Ninafanya Kazi Ya Kuchinja Nguruwe, Je, Halali?

 

SWALI:

Assalam alaikum wa rahamatullahi, ama baada ya salama ndugu wahusika niomba kuulizwa swali langu ambalo lina nisumbua kichwa kwa muda mrefu.

Mimi ni mvulana wa ki-islam ninaeshi hapa NEW ZEALAND nilijitahidi kila njia kutafuta kazi ila sikupata kwa muda wa miaka 2 hivyo nikalazimika kutafuta kazi yoyote ile kulingana na ugumu wa maisha, nilijaliwa kupata kazi katika sehemu ya vichinjoni (sehemu ya kuchinja). Tatizo ni moja hapo nalazimika kufanya kazi ya kucuna NGURUWE na japokua mimi ni muislam. Nimelazimika kufanya kazi hiyo kwa shingo upande kwani nikitoka kazini inabidi njitwarishe na kuanza ku sali. Sasa hukumu ni ipi muislam kutumika katika mambo ya nguruwe? Naomba kujua kuhusu jambo hilo jee ibada zangu zinakubaliwa au vipi???

    


 

 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Nyama ya nguruwe tunajua kwamba ni haraam kwa Waislamu kwa sababu Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

 

 

((قُل لاَّ أَجِدُ فِي مَا أُوْحِيَ إِلَيَّ مُحَرَّمًا عَلَى طَاعِمٍ يَطْعَمُهُ إِلاَّ أَن يَكُونَ مَيْتَةً أَوْ دَمًا مَّسْفُوحًا أَوْ لَحْمَ خِنزِيرٍ فَإِنَّهُ رِجْسٌ أَوْ فِسْقًا أُهِلَّ لِغَيْرِ اللّهِ بِهِ فَمَنِ اضْطُرَّ غَيْرَ بَاغٍ وَلاَ عَادٍ فَإِنَّ رَبَّكَ غَفُورٌ رَّحِيم))

 

((Sema: Sioni katika yale niliyofunuliwa mimi kitu kilicho harimishwa kwa mlaji kukila isipokuwa kiwe ni nyamafu, au damu inayomwagika, au nyama ya nguruwe, kwani hiyo ni uchafu; au kwa upotofu kimechinjwa kwa jina la asiyekuwa Allaah. Lakini mwenye kushikwa na dharura, bila ya kutamani wala kupita mipaka, basi hakika Mola wako  ni Mwenye kusamehe, Mwenye kurehemu)) [Al-An-'aam: 145]

 

Hakika ni kuwa kitu chochote ambacho ni haramu kutumia basi kula thamani yake pia inakuwa haramu. Mfano huu ni kama ule wa pombe ambao Mtume صلى الله عليه وآله وسلمamekataza kubebwa, kutengeneza, kunywa, kula thamani yake, na kadhalika.

Vile vile Mtume صلى الله عليه وآله وسلم ametufundisha kanuni muhimu aliposema:

 ((إن الله إذا حرَّم شيئاً حرَّم ثمنه))    رواه أبو داود  وصححه الشيخ الألباني في " غاية المرام "

((Allaah Anapoharamisha kitu, basi (pia) Huharamisha thamani yake)) [Abu Daawuud na ameipa daraja ya Sahiyh Shaykh Al-Albaaniy katika  Ghaayat al-Maraam]

Na katika hadiyth nyingine:

 

 

عن جابر بن عبد الله رضي الله عنهما أنه سمع رسول الله صلى الله عليه وسلم يقول عام الفتح وهو بمكة : (( إن الله ورسوله حرم بيع الخمر والميتة والخنزير والأصنام )) . فقيل : يا رسول الله ، أرأيت شحوم الميتة فإنها يطلى بها السفن ويدهن بها الجلود ، ويستصبح بها الناس ؟ فقال : (( لا ، هو حرام )) . ثم قال رسول الله صلى الله عليه وسلم عند ذلك : (( قاتل الله اليهود إن الله لما حرم شحومها جملوه ثم باعوه فأكلوا ثمنه)) . رواه البخاري ومسلم    

Imetoka kwa Jaabir ibn 'Abdullah  رضي الله عنهما kwamba amemsikia Mtume صلى الله عليه وآله وسلم alipokuwa Makkah wakati wa ushindi akisema: ((Allaah na Mtume Wake Wameharamisha uuzaji wa pombe, nyamafu, nguruwe na masanamu)) Ikasemwa: "Ewe Mjumbe wa Allaah, unaonaje ikiwa ni mafuta ya mnyama aliyekufa kwani merikebu (meli) zinakalafatiwa nayo na ngozi ya mnyama inapakwa nayo na watu wanatumia kuwashia taa zao"? Akasema: ((Hapana! Ni haraamu)) Kisha Mtume صلى الله عليه وآله وسلم akasema: ((Allaah Awalaani Mayahudi kwani Allaah Alipowaharamishia mafuta ya mnyama, waliyayusha na kuyauza na kutumia thamani yake)) [Al-Bukhaariy na Muslim]  

Na kufanya kazi ya kuchinja na kuchuna nguruwe haifai kwa Muislamu kwani huko kutakuwa ni kusaidia katika ubaya na uovu. Anatakiwa Muislamu azuie kadiri awezavyo jambo hilo la haramu hata kama ni biashara ya makafiri. Allaah سبحانه وتعالى Anasema:

 

 

((وَتَعَاوَنُواْ عَلَى الْبرِّ وَالتَّقْوَى وَلاَ تَعَاوَنُواْ عَلَى الإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ وَاتَّقُواْ اللّهَ إِنَّ اللّهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ))

))Na saidianeni katika wema na ucha Mungu. Wala msisaidiane katika dhambi na uadui. Na mcheni Allaah. Hakika Allaah  ni Mkali wa kuadhibu)) [Al-Maaidah:2]  

Vile vile kuchinja huko na kugusa damu na nyama ya nguruwe ni najis na hivyo inakubidi uwe unajitia tohara kila unapotaka kuswali.

Nawe tayari umeshaingiwa na shaka na jambo hilo basi hilo lilikutosha wewe kujiweka mbali na jambo hilo tangu awali kama alivyosema Mtume صلى الله عليه وآله وسلم   

 

 

عن النّوَّاسِ بْنِ سَمْعَانَ رضيَ اللهُ عَنْهُ عن النَّبي صلى الله عليه وسلم قَالَ: ((الْبِرُّ حُسْنُ الْخُلُقِ، وَالإِثْمُ مَا حاكَ في نَفْسِكَ وَكَرِهْتَ أَنْ يَطَّلِعَ عَلَيْهِ النَّاسُ))  رَوَاهُ مُسْلِمٌ  .

وعن وَابصَةَ بْنِ مَعْبَدٍ رضي اللهُ عَنْهُ قالَ:   قالَ رَسُولَ اللهِ صلى الله عليه وسلم   ((جِئْتَ تَسأَلُ عَنِ الْبِرِّ؟))  . قُلْتُ: نَعَمْ.  قَالَ: ((اسْتَفْتِ قَلْبَكَ، الْبِرُّ مَا اطْمَأَنَّتْ إلَيْهِ النَّفْسُ وَاطْمَأَنَّ إلَيْهِ الْقَلْبُ، وَالإِثْمُ مَا حاكَ في النَّفْسِ وَتَردَّدَ في الصَّدْرِ وَإنْ أَفْتَاكَ النّاسُ وَأَفْتَوْكَ)) حَدِيثٌ حَسَنٌ، رَوَيْنَاهُ في مُسْنَدَي الْإِمَامَيْنِ أَحْمَدَ بْنِ حَنْبَلٍ وَالدَّارِمِيّ   بِإِسْنَادٍ حَسَنٍ. 

 

Kutoka kwa An-Nawwaas Ibn Sam'aan رضي الله عنه  ambaye alisema kuwa Mtume صلى الله عليه وسلم  kasema: ((Uadilifu  ni tabia nzuri na udhalimu ni kile kitu ambacho huyumbayumba (chenye mashaka) katika nafsi yako na hupendelei watu kulitambua))  [Imesimuliwa na Muslim]

Na kutoka kwa Waabisah Ibn Ma'abad رضي الله عنه  ambaye alisema: "Nilikuja kwa Mtume صلى الله عليه وسلم naye akasema: ((Umekuja  kuuliza juu ya uadilifu?)) Nikasema: Ndio. Akasema:  ((Ushaurishe  moyo wako. Uadilifu ni kile ambacho nafsi yako inakihisi shwari na moyo wako pia unahisi shwari, na udhalimu ni kile kinachoyumbayumba katika nafsi na kwenda na kurudi kifuani ijapokuwa watu wamekupa shauri lao la kisheria)) (kukipendelea) [Hadiyth hasan katika musnad ya Imaam Ahmad bin Hanbal na Ad-Daaramiy kwa isnaad ya hasan].

 

Kwa hiyo kuiacha kazi hiyo ni bora kwako na utafute nyingine na uwe na tawakkul na Allaah سبحانه وتعالى  kuwa unapoacha jambo kwa ajili Yake basi Atakupa lililo bora zaidi ya hilo.   

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

 

Share