Kumfanyia Mzazi Aliyefariki Swadaqatun-Jaariyah Inakubalika? Thawabu Anapata Mzazi Au Mtoto?

 

 SWALI:

 Naomba tafadhali ufafanuzi wa suali langu hili linalonitatiza na tumebishana na jamaa hapa.

Ukimfanyie mzazi wako aliyefariki sadakat jariya kama kumjengea kisima cha maji au msikiti, je itakuwa ni amali yake mzazi? Kwa maana atakuwa anapata yeye thawabu za kuendelea zinazojulikana kuwa ni sadakat jariya? Au nitapata mimi thawabu hizo mtoto nnayemjengea? Nauliza kwa sababu hadithi inayosema – Amali za binadamu zinakatika isipokuwa mambo 3- sasa vipi mzazi akifarikia amali anayomtendea mwanawe itakuwa ni katika hayo mambo 3? Au haihesabiki kuwa ni amali yake?

 


 

 JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako zuri. Hiyo Hadiyth uliyoitaja ni sahihi, na kwa ukamilifu wake inasema:

 

"Anapokufa mwanadamu amali yake yote hukatika ila kwa mambo matatu: Sadaka yenye kuendela, elimu yenye manufaa na mtoto mwema anayemuombea du’aa" (Muslim).

 

 

Hata hivyo tufahamu kuwa hii si Hadiyth ya pekee kuhusu suala hili la sadaka ya kuendelea kwani yapo mambo mengine mengi ambayo mtoto anapomfanyia mzazi wake basi thawabu zake zinakwenda kwa mzazi huyo. Katika mambo ambayo mtoto anaweza kumfanyia mzazi na kumhijia, kumfungia ikiwa alikufa na deni na mengineyo.

 

Ukijenga Msikiti, kuchimba kisima, kujenga Madrsah kwa nia ya kumfanyia mzazi basi thawabu zinakwenda kwake. Dalili ya hili ni ile Hadiyth inayosema:

 

"Kulikuwa na mtu aliyemuuliza Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): 'Hakika mamangu amekufa, je, inamfaa kumtolea sadaka'. Akasema: 'Ndio" (al-Bukhaariy).

 

Naye Sa'ad bin 'Ubaadah (Radhiya Allaahu 'anhu) alisema:

 

"Ee Mtume wa Allaah! Hakika mamake Sa'ad ameaga dunia, ni sadaka gani iliyo bora?' Akasema: 'Maji'. Akachimba kisima na kusema: 'Cha mamake Sa'ad" (Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaa'iy na Ibn Maajah).

 

Kuchimba kisima kikawapatia watu maji ya kutumia kwa kunywa, kupikia n.k. ni katika sadaka nzuri inayomfaa maiti kutoka kwa mtoto wake. Watakuwa watu wamenufaika na maji kutokana na kisima ulichojenga, hivyo kwa kulinganisha ujenzi wowote unaonufaisha watu kama Msikiti, Madrassah, Shule, Maktaba n.k. itamfaa maiti.

 

Bonyeza kiungo kifuatacho kwa faida zaidi:  

 

‘Amali Za Kuwatendea Wazazi Waliofariki Waendelee Kupokea Thawabu

 

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share