Posho Nje Ya Mshahara

Posho Nje Ya Mshahara

Alhidaaya.com

 

 

 

SWALI:

 

 Assalamu alaykum;

Nabii Salla Allaahu alayhi wa sallaam amesema "Tumtumiaye kwenye kazi na tukampa rizki (mshahara) basi achukuacho juu ya hapo huwa ni haramu" Imesimuliwa na Abu Daud.

Suala langu la kwanza ni kuwa jee hizi posho zinazolipwa na Serikali kwa wafanyakazi ni halali? Posho ninayozungumzia hapa ni ile inayolipwa kiwango kadhaa na mwezi mwengine ukalipwa zaidi au chini ya kile cha mwezi uliopita. Na huenda ukalipwa mara moja au zaidi kwa mwezi mmoja. Posho hiii haipo fixed kama vile posho ya nyumba, usafiri, n.k ambayo inalipwa kila mwezi na ipo ndani ya mshahara wa mwezi. Sababu kuu inayotumiwa hapa ni kuwa mshahara wa mwezi ni mdogo hautoshelezi na wakuu wote wa juu wanaridhia hilo (posho). Posho hii huenda ikawa kubwa kuliko ule mshahara wa mwezi anayolipwa mfanyakazi.

 

Suala la pili linaloambatana hapa ni kwa ile posho ambayo inatolewa kwa semina, sikukuu, ziara na kadhalika inakubalika kupokewa?

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Hakika ni kuwa Hadiyth iliyo hapo juu ipo wazi na huenda kuandikwa hapo haijaeleweka vizuri. Hapa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yupo wazi kabisa kuwa mfanya kazi atakuwa ni mwenye kupatiwa mshahara kwa kazi anayopatiwa.

 

Katika Hadiyth nyengine mfanya kazi apewe haki yake kabla ya jasho lake halijakauka:  

 

وَعَنْ اِبْنِ عُمَرَ رَضِيَ اَللَّهُ عَنْهُمَا قَالَ: قَالَ رَسُولُ اَللَّهِ صَلَّى اللهُ عَلَيْهِ وَآلِهِ وَسَلَّمْ  {أَعْطُوا اَلْأَجِيرَ أَجْرَهُ قَبْلَ أَنْ يَجِفَّ عَرَقُهُ} رَوَاهُ اِبْنُ مَاجَهْ 

Kutoka kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mumpeni muajiriwa malipo yake kabla jasho lake kukauka. [Imetolewa na Ibn Maajah]

 

Ikiwa mfanya kazi huyu anapatiwa haki yake kikamilifu kwa nini achukue bila kuridhiwa kufanya hivyo. Sehemu ya pili ya Hadiyth inasema: “Achukuacho juu ya hapo…”, hii ina maana ya kwamba yule mfanya kazi ambaye atachukua kwa kuiba au kwa udanganyifu au kwa njia nyengine yoyote ya haraam basi pato hilo litakuwa haraam kwake.

Hii inaweza kufafanuliwa na Hadiyth nyengine ambayo inasema: “Mtu yeyote anayetufanyia kazi, ikiwa hana mke, atapata mmoja; ikiwa hana makazi, tutampatia; ikiwa hana mtumishi, tutampatia; ikiwa hana kipando (usafiri), tutampatia”. Si hivyo tu hata wasiokuwa Waislaam katika dola ambao walikuwa hawajiwezi walisaidiwa na dola ili waweze kujikimu kimaisha.

 

Mara zote kazi za serikali zinakuwa ni za mapatano, na ipo kanuni katika Uislaam inayosema: “Waislamu wapo juu ya masharti waliyowekeana”. Ikiwa upo mkataba kama huo baina ya mwajiri na mwajiriwa basi hakuna tatizo lolote kwani pande zote mbili zitakuwa zimeelewana.

 

Lakini hii sababu ambayo imetolewa hapa haingii akilini, kwa nini wasiongeze mshahara na wakapunguza posho. Labda hapa kubainishwe zaidi kwani huenda jambo hili likawa linafanyika zaidi huko uliko na sio katika maeneno mengine.

 

Ama kuhusu swali la pili, posho aina hiyo haina tatizo lolote kwani katika semina utakuwa umefanya kazi ya ziada au umetoa mada na katika kanuni huwa unapatiwa chochote kwa hayo.

 

Ama posho wakati wa sikukuu au kwa yule anayefanya kazi nzuri ni motisha kwa wafanyakazi ili waimarishe kazi zao. Hivyo kupokea hakuna tatizo lolote.

 

Na Allah Anajua zaidi

 

 

 

Share