Kuchukua Mkopo Wa Ribaa Kwa Ajili Kwenda Hijjah Inafaa?

 

 

Kuchukua Mkopo Wa Ribaa Kwa Ajili Kwenda Hijjah Inafaa?

 

Alhidaaya.com

 

 

Swali:

 

Asaalam Alykum,

 

Mimi nna nia ya kwenda hija, lakini hizi pesa nnazotaka kwendea Hijja ninataka kukopa kwenye chama chetu cha kuweka na kukopa. Mimi nimechangia sh.1,000,0000 na nna uwezo wa kukopa sh.3,000,000 lakini wanakata na intrest. Je pesa hizi zitafaa kuwendea hijja?

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Fardhi ya kutekeleza Hijjah ni fardhi inayompsa mtu kutekeleza akiwa na uwezo kama Anvyosema Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa):   

 

وَلِلَّـهِ عَلَى النَّاسِ حِجُّ الْبَيْتِ مَنِ اسْتَطَاعَ إِلَيْهِ سَبِيلًا ۚ 

Na kwa ajili ya Allaah imewajibika watu watekeleze Hajj katika Nyumba hiyo kwa mwenye uwezo. [Al-'Imraan: 96]

 

Na Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kutokana na Hadiyth iliyopokelewa kutoka na 'Umar bin Khatwaab (Radhwiya Allaahu 'anhu):  

((Na kwenda Hijjah ukiweza kufanya hivyo)) [Muslim, Abuu Daawuwd, At-Tirmidhiy, An-Nasaaiy]  

 

Ibara hii ya Aayah na Hadiyth yana maana ya kuwa kila Muislamu ni lazima ahiji mara moja katika maisha yake akiweza kufanya hivyo. Uwezo una tafswili nyingi na yaliyo muhimu ni: -

 

Awe na afya nzuri ya kuweza kustahamili mazito ya safari.

 

Kuwe na usalama njiani, kwenda na kurudi.

Awe na uwezo wa kutoa gharama za safari na kuacha masurufu yote ya wale wanaomtegemea. 

 

Ikiwa sharti moja katika hayo imekosekana basi Hijjah haijamlazimu mtu huyo. 

 

Fardhi hii ni sawa tu na fardhi ya kutoa Zakaah kwani maskini hana waajib wa kutoa Zakaah pamoja na kuwa Zakaah ni nguzo ya Uislam, na hata mwenye uwezo pia kuna masharti yake mfano, awe na kiasi maalum cha mali na pia sharti ya mali yenyewe iwe imetimia kwa mwaka mzima bila ya kutumiwa. Muislamu anaposhindwa kutimiza sharti hizo, waajib wa kutekeleza fardhi hizo huwa umemuondokea. Na hata atakapofariki akiwa katika hali ya kukosa uwezo basi hana jukumu wala dhambi mbele ya Allaah.

 

Ikiwa hali ni hiyo basi, kuchukua mkopo kwa ajili ya kutekeleza Hajj haifai, kwani ni jambo la kujikalifisha ambalo Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa)  Ametuondoshea.

 

Juu ya hivyo ni kwamba mkopo wenyewe una riba jambo ambalo ni haraam kwani haruhusiwi kula na kufaidika nayo wala kufanyia Hajj. Maonyo kadhaa yamethibiti kuhusu ribaa yakiwemo Hadiyth:

 

"Dirhamu ya ribaa anayokula mtu na huku anajua ni mbaya zaidi kuliko kuzini mara thelathini na sita." [Ahmad]

 

"Ribaa ina milango 73 iliyo nyepesi na sahali ni mtu kumuoa mamake." [Al-Haakim]

 

"Jiepusheni na mambo saba yenye kuangamiza… kula ribaa."  [Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Hivyo kufanya Hajj kunahitaji kipato kilichokuwa safi kutoka katika chanzo cha halaal.

 

Vile vile deni ni jambo zito katika Uislamu kwani ni haki ya mtu, hivyo ni jambo la kwanza la kutekelezwa kabla ya ‘ibaadah yoyote. Atakapofariki Muislamu mwenye deni, akasubiri kwanza alipe deni lake, kisha akafariki akiwa hakutimiza Hijjah, basi ataonana na Rabb wake akiwa amekamilisha Uislamu wake kwa sababu Hijjah haikuwa ni waajib kwake. Lakini akitekeleza Hijjah kabla ya kulipa deni kisha akafariki, atakuwa katika hatari kwa sababu hata wanaofariki wakiwa Mashahidi wanasamehewa kila kitu isipokuwa deni. Sasa vipi basi iwe wengine?

 

Hitmisho ni kwamba haikupasi kuchukua mkopo kwa ajili ya kutekeleza Hijjah ikiwa ni mkopo wenye riba au hata bila ya riba.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

Share