Hijja Wanayopelekwa Watu Na Serikali Au Mialiko Ya Nje Inafaa?
Hijja Wanayopelekwa Watu Na Serikali Au Mialiko Ya Nje Inafaa?
Swali:
AAWW!
Nauliza:
Hizi Hijja wanzokwenda viongozi kwa gharama za serikali au mialiko ya mfalme wa Saudia zinasihi?
Wabillahi Taufiq,
Jibu:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Kwanza tunapenda kukumbusha ndugu muulizaji kuacha kufupisha salaam unapoandika, unapoteza fadhila na ujira kwa kufanya hivyo.
Kwa hakika usaidizi unatakiwa upewe Waislamu wanaostahiki ambao ni hohehahe. Mara nyingi fursa hizi huwa zinatumiwa vibaya kwa kupewa watu ambao ni viongozi wenye uwezo au ambao tayari wameshakwenda kufanya Hijjah kama ambavyo tunaona wanavyofanya baadhi ya viongozi wa taasisi za Kiislamu. Na jambo lenye kusikitisha zaidi, kuna baadhi ya viongozi wa Taasisi fulani za Kiislamu huuza hizo tiketi za bure wanazopewa na serikali ya Saudia Arabia ambayo inafanya juhudi kubwa sana za kusaidia nchi nyingi duniani kila mwaka ili wale wasio na uwezo wapate nao fursa ya kutekeleza nguzo hiyo tukufu.
Na haitokuwa vyema ikiwa mtu ana uwezo kukubali mwaliko kama huo na vizuri akatae ili fusra hiyo wapewe wale wasio na uwezo na hususan wale wenye umri mkubwa.
Hata hivyo, wakati mwengine serikali ya Saudia huwa inataka viongozi wa nchi tofauti kwa ajili ya makongamano na mikutano na ikiwa ni msimu wa Hijjah basi hutaka waalikwa wao wafanye Hijjah kabisa na katika hilo hakuna tatizo. Hijjah aina hizi hazina tatizo lolote na ni thawabu kwa wenye kujitolea kwa hilo. Hata hivyo kujitolea huko kungekuwa natija nzuri zaidi lau wangepatiwa:
- Waislamu wasiokuwa na uwezo (masikini na mafakiri) ambao hawajawahi kwenda.
- Wengine wasio na uwezo kama madu'aat (walinganiaji) ambao hawajawahi kwenda.
- Wenye uwezo kukataa kuchukua fursa hizo na badala yake kupendekeza watu wengine.
- Kina mama pia nao wapatiwe fursa hizo (Wakiwa wana mahaarim zao)
- Kusiwe na ubaguzi katika kuchagua watu.
Na Allaah Anajua zaidi