Tajiri Anayetumia Pesa Kwa Kujionyesha

SWALI:

 

Kama tajiri anatoa zaka sadaka pesa nyingine anatumia kununulia magari ya kifahari, watu wanamuona na kumsifia inaswikh! Inshaallah Allah atuafikishe katika kila jambo la khayr.


 

JIBU

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola Mlezi wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa swali lako kuhusu tajiri anayetumia pesa zake kununua magari ya kifahari na mengineyo. Tunamuombea mtu huyo kama kweli yuko Amzidishie katika kutoa Zakaah na Swadaqah kwa ajili ya Uislamu. Kulingana na swali lako ni kuwa watu ndio wenye kusema wala sio yeye, kwa hivyo yeye hana makosa yoyote kuhusu hilo.

 

Jambo ambalo linakatazwa ni yeye mwenyewe kutoa kwa shughuli hizo, kama Zakaah na Swadaqah kisha akawa anahadithia na kujiona katika hilo. Na kujionyesha kawaida hakufichiki kabisa. Hivyo, akitoa kwa ajili ya Allaah Aliyetukuka na watu wenyewe wakawa wanahadithia, mwenye kutoa hatakuwa na makosa kabisa. Kununua magari ya fahari ikiwa unacho cha kununulia bila taklifu si kujionyesha pekee kama tunavyodhania. Lakini pia naye anapaswa achunge katika kufanya hivyo kujiingiza katika israfu, kwani Allaah Hawapendi wenye kufanya israfu na ubadhirifu.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share