Ununuzi Kwa Njia Ya Ushindani (Mnada)

 

SWALI:

 

Pili, ni suala la kununua kwa njia ya ushindani maarufu kama mnada huku kwenu, tena basi, kwa mfano, mnunuzi ananukua nyumba ya Muislamu aliyeshindwa kulipa mkopo uliotolewa kwa njia ya ribaa, na nyumba yake imebidi iuzwe kwa kushindwa kurejesha deni hilio. Je, inaswihi kwa Muislamu kununua hiyo nyumba, tena basi ktk utaratibu wa ushindani wa kupandishiana bei?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Shukrani zetu za dhati kwa ndugu yetu muulizaji swali. Awali ya yote hayo tufahamu kuwa hili Muislamu analopata kwa kuuziwa nyumba yake kwa njia hiyo ni adhabu kwake hapa hapa duniani kwa sababu ya kukiuka mipaka ya Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) kwa kuendea madhambi makubwa.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema kuhusu ulaji wa ribaa:

Wale walao ribaa hawasimami ila kama anavyosimama aliyezugwa na Shaytwaan kwa kumgusa. Hayo ni kwa kuwa wamesema: Biashara ni kama ribaa. Lakini Allaah Ameihalalisha biashara na Ameiharimisha ribaa” (2: 275).

 

Na Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia dhambi hilo la ribaa pale aliposema:

Allaah Amemlaani mwenye kula ribaa, mwenye kuitoa, mashahidi wake na mwandishi wake(Ahmad, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy, an-Nasaaiy na Ibn Maajah).

 

Mbali na makosa yaliyofanya na Muislamu huyo kwa kuchukua mkopo wa ribaa Waislamu wanatakiwa wamsaidie, hasa wale wenye uwezo kwa kumkopesha bila ribaa ili alipe polepole. Haifai kwa Muislamu kuchukua hiyo ni fursa ya kuweza kupata haki ya mwenziwe. Ndio Uislamu ukaweka fungu moja la Zakaah ni kuweza kusaidia watu walioingia katika deni na kisha kushindwa kulipa. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Na wenye madeni” (9: 60).

 

Ama tukija katika mas-ala ya mnada ni kuwa Uislamu umeikubali biashara inayofanywa kwa njia hiyo kwani hiyo ni fursa kuwakutanisha baina ya wauzaji na wanunuzi na wote wawili huwa wakisahilishiwa kupata bidhaa wanazohitajia. Hivyo, hata mtu anayefanya kazi ya udalali anaweza kuchukua ujira kwa kazi anayoifanya kwa maelewano walioekeana na yule anayetaka kuuziwa bidhaa yake/ zake.

 

Hata hivyo, udalali unaruhusiwa ikiwa masharti yafuatayo yatatimizwa:

 

  1. Asimdanganye mmoja katika wafungao mkataba kwa ajili ya mwenzake au kwa jili yake mwenyewe;
  2. Achukue ujira wa kutosheleza juhudi yake bila udanganyifu wala unyonyaji.

 

Mbali na hayo masharti yanayomhusu dalali inafaa shughuli yenyewe ili iwe halali kusiwe na najash. Neno hilo limefasiriwa na Ibn ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ifuatavyo, ni kuipa bidhaa bei kubwa kuliko thamani yake bila kukusudia kununua, ili wengine nao wazidishe kupandisha kwa ajili ya mashindano, na mara nyingi huwa ni kuafikiana kuwahadaa wengine, hasa katika mnada. Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu hilo anatuambia:

Msihusudiane, wala msiongezeane bei (pasina kuwa na haja ya kununua), wala msichukiane, wala msipeane nyongo, wala wasinunue baadhi yenu kilichokwisha kuuziwa wenzenu, lakini kuweni enyi waja wa Allaah ndugu. Muislamu ni ndugu wa Muislamu: hamdhulumu, wala haachi kumsaidia wala hamdanganyi wala hamdharau(Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya Allaahu ‘anhu]).

 

Hakika Hadiyth iliyopo juu inatujibia swali letu barabara nasi kama ndugu moja inatakiwa tusaidiane kwa njia iliyo bora. Hakuna njia iliyo bora kama kumtoa nduguyo katika matatizo. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:

Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah” (5: 2).

 

Tufahamu kuwa usaidizi huo hauruki patupu kwani Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuambia:

Mwenye kumuondolea Muumini shida miongoni mwa shida za ulimwengu, Allaah Atamuondolea shida miongoni mwa shida za Siku ya Qiyaama. Na mwenye kumsahilishia mwenye mazito, Allaah Atamsahilishia mazito yake duniani na Aakhirah, na mwenye kumsitiri Muislamu, Allaah Atamsitiri duniani na Aakhirah” (Muslim kutoka kwa Abu Hurayrah [Radhiya Allaahu ‘anhu]). Je, zipo fadhila kama hizo? Hivyo, Muislamu anafaa amfikirie mwenziwe mwenye matatizo.

 

Mbali na kusema hayo Muislamu anaweza kununua bidhaa kama hiyo inayouzwa ikiwa hakutakuwa na najash na kukiwa na hofu ya kwamba waliopo kwenye mnada ni mchanganyiko Waislamu na wasiokuwa Waislamu. Huenda ikiachiliwa basi nyumba hiyo inaweza kwenda kwa asiyekuwa Muislamu.

 

Hata hivyo, kumsaidia katika tatizo ndio vyema na uzuri zaidi.

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share