Vipi Kutekeleza Umrah

 

Vipi Kutekeleza Umrah

 

Alhidaaya.com

 

Swali:

 

Asalam Alaykum.

 

Tafadhali Naomba Mnijulishe Yanayopasa Kufanya Ktk Umra Toka Kukusudia Kwenda Makka Dua Za Kusoma Na Mahali Panapohusu Kusoma Na Yote Yanayo Mhusu Kufanywa Ktk Safari Hii. Nimekusudia Kwenda Ktk Kumi La Mwanzo La Mwezi Wa Ramadhwaan In Shaa Allaah Mwaka Huu.

 

Shukuran

 

 

Jibu:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

Kwanza tunatambua kutokana na barua yako kuwa wewe ni mwanamke hivyo haikupasi kwenda ‘Umrah peke yako bila ya kuwa na Mahram (mumeo au kaka zako au baba au ‘ami au  yeyote mwenye undugu wa damu na wewe ambaye kisheria hawezi kukuoa). ‘Umrah kawaida unaweza kuikamilisha kwa siku moja tu, bali ni masaa machache tu utakuwa umemaliza ‘Umrah yako na sio kama Hajj ambayo inahitaji masiku kadhaa na taratibu ndefu.

 

Yafutayo ni ya kufanya kwa mpangilio:

 

 

Nia: 

 

Nia ya ‘Umrah au ya ibada yoyote inakuwa moyoni na haitamkwi kwa ulimi. Kwa hiyo unapofika Miyqaat (sehemu ya kuanzia ibada yako hiyo, ambapo atakoga na kuvaa ihraam) utakapomaliza ndio utakuwa umetia nia yako moyoni kisha utaleta talbiyah ifuatayo:

 

لبيك عمرة، لبيك اللهم لبيك، لبيك لا شريك لك لبيك، إن الحمد والنعمة لك والملك لا شريك لك.

Labbayka '‘Umrah, Labbayka-Llaahumma Labbayk.  Labbayka Laa Shariyka Laka Labbayk. Innal-Hamda Wan-Ni'imata Laka Wal-Mulk Laa Shariyka Lak.

 

"Nimekuitikia Ee Allaah '‘Umrah, Nimekuitika Ee Allaah nimekuitika, nimekuitika Huna mshirika Wako nimekuitika, hakika Sifa njema na Neema na Ufalme ni Vyako Huna mshrika"

 

Sehemu hiyo ya Miyqaat inategemea usafiri wako, kama ni wa gari basi ndio itabidi ufikie hapo kutia tohara. Na kama ni usafiri wa ndege basi tohara na nia hiyo itabidi utie tokea nyumbani. 

 

 

Twawwaaf:

 

Ni kuzunguka mara saba kuanzia Hajarul-Aswad (jiwe jeusi) na kuanza kwa kusema:

بسم الله والله أكبر

Bismillahi Wa-Allaahu Akbar

 

Unapozunguza Twawwaaf, unaweza kusoma Qur-aan au kumtukuza Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) yaani Subhaana Allaah, au Kumshukuru, yaani Alhmadulillah, au Tahliyl yaani Laa Ilaah Illa Allah, au kuleta takbiyr yaani Allaahu Akbar, au kumswalia Nabiy (Swallah Allahu 'alayhi wa aalihi wa sallam), au kusoma duaa zozote unazotaka. Lakini sio kusoma vile vitabu ambavyo vinauzwa na vimeandikwa duaa za kila Twawwaaf na du’aa yake, vitabu hivyo vimeandikwa na watu na havina ushahidi kutoka katika Hadiyth za Nabiy kuwa alifundisha du’aa hizo zilizopangiliwa kwenye hivyo vitabu, bali ni mambo ya uzushi na juu ya hivyo yanasababisha zahma za watu kwa kutembea pole pole huku wakisoma vitabu kwa sauti. Ni bora kusoma du’aa zako mwenyewe unazohitajia kwa matatizo yako na shida zako, kwani hiyo ni fursa ya kuomba kila unachokitaka na kutamani kuliko kusoma vitabu hivyo ambavyo wengi hawajui hata maana ya yaliyoandikwa ndani yake.

 

Na kila unapofika katika Rukn (nguzo) ya Yamani hadi katika jiwe jeusi unasema:

 

 رَبَّنَا آتِنَا فِي الدُّنْيَا حَسَنَةً وَفِي الاَخِرَةِ حَسَنَةً وَقِنَا عَذَابَ النَّارِ 

((Rabbanaa Aatinaa Fid-Duniyaa Hasanataw-Wafil-Aakhirati Hasanataw-Waqinaa 'Adhaaban-Naar)).

 

"Rabb wetu Mlezi, Tupe duniani mema, na Aakhirah mema, na Utulinde na adhabu ya Moto"

 

Ukifika katika Hajarul-Aswad (jiwe jeusi) utaashiria kwa mkono wako kuelekea jiwe hilo na kusema

 بسم الله والله أكبر 

Bismillahi Wa-Allaahu Akbar

 

Utakuwa umemaliza Twawwaaf moja. Utaendelea hivyo hadi umalize Twawwaaf (mizunguko) zote saba.

 

Haifai kujilazimisha kwenda kuligusa au kulibusu Hajarul-Aswad na kusababaisha zahma na kusongamana zaidi na watu kwani inatosheleza kuashiria kwa mkono na thawabu ni zile zile, bali pengine ni zaidi kuliko mwenye kusababisha kusukumana na wenzake kwa ajili ya kutaka kuligusa jiwe.

 

 

Rakaa Mbili Katika Maqaamu Ibrahiym 

 

Ukimaliza Twawwaaf ya saba utasogea upande wa Maqaamu Ibraahiym na utaswali Rakaa mbili, Rakaa ya kwanza utasoma Suwrah Al-Kaafiruun (Qul Yaa Ayyuhal-Kaafiruun) na ya pili utasoma Suwral Al-Ikhlaasw (Qul-Huwa Allahu Ahad).

 

Kwa hali ilivyo hivi sasa sehemu hiyo imekuwa ni zahma sana, hivyo haikupasi kujilizamisha kuswali karibu kabisa na Maqaamu Ibraahiym, bali unaweza kusogea mbali kabisa almuradi umeelekea hiyo Maqaam ya Ibraahiym. Ni makosa kusababisha zahma zaidi na msongamano na kuswali sehemu ambazo zina zahma kuzidi kuleta mashaka kwa Waislamu wengine.

 

 

Sa'y

 

Utakwenda Swafaa na kuanza Sa’y kwa kupanda juu ya kilima cha Swafaa na utaelekea Kaaba na kusema: 

 

 لا إِلهَ إلاَّ  اللهُ وَحْدَهُ  لا شَرِيكَ لَهُ، لَهُ المُلْكُ وَلَهُ الحَمْدُ وهُوَ عَلى كُلِّ شَيءٍ قَديرٌ، لا إِلَهَ إلا اللهُ وَحْدَهُ أَنْجَزَ وَعْدَهُ، وَنَصَرَ عَبْدَهُ وَهَزَمَ الأَحْزَابَ وَحْدَهُ  

Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu Laa Shariyka Lah, Lahul-Mulku Walahul-Hamd Wa Huwa 'Alaa Kulli Shay-in Qadiyr.  Laa Ilaaha Illa-Allaah Wahdahu, Anjaza Wa'dahu Wanaswara 'Abdahu Wahazamal-Ahzaaba Wahdahu))

 

"Hapana Rabb Apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah, hali ya kuwa peke Yake, wala Hana mshirika Wake, ni Wake Ufalme na ni Zake sifa njema. Naye juu ya kila kitu ni Muweza.  Hapana Rabb apasae kuabudiwa kwa haki ila Allaah hali ya kuwa peke Yake, Ametekeleza ahadi Yake, na Amemnusuru mja Wake, na Amevishinda vikosi peke Yake"

 

Utaomba du’aa zako unazotaka kisha utaanza Sa’y ukifika Marwa utakuwa umemaliza Sa’y moja, utapanda kilima na kusema hivyo hivyo na kuomba kwa kuelekea vile vile Ka’abah. Kuanzia Swafaa na kufika Marwa unahesabu kuwa ni moja, na kutoka Marwa na kufika tena Swafaa ni mbili hivyo hivyo hadi utamalizia Sa’y yako ya saba katika kilima cha Marwa.

 

Kama ni mwanamme atanyoa au kukata nywele, na wewe utakata tu kidogo nywele zako kama inchi moja hivi au chini yake.

 

 

Kunywa Maji Ya Zamzam

 

Utakunywa maji ya zamzam na kuomba du’aa unayotaka na hapa utakuwa umemaliza ‘Umrah yako.

 

 

Ya Kuzingatia:

 

Du’aa hizo ni kuzisoma kwa Kiarabu tu.

 

Unaweza kunywa maji ya Zamzam kabla ya Sa’y au baada yake upendavyo.

Kwa maelezo zaidi tafadhali soma mada hii ifuatayo ambayo iko www.alhidaaya.com katika kiungo kifuatacho:

 

Bonyeza hapa:

 

TARATIBU ZA HAJJ NA ‘UMRAH

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

 

Share