20-Uswuul Al-Fiqhi Baada Ya Al-Imaam Ash-Shaafi’iy

Sura Ya Tano

 

Uswuul Al-Fiqhi Baada Ya Al-Imaam Ash-Shaafi’iy

 

Ar-Risaalah ya Al-Imaam ash-Shaafi’iy ilihodhi masomo ya Maarifa ya Sheria za Kiislamu pale tu ilipoanza kutoka. Hakika matokeo yake ni kwamba; wanazuoni walijigawa kwenye makundi mawili. Kundi la kwanza ambalo ni wengi wao ni Ahl al-Hadiyth, waliikubali, na waliitumia kwa kuitetea elimu ya Shaafi’iy katika Maarifa ya kisheria. Kundi jengine, ambalo hata hivyo, walikataa mengi yaliyokuwemo humo, na walijaribu kubadilisha chochote ambacho kazi ya al-Imaam ash-Shaafi’iy iligongana na taratibu zao na mwendo wao, kabla haijapata nafasi (ar-Risaalah) ya kuwashajiisha watu. Wajumbe wa kundi hili wengi wao hakika walitokana na Ahl ar-Rai’iy, ambao wote hao walikuwa hawakubaliani na chochote, takriban mambo yote aliyoandika al-Imaam ash-Shaafi’iy.

 

Ibn al-Nadiym ametaja vitabu ambavyo vimeandikwa kwenye somo la Uswuul al-Fiqh baada ya ar-Risaalah, vikiwemo an-Naasikh wa al-Mansuukh na as-Sunnah cha al-Imaam Ahmad bin Hanbal (Amefariki mwaka 233 H). As-Sunnah, hata hivyo, ni kitabu kilichojikita zaidi kwenye Tawhiyd na itikadi za msingi za Uislamu “’Aqaaid” kuliko maarifa ya Sheria za Kiislamu. Kuna matoleo mawili ya kazi hii katika kuchapishwa, toleo kubwa ni lile lililochapishwa Makkah mwaka 1349 H; ambalo lina nakala za kurasa huko Dar-al-Kutub na Maktaba ya Dhwaahiriyyah - Egypt na Damascus zilizo halisi. Toleo dogo iliyochapishwa Cairo bila ya tarehe, inahusiana na itikadi za msingi za imani halisi za Sunni (Sunni Orthodoxy), au “Ahl as-Sunnah”.

 

Al-Imaam Ahmad pia ameandika kitabu cha Twa’at ar-Rasuul “Utiifu kwa Mtume”. Ibn al-Qayyim amenukuu kutoka kitabu hicho ndani ya kitabu chake cha I’laam al-Muwaqqi’iyn, na inaonekana kwamba amehodhi nakala yake. Juu ya hivyo, nimekitafuta kitabu hichi sehemu nyingi, lakini nimeshindwa kukiona. Kutoka kurasa zilizonukuliwa za kitabu cha Ibn al-Qayyim, ni uwazi kwamba kitabu hicho hakika kilikuwa ni kitabu muhimu kwenye somo la Maarifa ya Sheria za Kiislamu, na utaratibu wa kushughulika na Sunnah. Inawezekana kuwa kimepotea baada ya wakati wa Ibn al-Qayyim, au kimetiwa jalada ndani ya kitabu chengine, au kurasa zake zimepotea hadi kuweza kupatikana baada ya kutafuta sana.

 

Vyanzo pia vimetaja kwamba Daawuud adh-Dhwaahiriy (Amefariki Mwaka 270 H.) ameandika kuhusu al-Ijmaa’ “Makubaliano” Ibtwaal at-Taqliyd “Katika Kuondosha Kunukuu Kusiko Halisi”, Khabar al-Waahid “Katika Usimuliaji wa mmoja-pekee”, al-Khuswuus wa al-‘Umuum “Katika Mahsusi na iliyo Jumla”, al-Mufassar wa al-Mujmal “Maneno Machache (lakini dhahiri) na ya Maelezo”, al-Kaafi fiy Muqabbalaat al-Muttalibi, yaani al-Imaam ash-Shaafi’iy, “Katika kushindana na ash-Shaafi’iy”, Mas-alatun Khalafa Fihima ash-Shaafi’iy “Masuala Mawili Aliyotofautiana nayo pamoja na al-Imaam ash-Shaafi’iy”.

 

Wakati wa kipindi hichi “’Ulamaa” waliokubaliana na mafunzo ya fikra za al-Imaam Abuu Haniyfah walijitolea umakini wao katika kusoma ar-Risaalah ya ash-Shaafi’iy, vyote vyote; kwa lengo la kuziharibu yale wasiyokubaliana, na kutoa aina yao ya vyanzo-utaratibu na Misingi ya Maarifa ya Sheria za Kiislamu kutoka kwenye kesi za kisheria Fataawa ya al-Imaam Abuu Haniyfah.

 

Kwa dalili hizi, wanazuoni wa Hanafi walitoa vitabu (vingi) tofauti. ‘Iysa bin Abbaan (Amefariki Mwaka 220 H.) ameandika Khabar al-Waahid, Ithbaat al-Qiyaas, “Kuthibitisha Mfanano al-Qiyaas”, na Ijtihaad ar-Rai’, “Matumizi ya Hoja za Kisheria”.

 

Al-Barzai (Amefariki Mwaka 317 H.) ameandika Masaa’il al-Khilaaf “Masuala ya Kutokubaliana”, ambacho kina nakala za kurasa 236 ndani ya Maktaba ya Zaytuunah huko Tunisia, nambari 1619.

 

Abuu Ja’far at-Twahaawiy (Amefariki Mwaka 321 H.) ameandika Ikhtilaaf al-Fuqaaha “Kutokubaliana kwa Wanazuoni”, ambacho kilifanyiwa ufupisho na Abuu Bakr al-Jassaas (Amefariki Mwaka 370 H.). Kuna nakala ya kitabu huko Cairo. Kwa maelezo zaidi, rudia Fahrisi ya Ma’had al-Makhtuutat (1/329).[55]

 

Al-Karabiysi an-Najafi (Amefariki Mwaka 322) ameandika al-Faruuq “Tofauti”, ambacho kina nakala za kurasa za Ahmad III na Fayd Allaah, Maktaba ya Istanbul.

 

Baadhi ya kazi zisizo na majina kwenye Maarifa ya Sheria za Kiislamu pia zilihusishwa kwa Ibn Sama’ah (Amefariki Mwaka 233).[56]

 

Al-Kannani (Amefariki Mwaka 289) ameandika al-Hujjah fi ar-Radd Ala ash-Shaafi’iy, “Ushahidi wa Kutokubaliana na Imaam ash-Shaafi’iy”.

 

‘Aliy bin Muussa al-Qurumi, dhehebu la Hanafi (Amefariki mwaka 305) ameandika Maa Khalafa Fiyhi ash-Shaafi’iy al-‘Iraaqiyiin Fii Ahkaam al-Qur-aan” “Namna Ambazo ash-Shaafi’iy Alipingana na Wairaqi Kuhusu Tafsiri ya Kisheria ya Qur-aan”, Ithbaat al-Qiyaas, al-Ijtihaad na Khabar al-Waahid.

 

Abuu al-Hassan al-Karkhi (Amefariki Mwaka 340) ameandika kitabu chake maarufu cha al-Uswuul “Vyanzo”, ambacho kilichapishwa pamoja na majumuisho ya vitabu vyengine nchini Cairo (hamna tarehe).

 

Abuu Sahl al-Nawbakhtiy (Amefariki mnamo mwaka 93 H.) akitokana na Imaamiyyah, ameandika Naqd Risaalat ash-Shaafi’iy “Ukosoaji wa ar-Risaalah ya Shaafi’iy”, Ibtwaal al-Qiyaas “Kuzikataa al-Qiyaas”, na ar-Radd ‘Ala Ibn ar-Rawandi Fi Ba’d Ara’ihi al-Uswuuliyyah “Kuziharibu Baadhi ya Mawazo ya Kisheria ya Ibn ar-Rawandi”. Ibn Junayn (Amefariki Mwaka 347), anayetoka kundi la Zaydiyyah, ameandika al-Faskh ‘Alaa Man Ajaza al-Nasakh lima Tamma Shar’uhu wa Jalla Naf’uhu “Ubatilishaji wa Utenguzi ulioruhusiwa katika Sheria ambazo Zimekwishatenguliwa na Kuthibitishwa kuwa na Manufaa”, na al-Ifhaam li Uswuul al-Ahkaam “Kuelewa Misingi ya Maarifa ya Sheria za Kiislamu.”

 

Wafuasi waliobobea Mafunzo ya al-Imaam ash-Shaafi’iy kwenye fikra za kisheria walitoa kazi zifuatazo:-

 

  • Abuu Thawr (Amefariki mwaka 240) ameandika Ikhtilaaf al-Fuqaaha “Kutokubaliana kwa Wanazuoni”.

  • Abuu ‘Abd Allaah Muhammad bin Nasr al-Marwazi (Amefariki mwaka 294) pia ameandika kitabu katika somo hilo hilo.

  • Abuu Abbaas bin Surayj (Amefariki mwaka 305) ameandika kitabu akiwakataa wote wawili ‘Iysa bin Abbaan na Muhammad bin Daawuud adh-Dhwaahiriy kwenye masuala ambayo walipingana na al-Imaam ash-Shaafi’iy.

  • Ibraahiym bin Ahmad al-Marwazi (Amefariki mwaka 340) ameandika Al-Umuum wa al-Khuswuus “Jumla na Mahsusi” na Al-Fuswuul fi Ma’rifat al-Uswuul.[57] Sura kuhusiana na Elimu ya Chanzo-Utaratibu wa Kisheria.

 

Baadhi ya wanazuoni hawa, walijitolea fikra zao katika kutoa ufafanuzi wa ar-Risaalah ya ash-Shaafi’iy kama kwa Abuu Bakr as-Sayraafi (Amefariki mwaka 330). Abuu al-Waliyd an-Nisaburi (Amefariki mwaka 365 au 363), Abuu Bakr al-Jawzaqi (Amefariki mwaka 388) na Abuu Muhammad al-Juwayni, baba wa (anayejulikana na wengi) Imaam al-Haramayn, mwalimu kwa al-Imaam al-Ghazzaali.

 

Ufafanuzi kwenye ar-Risaalah pia umedhaniwa kuwa ni kazi ya wanazuoni wengine watano, kwa majina ni: Abuu Zayd al-Jazuuli, Yuusuf bin ‘Umar, Jamaal ad-Diyn al-Afqahsi, Ibn Fakiham na Abuu al-Qaassim ‘Iysa bin Naji. Hakuna kutokana na fafanuzi hizi, ambapo wanazuoni wamekuwa wakinukuu hadi baada ya karne ya saba, ndio wamepata nuru nyakati za leo.

 

Shaykh Mustwafa ‘Abdur-Razzaq,[58] ametaja kwamba maktaba ya wazi nchini Paris inashikilia nakala ya fafanuzi kutoka kwa al-Juwayni kuhusiana na ar-Risaalah, na kunukuu baadhi ya sehemu hizo. Mimi, mwenyewe, nimejaribu kuzipata kurasa hizi nchini Paris, lakini nimeshindwa. Labda, zimewekwa pamoja na vitabu vyengine chini ya mada au jina tofauti. Huenda, njia pekee ya kuipata ni kuitafuta kwenye kurasa zote tofauti. Kwamba, hata hivyo, hiyo ni kazi inayotisha, kwani mchunguzi atahitaji kutumia muda wake mkubwa mno katika kukifanya kibarua hichi.

 

 

MAENDELEO YA USWUUL AL FIQH
BAADA YA AL-IMAAM ASH-SHAAFI’IY

 

Yale tuliyoyataja hadi kufikia hapa yanaweza kutambulika kama ni maendelo. Kwani kimsingi ni mzunguko wa kukanusha, kukubali au kutoa maoni kuhusiana na ar-Risaalah na ukweli hauendelei mbali zaidi ya hapo. Pale tu taratibu zinaposimamishwa, basi taratibu hizi zilizopatikana hadi mnamo mwa mwanzo wa karne ya tano H, ndipo inaweza kutambulika kuwa ni maendeleo yalio muwafaka kuanza kuchukua hatamu kwenye uwanja huo.

 

Wakati wa kipindi hichi, al-Qaadhi al-Baqillaani (Amefariki mwaka 402 H.) na al-Qaadhi ‘Abdul-Jabbaar al-Hamadan (Amefariki mwaka 415 H.) ameibeba kazi ya kuandika upya somo lote la mafunzo na misingi ya Maarifa ya Sheria ya Kiislamu – Chanzo na Utaratibu, au al-Uswuul.

 

Ndani ya kitabu chake cha al-Bahr, az-Zarkhasi ameandika “…majaji wawili, Qaadhi wa Ahl as-Sunnah, Abuu Bakr Twayyib al-Baqillani, na Qaadhi wa Mu’tazilah, ‘Abdul-Jabbaar, alikuja na kupanua kuhusiana na yale yaliyoandikwa, kutolea maelezo kwa yaliyokuwa huko kale ni kidogo kuliko na yanayoonekana, akatoa maelezo kwa yale yaliyotajwa kwa njia ya jumla, na kuondosha utata.”

 

Al-Qaadhi al-Baqillani alitunikiwa cheo cha Shaykh al-Uswuuliyyiin[59] “Shahada ya Pili ya Wanazuoni wa al-Uswuul”, baada ya kuandika at-Taqriyb wa al-Irshaad “Ubainifu na Muongozo”. Kitabu hicho kimepotea kwa karne (zaidi ya moja), ingawa inawezekana kikatokea kwenye maandiko ya mjumuisho mmoja au mwengine. Katika kesi yeyote, wanazuoni wa al-Uswuul waliendelea kunukuu ndani (ya hicho kitabu) hadi karne ya tisa AH.

 

Kwa sehemu yake, al-Qaadhi ‘Abdul-Jabbaar ameandika kitabu chenye jina la ama al-’Ahd “Maagano” au al-‘Amad “Nguzo” na kuandika ufafanuzi wake kuhusiana na hicho kitabu.

 

Imaam al-Haramayn (Amefariki mwaka 478 H) amefupisha kitabu cha al-Baqillaani cha at-Taqriyb wa al-Irshaad, ndani ya kitabu chenye jina la at-Talkhiys “Iliyofupishwa” au al-Mulakhkhas “Ufupisho”, ambacho baadhi ya kurasa zake zimehifadhiwa ndani ya mjumuisho wa baadhi ya maandiko. Baadaye, wanazuoni wa Maarifa ya Sheria za Kiislamu walitumia fikra nyingi za al-Baqillaani kutoka kwenye kitabu chake.

 

Imaam al-Haramayn alitoa kelelezo cha kazi yake kwenye al-Uswuul, al-Burhaan “Ushahidi”, kwenye kitabu cha al-Baqillaani cha at-Taqriib, ambapo humo imejumuisha matawi ya Uswuul, kilikuwa kipo huru na taratibu zake, na kikafuata ushahidi wowote uliopatikana.[60] Imaam al-Haramayn hakukubaliana na walimu wake (yaani al-Imaam al-Ash’ari na al-Imaam ash-Shaafi’iy) katika makala nyingi. Na kwamba wengi wa wanazuoni wake wa karibu kutoka kwenye mafunzo ya fikra za kisheria za ash-Shaafi’iy, walikataa ufafanuzi wake na wala hawakuitambua namna ilivyohitaji, ingawa sehemu kubwa wamekitumia ndani ya vitabu vyao.

 

Wanazuoni wawili wa Maliki, al-Imaam Abuu ‘Abdillaah al-Maziri (Amefariki mwaka 536 H.) na Abuu al-Hassan al-Abyari (Amefariki mwaka 616 H.) waliandika ufafanuzi kwenye al-Burhaan, na mwanazuoni wa tatu wa ki-Maliki, Abuu Yahya, ameunganisha fafanuzi mbili hizo lakini bado, wanazuoni wote hawa watatu walichambua kwa pupa, kama sio kusikokuwa na haki, kwa Imaam al-Haramayn. Kwa sababu wa yale waliyoyatambua kuwa ni ujasiri katika kumkana al-Imaam al-Ash’ari kwenye mambo asiyokubaliana pamoja nao na katika kumkana al-Imaam Maliki kwenye suala la al-Maswaalih al-Mursalah. Imaam al-Haramayn aliongezea utangulizi kwa kitabu cha al-Imaam ash-Shaafi’iy ambacho kilizungumzia masuala yasiyopatikana ndani ya ar-Risaalah. Alianza kwa kujadili elimu ya vyanzo hivyo na dhana ambazo yeyote aliyependa kusoma sayansi yoyote kwa ndani, ni lazima asome. Alieleza kwamba vyanzo vya Uswuul al-Fiqh vilikuwa ni ‘Ilm al-Kalaam, lugha ya Kiarabu na Fiqh. Baadaye, alijadili kuhusu hukumu ya kisheria, wajibu na uwezo. Akijadili kwa undani, masuala yanayohusiana na sayansi tofauti, na kueleza yale ambayo yanaweza kueleweka kwa hoja. Na ambayo kwa dini, masuala yote hapo juu yanafanya utangulizi wa mjadala wa neno la al-Bayaan “Tamko lililo dhahiri”, mada ambayo al-Imaam ash-Shaafi’iy alianza nayo kwenye ar-Risaalah.

 

Hata hivyo, ni uwazi ulio dhahiri, pale tunapoona namna Imaam al-Haramayn alivyojadili mada ya al-Bayaan na kwa mada nyengine, ametaja ndani ya ar-Risaalah, kwamba al-Imaam al-Haramayn ametafsiri misamiati ya maneno; ikiwemo al-Bayaan kwa vizuri zaidi kuliko al-Imaam ash-Shaafi’iy alivyofanya. Alilitafsiri, akaelezea sifa zake, akataja kutokubaliana kuhusiana nayo, na akaweka mafungu yake tofauti. Pia alijadili jambo jengine ambalo al-Imaam ash-Shaafi’iy hakulijadili, Taakhiyr al-Bayaan ilaa Waqt al-Hajah “Kuiakhirisha al-Bayaan hadi muda utakaotakiwa”, na kuhusu kutokubaliana nayo. Baadaye katika kujadili mafungu tofauti ya al-Bayaan, alikariri kwa mara nyengine mafungu matano ambayo aliyataja al-Imaam ash-Shaafi’iy, akawakilisha maoni ya Abuu Bakr Daawuud adh-Dhwaahiriy kwenye mada hiyo, na baadaye akataja mafungu mengine ya al-Bayaan ambayo wanazuoni wengine walishauri.

 

Imaam al-Haramayn alishikilia ushauri wa kwamba al-Bayaan ina maana ya ‘ushahidi’, ambayo ina aina mbili: ‘Aqli “akili” na Sami’i “kupokea”. Msingi wa ushahidi wa “kupokea” ni Qur-aan iliyo na miujiza na kwamba; namna ukaribu wa ushahidi ulivyo kwa Qur-aan, ndivyo inavyotengeneza sheria/hukumu ya kufuatwa. Matokeo yake ni kwamba; mfuatano wa protokoli katika ushahidi wa “kupokea” ni: Qur-aan, Sunnah, al-Ijmaa’, Khabar al-Waahid na al-Qiyaas.

 

Baadaye alijadili kuhusu lugha, na kueleza kwamba, wanazuoni wa Maarifa ya Sheria za Kiislamu wamejadili kuhusu elimu ya lugha, kitu ambacho wanazuoni wa Kiarabu wamekiacha, kama vile Awaamir “Amri”; Nawaahi “Makatazo”, na al-‘Umuum wa al-Khuswuus “Jumla na Mahsusi” ambayo al-Imaam ash-Shaafi’iy amejadili.

 

Kwenye mjadala wa mada ya elimu ya lugha, ametaja baadhi ya mawazo ya al-Baqillaani ambayo yanaonesha wazi kwamba al-Baqillaani tayari amekwishaunganisha mambo haya, kwa taratibu za al-Imaam ash-Shaafi’iy.

 

Pale al-Imaam al-Ghazzaali alipokuwa mwanafunzi wa al-Haramayn, ilikuwa ni asili tu kwamba, amesukumwa na yeye. Ukweli ni kwamba, al-Imaam al-Ghazzaali ameandika vitabu vinne kwenye somo la al-Uswuul. Kazi ya mwanzo kati ya hizi ilikuwa al-Mankhuul “Mchakato”, toleo la ukubwa na wa wastani, iliyoandikwa kwa (ajili ya) wanaoanza na wanaonyanyukia kwenye kusoma al-Uswuul. Cha pili katika kitabu, hakuna kinachojulikana isipokuwa kwamba ilinukuliwa kwenye al-Mustwasfaa,[61]na kwamba mada yake ilikuwa Tahdhiyb al-Uswuul “Ustaarabu wa al-Uswuul”. Kitabu cha tatu kina jina la Shifa’ al-Ghaliyl fiy Bayaan ash-Shibh wa al-Mukhayyal wa Masaalik at-Taliyl, na kilifanyiwa uhariri na kuchapishwa nchini Baghdad mwaka 1390/1971. Mkusanyiko wake (encyclopedia) wa Shari’ah Chanzo-Utaratibu. Kitabu chake cha nne kwenye mada hiyo, na neno lake la mwisho, kilikuwa ni al-Mustwasfaa, ambacho kilichapishwa mara kadhaa nchini Misr na kwengineko. Hakika, hii ni kazi aliyoiandika baada ya kukaa mafichoni akifanya uchunguzi.[62]

 

Al-Imaam alianza kitabu chake kwa utangulizi ambapo aligusa takriban dhana zote za Aristotle, somo ambalo daima alikuwa akilipenda. Baadaye aliandika kuhusu ‘Hadd’ “Adhabu zilizotajwa”, kuhusu masharti ambayo ni lazima yatimizwe kabla ya kutendewa kazi, na kuhusu aina tofauti za Huduud. Baadaye alijadili kuhusu Daliyl “Ushahidi” na aina zake tofauti.

 

Kwa nukta hii ndani ya kitabu chake, al-Imaam al-Ghazzaali aliendelea kujadili pembe nne za kazi yake, mada ambazo zimekamata kila kitu ndani ya uwanja wa al-Uswuul, na ambazo mwalimu wake, Imaam al-Haramayn na waliomtangulia, kama vile al-Baqillaani, walijishughulisha nazo zaidi. Kwa vile mwalimu wake, alikuwa na maoni yake ambayo yalitofautiana na yale ya al-Imaam al-Ghazzaali alishikilia mawazo ambayo yapo tofauti. Kama ya waliomtangulia na kama ilivyo kawaida, wakati wa al-Imaam al-Ghazzaali kulikuwepo na wale waliokubaliana na mawazo yake na wale wasiokubaliana.

 

Haya ndio yalikuwa ni maendeleo muhimu yaliofanywa na wafuasi wa al-Imaam ash-Shaafi’iy ndani ya uwanja wa Uswuul.

 

Kundi la pili lililochangia kwenye maendeleo ya somo ni Mu’tazilah. Baada ya Qaadhi ‘Abdul-Jabbaar kuandika kitabu chake al-‘Amad au al-‘Ahd, na kuandika ufafanuzi wake uliokamilika kwenye kitabu hicho, alihifadhi baadhi ya mawazo ya al-Uswuul ndani ya mjumuiko wa kitabu kikuu (encyclopedia), baadhi ya sehemu zake ambazo zimepatikana na kuchapishwa chini ya mada ya al-Mughni “Maandiko” (volume) kumi na saba ya ‘encyclopedia’ hii yalitunukiwa kwenye masomo la al-Uswuul.

 

Kama alivyojihusisha Imaam al-Haramayn kwenye kitabu cha al-Baqillaani, ndivyo Abuu al-Husayn al-Basri al-Mu’tazili (Amefariki mwaka 435 H.) alivyojihusisha na vitabu vya al-Qaadhi ‘Abdul-Jabbaar, na kuandika ufafanuzi kwenye al-‘Amad/al-‘Ahd. Pale alipohisi kwamba ufafanuzi huu ulikuwa mkubwa, alikifupisha ndani ya kitabu chake maarufu cha al-Mu’tamad “Chenye Kutegemewa”, ambacho kimechapishwa na kinapatikana sehemu nyingi mno.

 

Wakati wa kipindi hichi, ash-Shaykh Abuu Ishaaq ash-Shiraazi (Amefariki mwaka 476 H.), ameandika vitabu vyake viwili al-Lam “Nuru yenye Kung’aa” na at-Tabswiyrah “Uwongofu”, vyote ambavyo vimechapishwa.

 

Al-Qaadhi Abuu Yahya al-Farra’ al-Hanbali ameandika kitabu kwenye Uswuul chenye jina la al-‘Uddah fi Uswuul al-Fiqhi “Zana za Uswuul al-Fiqhi”, ambacho kilifanyiwa uhariri na kuchapishwa nchini Saudi Arabia 1400/1980.

 

Ibn ‘Aqil al-Baghdadiy, ambaye ni mwanazuoni mwengine wa ki-Hanbali, ameandika al-Waadhwih Fiy al-Uswuul “Yaliyo Wazi Kwenye Uswuul”.

 

Abuu al-Khattaab ameandika kitabu chake maarufu, at-Tamhiyd “Dibaji”, ambayo ilifanyiwa uhariri hivi karibuni na kuchapishwa Makkah.

 

Miongoni mwa vitabu walivyoandika wanazuoni wa mafunzo ya mawazo ya kisheria ya Maliki kwa wakati huu ni ‘Uyuun al-Adillah Fiy Masaa’il al-Khilaaf Bayna Fuqaaha al-Amswaar “Wingi wa Ushahidi katika Masuala yenye Mgongano Miongoni mwa Wanazuoni wa Fiqh wa miji”, kilichoandikwa na Ibn al-Qasswaar al-Baghdaadiy (Amefariki mwaka 398 H.), ambacho kina nakala mpya huko Chuo Kikuu cha al-Qarawiyyiin nchini Fez.[63] Mwanazuoni ash-Shiraazi anakitaja kuwa ni kitabu bora kilichowahi kuandikwa miongoni mwa wanazuoni wa Maliki kwenye mada ya tofauti za wanazuoni. Ibn al-Qasswaar pia aliandika Muqaddimah fiy Uswuul al-Fiqh “Utangulizi kwa Uswuul al-Fiqh”, ambacho kina makala yake katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha al-Azhar.

 

Vitabu vya Shaafi’yyah, Hanaabila, Maalikiyyah na Mu’tazilah, vyote vilifuata mtindo kama huu, katika mtiririko wa sura zao na ufumbuzi wa masuala yao muhimu. Hatimaye mtindo uliokuja kugundulikana kwa jina la “Taratibu za Mutakallimuun”.



[55] Toleo la sehemu ya ufupisho wa Jassas wa kitabu hichi ulichapishwa nchini Pakistan na Islamic Research Institute-Taasisi ya Uchunguzi wa Kiislamu-Mhariri wa toleo hiyo, hata hivyo amefanya makosa kuihusisha kazi hiyo moja kwa moja kwa Abuu Ja’far at-Twahaawiy.

[56] Angalia, Ibn al-Nadiym, Al-Fihrisi, uk. 284.

[57] Ibn al-Nadiym, Al-Fihrist, uk. 299.

[58] Angalia, ‘Abdur-Razzaaq, Tamhiyd li Taariykh al-Falsafah, Cairo.

[59] Angalia, al-Quraffi, Nafaa’ii, I, uk. 149.

[60] Toleo safi la Al-Burhaan limechapishwa hivi karibuni huko Qatar.

[61] Angalia al-Ghazzaali, al-Mustwasfaa, I, uk. 187. Tafsiri iliyo nzuri kabisa kwa lugha ya Kiingereza ya al-Mustwasfaa ya al-Ghazzaali ilifanywa na Dr. Ahmad Zaki Hammaad.

[62] Angalia rejeo chini ya ukurasa’ nambari 61.

[63] Angalia Brockermann, Hati, II, uk. 963, no. 49.

Share