SWALI:
Nilikua nikitamani mtoto nikaenda masjid kuswali kawaida nikamuona mwanamke aitwa Sultani akaniambia nitakuombea Allah upate nikamwambia INSHALLAH nikipata nitamwita jina lake Sultani. Nikapata mtoto lakini sikumwita hilo jina nilosema ndani ya masjid. Je itakua nimepata dhambi? Je itakua ni kama Nadhiri? Sikumwita kwa sababu mkwe wangu naye ni mzee alitoa jina. Sikuweza kumpinga. Nakutakia kila la kheir katika kumi la mwisho. ALLAH atutakabalie SWAUM na Ibadah zote AMIN. Ukhty in ISLAM. Jaazakallahul kheir
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola i wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho
Shukran kwa swali lako kuhusu mas-ala uliyoyataja. Hakika ni kuwa hilo ulilomwambia huyo dada Sultani si Nadhiri bali ni ahadi na ahadi ni deni. Uislamu umehimiza sana kwa mtu kuweza kutimiza ahadi anapotoa. Na ni mojawapo wa sifa ambazo Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Amemuahidi mja Wake Pepo ya Firdaws kama Anavyosema:
﴿ بِسْمِ اللّهِ الرَّحْمَنِ الرَّحِيمِ ﴾
قَدْ أَفْلَحَ الْمُؤْمِنُونَ ﴿1﴾ الَّذِينَ هُمْ فِي صَلَاتِهِمْ خَاشِعُونَ ﴿2﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَنِ اللَّغْوِ مُعْرِضُونَ ﴿3﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِلزَّكَاةِ فَاعِلُونَ ﴿4﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِفُرُوجِهِمْ حَافِظُونَ ﴿5﴾ إِلَّا عَلَى أَزْوَاجِهِمْ أوْ مَا مَلَكَتْ أَيْمَانُهُمْ فَإِنَّهُمْ غَيْرُ مَلُومِينَ ﴿6﴾ فَمَنِ ابْتَغَى وَرَاء ذَلِكَ فَأُوْلَئِكَ هُمُ الْعَادُونَ ﴿7﴾ وَالَّذِينَ هُمْ لِأَمَانَاتِهِمْ وَعَهْدِهِمْ رَاعُونَ ﴿8﴾ وَالَّذِينَ هُمْ عَلَى صَلَوَاتِهِمْ يُحَافِظُونَ ﴿9﴾ أُوْلَئِكَ هُمُ الْوَارِثُونَ ﴿10﴾ الَّذِينَ يَرِثُونَ الْفِرْدَوْسَ هُمْ فِيهَا خَالِدُونَ ﴿11﴾
KWA JINA LA ALLAH MWINGI WA REHEMA MWENYE KUREHEMU
1. HAKIKA wamefanikiwa Waumini
2. Ambao ni wanyenyekevu katika Sala zao
3. Na ambao hujiepusha na mambo ya upuuzi
4. Na ambao wanatoa Zaka
5.Na ambao wanazilinda tupu zao,
6. Isipokuwa kwa wake zao au kwa iliyowamiliki mikono yao ya kulia. Kwani hao si wenye kulaumiwa
7. Lakini anayetaka kinyume cha haya, basi hao ndio warukao mipaka.
8. Na ambao wanazitimiza amana zao na ahadi zao
9. Na ambao Sala zao wanazihifadhi
10. Hao ndio warithi
11. Ambao watairithi Pepo ya Firdaws, wadumu humo)) [Al-Mu'minuun:1-11]
Muislamu anatakiwa anapokuwa hana hakika na jambo kulitimiza basi ni afadhali sana asitoe ahadi. Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) Anasema: “Enyi mlioamini! Timizeni ahadi” (5: 1).
Na kuanzia mwanzo ungekuwa ni mwenye kumuambia nitamuita jina lako ikiwezekana kwani ulifahamu kuwa hujamshauri mke wako. Hivyo, jambo ambalo linatakiwa kwako ni kumtafuta huyo dada na kumwambia ukweli pamoja na kumtaka radhi kwa hilo na Insha’Allah atakuwa ni mwenye kukuelewa na kukusamehe. Pia taka msamaha kwa Allah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa kuleta istighfaar na kufanya mambo mema.
Na Allah Anajua zaidi