Swalah Na Du’aa Zipi Za Kusoma Unapotaka Kutubu?

 

SWALI:

 

Mimi ni msichana wa kiislam nina umri wa miaka 25 naomba mnisaidie nahitaji kujua dua za kuomba na sala za kusali kwaajili ya kutubu madhambi yangu kwa Allah.nahitaji kurudi kwa mola wangu

 wabillahi Tawfiq  

 


 

JIBU:

 

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho. 

Tumepokea swali lako na tumefurahi sana kuona kwamba wako ndugu zetu kama wewe wenye kufanya makosa lakini AlhamduliLLaah wanatambua makosa yao na kutaka kurudi kwa Mola wao. Kwa hiyo tambua kuwa hiyo ni neema kwako kutoka kwa Mola wako kwamba Amekupenda hadi Akakuonyesha uongofu wa kutambua makosa yako hata utukabili sisi utake kujua vipi utubu.  

Hivyo, jambo la kwanza linalokupasa ni kumshukuru Allaah (Subhaanahu Wa Ta'alaa) kwa Kukuzindua ukatambua kuwa uko makosani kabla ya adhabu Yake au mauti kukufika. Vile vile kupata uongofu katika umri kama huo pia ni jambo la kumshukuru Allaah kwani wengi huendelea na maasi na kuendelea kuchuma madhambi hadi wanafikia katika umri mkubwa. Yote hayo ni neema kutoka kwa Mola wako unapasa umshukuru sana kila wakati. 

Kuomba Maghfirah unaweza kuswali Rakaa mbili tu kwa nia moyoni ya kuomba Tawbah kwa Mola wako kama utakavyoona dalili katika mada za Tawbah tunazokuwekea viungo vyake chini. 

Ama du’aa, ziko mbali mbali ambazo hata Mitume waliomba walipokuwa wakifanya makosa au katika kawaida ya kumdhukuru Allaah, pamoja na adhkaar mbali mbali alizotufunza Mtume (Swallah Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)

 

Du’aa ifuatayo ambayo inaitwa ‘Sayyidul-Istighfaar’ (Bwana wa Kuomba Maghfirah) inapasa uisome kila mara na katika usimulizi Swahiyh ni kwamba pindi ukiisoma asubuhi ikawa ni ajali yako kuondoka duniani basi utaingia Peponi. Na pindi ukiisoma jioni ikawa usiku huo ni siku ya kuondoka duniani basi utaingia Peponi. Hivyo inampasa kila Muislamu awe anaidumisha du’aa hii kila siku asubuhi na jioni:

 

اللّهـمَّ أَنْتَ رَبِّـي لا إلهَ إلاّ أَنْتَ ، خَلَقْتَنـي وَأَنا عَبْـدُك ، وَأَنا عَلـى عَهْـدِكَ وَوَعْـدِكَ ما اسْتَـطَعْـت ، أَعـوذُبِكَ مِنْ شَـرِّ ما صَنَـعْت ، أَبـوءُ لَـكَ بِنِعْـمَتِـكَ  عَلَـيَّ وَأَبـوءُ بِذَنْـبي فَاغْفـِرْ لي فَإِنَّـهُ لا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْتَ .

‘Allaahumma Anta Rabiiy laa Ilaaha illa Anta Khalaqtaniy wa ana ‘Abduka wa ana ‘alaa ‘Ahdika  wa Wa’dika mastatwa’tu, A’uudhu Bika min sharri maa Swana’tu, abu-u Laka Bini’matika ‘alayya wa abu-u bidhanbiy, Faghfir-liy fainnahu laa yaghfirudh-dhunuuba illa Anta’

Ee Allaah! Wewe ni Mola wangu, hapana muabudiwa wa haki ila Wewe, Umeniumba mimi na mimi ni mja Wako, nami niko juu ya  ahadi Yako, na agano Lako, kiasi cha uwezo wangu, najilinda Kwako kutokana  na shari ya nilichokifanya, nakiri  Kwako kwa Kunineemesha, na nakiri kwa madhambi yangu, basi nakuomba Unisamehe kwani hasamehe madhambi ila Wewe”

 

Vile vile:

 

Du’aa ya kusoma baada ya Tashahhud na kabla ya kutoa Salaam katika Swalah:

 

اللّهُـمَّ إِنِّـي ظَلَـمْتُ نَفْسـي ظُلْمـاً كَثـيراً وَلا يَغْـفِرُ الذُّنـوبَ إِلاّ أَنْت ، فَاغْـفِر لي مَغْـفِرَةً مِنْ عِنْـدِك وَارْحَمْـني، إِنَّكَ أَنْتَ الغَـفورُ الرَّحـيم

Allaahuuma inniy dhwalamtu nafsiy dhwulman-kathiyran wa laa yaghfirudh-dhunuuba illa Anta. Faghfir-liy maghfiratam-min ‘Indika War-Hamniy, Innaka Antal-Ghafuurur-Rahiym.

‘Ee Allaah  hakika mimi nimejidhulumu nafsi yangu, dhulma kubwa, na hasamehe madhambi ila Wewe, basi nisamehe msamaha kutoka Kwako, na Unirehemu, hakika Wewe  ni mwingi wa kusamehe, mwingi wa kurehemu’

 

Zifuatazo pia ni du’aa chache kutoka katika Qur-aan ambazo tunazinukuu kwa wepesi wako, lakini ingia katika kiungo kifutacho utapata zaidi ya hizo:

 

Duaa Za Qur-aan Maana na Matamshi Yake

 

 

Du’aa aliyoomba baba yetu Aadam alipofanya makosa ya kumfuata ibliys.

 

رَبَّنَا ظَلَمْنَا أَنفُسَنَا وَإِن لَّمْ تَغْفِرْ لَنَا وَتَرْحَمْنَا لَنَكُونَنَّ مِنَ الْخَاسِرِينَ   

Rabbanaa (Mola wetu)! Tumedhulumu nafsi zetu, na basi Usipotughufuria na Ukaturehemu; bila shaka tutakuwa miongoni mwa waliokhasirika.”  [Al-A'araaf: 23]  

 

Du’aa Ya Nabii Yuunus (‘Alayhis-Salaam) alipokuwa tumboni mwa nyangumi:

 

لا إِلَهَ إِلا أَنتَ سُبْحَانَكَ إِنِّي كُنتُ مِنَ الظَّالِمِينَ 

“(hakuna muabudiwa wa haki isipokuwa Wewe, Utakasifu ni Wako, hakika mimi nilikuwa miongoni mwa madhalimu).” [Al-Anbiyaa: 87]  

 

 

رَبَّنَا لاَ تُؤَاخِذْنَا إِن نَّسِينَا أَوْ أَخْطَأْنَا رَبَّنَا وَلاَ تَحْمِلْ عَلَيْنَا إِصْرًا كَمَا حَمَلْتَهُ عَلَى الَّذِينَ مِن قَبْلِنَا رَبَّنَا وَلاَ تُحَمِّلْنَا مَا لاَ طَاقَةَ لَنَا بِهِ وَاعْفُ عَنَّا وَاغْفِرْ لَنَا وَارْحَمْنَا أَنتَ مَوْلاَنَا فَانصُرْنَا عَلَى الْقَوْمِ الْكَافِرِينَ  (البقرة 286)

Rabbanaa (Mola wetu) Usituchukulie tukisahau au tukikosea. Rabbanaa (Mola wetu), Usitubebeshe mzigo kama Ulivyoubebesha juu ya wale waliokuwa kabla yetu. Rabbanaa (Mola wetu), Usitutwike tusiyoyaweza, na Tusamehe, na Tughufurie na Turehemu, Wewe ni Mawlaa (Mlezi, Mlinzi, Msimamizi) wetu, basi Tunusuru dhidi ya watu makafiri. [Al-Baqarah: 286]

 

Na muhimu zaidi ya hayo ni kuwa usome mada zinazohusu Tawbah, vipi kufanya Tawbah, masharti yake na fadhila zake ambazo zote utazipata katika kiungo kifuatacho:

 

 

 Tawbah

 

Nataka Kutubia...lakini!!

 

Toba Na Maghfira

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Azidi Kukupa uongofu ubakie katika taqwa na uwe miongoni mwa waja Wake wema. Aamiyn.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share