Al-Mas-hu ‘Alal Khuffayn (Kupangusa Juu Ya Khufu Mbili) Kwa Ajili Ya Wudhuu
Al-Mas-hu ‘Alal Khuffayn (Kupangusa Juu Ya Khufu Mbili)
Kwa Ajili Ya Wudhuu
SWALI LA KWANZA:
Tunawaombea Alhidaaya uwezo wa kujibu maswali yetu kwani tunafaidika na mengi tusiyoyajua.
Nimesikia kuwa unaweza kufanya wudhu wa sala bila ya kuosha miguu na badala yake uvae soksi na upanguse kwa maji. Je ni kweli? Na hata kama umekwenda haja kubwa na ndogo wudhu humo miguuni utakuwa haujavunjika? Na ni muda gani unaweza kufanya hivo? Na vipi kufuta hizo soksi. Nitashukuru kupata jibu. Asala aleikum
SWALI LA PILI:
Naomba kujua kwa hali ya kawaida mtu anaruhusiwa kusali akiwa amevaa soksi pamoja na kutawadha kwa kupitisha maji chini ya soksi hizo.
JIBU:
Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote, Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani zetu za dhati kwa ndugu muulizaji swali. Suala la kupangusa juu ya soksi ni katika jambo ambalo linaondoa uzito kwa Muislamu pindi anapokuwa anataka kutekeleza Ibaadah ya Swalah. Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) Anatueleza kuhusu usahali na wepesi wa Dini hii inayokwenda sambamba na maumbile ya mwanaadamu:
“Wala hakuweka juu yenu mambo mazito katika Dini” (22: 78).
Ama kupangusa kwenye soksi ina masharti yake ambayo yanafaa kutimizwa ili kupangusa huko kuwe sahihi kabisa. Kupangusa huko ni kweli kabisa kwani kumo katika sheria hii ya Uislamu.
Ama kuhusu masharti ambayo yanafaa yatekelezwe ni:
- Inatakiwa uvae soksi ukiwa na wudhuu, ndipo unapotenguka ima kwa kwenda haja kubwa au ndogo au kutokwa na upepo ndipo unapoweza kupangusa.
- Kwa mwenyeji anaweza kupangusa juu ya soksi kwa masaa 24 ilhali msafiri ameruhusiwa kwa masaa 72 ikiwa hatatoa soksi.
- Soksi zenyewe zinatakiwa zifunike sehemu ya kuoshwa miguu, yaani mguu hadi vifundoni.
Kuna tofauti ya rai miongoni mwa Maulamaa kuhusu ikiwa mtu atakapovua soksi au khuff zake basi wudhuu wake utatenguka au kubakia. Rai iliyo sahihi ni kuwa wudhuu utakuwa bado upo na haujatenguka kwa kuwa hakuna katika mapokezi ya kisheria yaliyoeleza kutenguka kwa wudhuu katika hali hiyo ingawa mapokezi yameeleza jinsi ya kufanywa wakati wa kuchukua wudhuu. Rai hiyo ni ya wema waliotangulia na Maulamaa wakubwa, nao ni: Qataadah, al-Hasan al-Baswriy na Ibn Abi Layla. Na imeungwa mkono na Ibn Hazm na ndio rai ya Shaykhul Islaam Ibn Taymiyah na Ibn al-Mundhir na katika wanachuoni wa karibuni ni Shaykh Ibn 'Uthaymiyn. Imaam An-Nawawiy kasema kuwa hii ndio rai yenye nguvu.
Na kuhusu soksi kuwa na tundu dogo au kubwa, au ni nyepesi inaonyesha mwili, ingawa tulitumia rai ya nyuma kuwa hazifai, lakini rai iliyo sahihi ni kuwa hazina neno kwani sheria haikuweka masharti hayo na kama kungekuwa na matatizo katika hayo, basi Mtume (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) angesema na kuweka wazi hilo. Rai hii wamekubaliana Maulamaa wengi wakiwemo; Imaam Ash-Shafi'iy, Imaam Ahmad, Imaam Sufyaan ath-Thawry, Shaykhul Islaam Ibn Taymiyyah, Imaam an-Nawawiy, Ibnul Mubaarak, Ibn Uyaynah, Abu Thawr na wengineo. Ama Imaam Abu Haniyfah na Imaam Maalik wao wamekwenda kwenye msimamo wa kuwa soksi zikiwa na matundu makubwa katika sehemu zenye kupaswa kutiwa wudhuu zinakuwa hazifai.
Kwa kifupi ni kuwa, maadam soksi hata kama ina matundu lakini bado imebaki kwenye maana ile ya kuwa ni yenye kuvalika na kukanyagalika kwa kutembea nayo, basi hukumu inakuwa pale pale kuwa yafaa kupanguswa na haina neno japo ina tundu kwani hakukupatikana dalili ya kulikataza hilo.
Soksi zinafutwa juu na wala sio chini kwa mujibu wa kauli ya ‘Aliy bin Abi Twaalib (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliposema: “Lau Dini ingekuwa inakwenda kwa rai basi kupangusa kungekuwa chini na wala sio juu, kwani hivi ndivyo nilivyomuona Mtume akifanya”.
Katika mas-ala ya Ibaadah Dini hii haiendi na rai zetu bali ni juu yetu kufuata alivyofanya Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Kwa hali yoyote Muislamu anaruhusiwa kuswali akiwa amevaa soksi bila ya utata wala tatizo lolote.
Kwa manufaa zaidi bonyeza viungo vifuatavyo:
034 Kupaka Juu Ya Vizuizi - Kupaka Juu Ya Khufu
035 Masharti Ya Kupukusa Juu Ya Khufu Mbili
036 Yanayotengua Kupukusa (Kupaka/Kupangusa) Juu Ya Khufu Mbili
037 - Kupaka Kwenye Soksi Na Viatu
038 - Kupaka Juu Ya Kinachofunika Kichwa
Mtu Mgonjwa (Kilema) Afanye Wudhuu Vipi Na Aswali Vipi?
Tunatumai kuwa tutakuwa tumeeleweka.
Na Allaah Anajua zaidi