Anawaza Mambo Machafu Na Anakhofu Mauti; Afanyeje?

SWALI:

 

a.aleykum,kwanza nianze kwa kumshukuru mwenyezi mungu kwa rehma zake na utukufu wake,mimi ni msichana na umri wa miaka 21, mimi zamani nilikuwa sifati mambo ya dini japokuwa me ni muislamu, siku moja ni kenda kwa dada yangu akaweka dvd ya mtu alikuwa haswali ikaonyweshwa jinsi alivyokuwa anatolewa roho nikaogopa sana, basi alhamdulillah nikaanza kuswali na nikaacha mambo yote niliyokuwa nafanya kwa mara moja nilivoona tu hiyo dvd, lakini toka siku hiyo sina raha nikiswali nawaza mambo machafu namlani shetani lakini wapi muda mwingine inakuwa hivyo hivyo, halafu nakaa kwa kuogopa naona kama taondoka saa yeyote duniani hiyo inanipa shida sana miezi karibu 3 sasa nakaa kwa uoga sina raha. sasa nilikuwa nauliza nifanyeje dua gani niombe au nifanye nini nisikate tamaa ya kuishi,nisaidieni ndugu zangu.


 

 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

 

Tunapenda kukutanabahisha kwamba hiyo ni neema kutoka kwa Mola wako aliyekupatia njia ya kukuongoa kwa kukuwezesha kutazama jinsi mtu muovu anavyotolewa roho. Hivyo basi inapasa kumshukuru Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) kwa neema hiyo kwani sio kila mtu hujaaliwa hayo. Kama ulivyosema kuwa ulikuwa hufuati dini yako kisha ukapata sababu ya kujirekebisha.

 

Inavyoelekea hali yako sasa ni kuwa shaytwaan anataka kukupotoza kwani hiyo ndio kazi yake anapomuona mja yumo katika taqwa na anamkaribia Mola wake, humtia wasiwasi mja kwa kila njia, kama kumti mawazo machafu khaswa katika Swalah. Hivyo basi hiyo ni hali ya kawaida kwa mja yeyote, isikutiie wasi wasi  na wala usimuendekeza shaytwaan akakutoa katika njia uliyoanza kuelekea.

 

Hali kadhalika kukhofu mauti na kukosa raha inaweza kuwa ni khofu ya kukutana na Mola wako na hali hujakuwa tayari kwa kufanya mema mengi kwa vile hukuwa mwanzo mtu wa kufuata dini. Hii pia ni alama ya kumkhofu Allaah na kuongezeka taqwa na iymaan. Huenda pia ikawa ni wasiwasi huo huo wa shaytwaan, anazokutia ili ukose raha, uone dhiki na ujitie mashaka katika ibada zako. Linalokupasa kufanya ni yafuatayo ili ubakie salama Insha-Allaah.

 

  1. Kila zikikujia fikra mbovu, jikinge na Allaah kutokana na shaytwaan kwa kusema: A'uudhu BiLLaahi mina-shaytwaanir-rajiym'. Hata katika Swalah anapokujia kukutia wasiwasi pia unaweza kusema kauli hii kwa kutema mate mara tatu upande wa kushoto.

 

  1. Soma sana Qur-aan

 

  1. Dumisha Adhkaar  za asubuhi na jioni ambazo zinapatikana katika kitabu cha Hiswnul-Muslim kinachouzwa kwa bei ndogo kabisa. Kudumisha hizi Adhkaar ni kinga kubwa kabisa na shaytwaan na kila shari. Nacho kinapatikana Alhidaaya katika viungo vifutavyo:

 

Hiswnul-Muslim: Du’aa Na Adhkaar Kusoma Na Kwa Kusikiliza (Toleo Lilohaririwa)

 

 

027-Hiswnul-Muslim: Nyiradi Za Asubuhi Na Jioni

 

 

  1. Soma makala zilizomo Alhidaaya na sikiliza mawaidha ambayo yamejaa tele Alhidaaya, yatakuburudisha na kukuliwaza.

 

  1. Amka usiku wa manane umuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta'ala) Akuondoshee mbali ibliys anayekutia wasiwasi. Pia tumia nyakati za kukubaliwa du'aa kama baina ya Adhaan na Iqaamah, inaponyesha mvua, unapokuwa katika Swawm n.k.

 

 

Tunakuombea Allaah Akuondoshee dhiki na Akuondoshee wasiwasi wa shaytwaan na Akufunulie moyo wako.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share