إِلَّا مَا سَعَىٰ ﴿٣٩﴾
Na kwamba insani hatopata (jazaa) isipokuwa yale aliyoyafanyia juhudi.
وَأَنَّ سَعْيَهُ سَوْفَ يُرَىٰ ﴿٤٠﴾
Na kwamba juhudi yake itakuja kuonekana
ثُمَّ يُجْزَاهُ الْجَزَاءَ الْأَوْفَىٰ ﴿٤١﴾
Kisha atalipwa jazaa kamilifu. [An-Najm: 39-41]
Hivyo basi mwana Aadam anapofariki huwa ndio mwisho wa matendo yake isipokuwa yale ambayo imepatikana dalili kuwa yanamfaa kama yalivyotajwa katika Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam):
إذَا مَاتَ الإِنْسَانُ انْقَطَعَ عَمَلُهُ إلاَّ مِنْ ثَلاَثَةِ: إِلاَّ مِنْ صَدَقَةٍ جَارِيَةٍ، أَوْ عِلْمٍ يُنْتَفَعُ بِهِ، أَوْ وَلَدٍ صَالِحٍ يَدْعُو لَهُ
((Anapokufa mwana Aadam hukatika 'amali zake zote isipokuwa mambo matatu, swadaqah inayoendelea, au elimu yenye kunufaisha, au mtoto mwema anayemuombea)) [Al-Bukhaariy na Muslim]
Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:
‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu
Na Allaah Anajua zaidi