Ni Kweli Mwenye Kuhifadhi Qur-aan Haozi Kaburini?

 

Ni Kweli Mwenye Kuhifadhi Qur-aan Haozi Kaburini?

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:
 
Shukran Allaah Awajazi Kila La Kheri Kwa Kazi Yenu. Mtu Akiwa Hafidhul Qur-aan Akifa Huwa Haozi Nauliza Ni Quran Yote Ama Kuhifadhi Baadhi Ya Suwrah Ama Juzu Fulani Anaingia Mtu Katika Fadhla Hii.
 
Fi Amanillah 
 
Sister In Islam.

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho

 

Mwanzo tufahamu fadhila za Qur-aan ni muhimu, kubwa na nyingi, lakini ifahamike kuwa fadhila hizi zinatokana na maelezo tuyopewa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) na Nabiy Wake, Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatuelezea yafuatayo katika ubora wa Qur-aan:

 

1.       Amesema Abu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba amemsikia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Isomeni Qur-aan kwani hakika itakuja Siku ya Qiyaama kumuombea Swahibu yake (aliyeisoma)” (Muslim).

 

2.       Na amesema an-Nawwaas bin Sam‘aan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akisema: “Siku ya Qiyaama italetwa Qur-aan pamoja na wale waliokuwa wakifuata maagizo yake duniani. Itamtangulia Suwrah Al-Baqarah na Aal ‘Imraan zikimtetea Swahibu yake (wale waliokuwa wakizisoma katika maisha yao)” (Muslim na at-Tirmidhiy). 

 

3.       Na imepokewa kwa ‘Uthmaan bin ‘Affaan (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mbora wenu ni yule aliyejifunza Qur-aan na akaifundisha” (al-Bukhaariy, Abu Daawuud na at-Tirmidhiy).

 

4.       Na imepokewa kutoka kwa mama wa waumini ‘Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Yule ambaye anasoma Qur-aan naye ni mahiri katika hilo, atakuwa pamoja na Malaika na Rusuli watukufu wenye kutii na yule ambaye anasoma Qur-aan na huku anaona ugumu na anapata shida, atapata malipo mawili” [Al-Bukhaariy, Muslim, at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

5.       Na imepokewa kwa Abu Musa al-Ash‘ariy (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mfano wa Muumini ambaye anasoma Qur-aan ni kama mfano wa mbalungi, harufu yake ni nzuri na ladha yake ni nzuri, na mfano wa Muumini ambaye hasomi Qur-aan mfano wake ni kama tende, haina harufu na ladha yake ni tamu. Na mfano wa mnafiki ambaye anasoma Qur-aan ni kama mfano wa mrehani, harufu yake ni nzuri na ladha yake ni chungu; na mfano wa mnafiki ambaye hasomi Qur-aan ni kama mfano wa handhala, hauna harufu na ladha yake ni chungu” [Al-Bukhaariy, Muslim, Abu Daawuud, at-Tirmidhiy na an-Nasaa’iy].

 

6.       Na imepokewa kwa ‘Umar bin al-Khatwaab (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika Allaah Atawanyanyua watu kwa Kitabu hichi na kuwatweza kwayo wengine” (Muslim).

 

7.       Na imepokewa kwa Ibn ‘Umar (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakuna husuda isipokuwa katika mambo mawili: Mtu aliyepewa na Allaah Qur-aan, akawa anaisoma nyakati za usiku na nyakati za mchana; na mtu aliyepewa na Allaah , naye akaitoa hiyo nyakati za usiku na nyakati za mchana” (al-Bukhaariy na Muslim). malimali

 

8.       Na amesema al-Baraa’ bin ‘Aazib (Radhwiya Allaahu ‘anhu): Mtu mmoja alikuwa anasoma Suwrah Kahf na kulikuwa na farasi aliyekuwa amefungwa karibu yake kwa kamba mbili, ukamfunika yeye ukungu (wingu) na farasi wake akawa anaogopa huku anaruka ruka na kumkimbia. Kulipopambazuka alikwenda kwa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kumweleza kisa hicho. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimwambia: “Hiyo ni as-Sakiynah (utulivu) unaoteremka kwa ajili ya Qur-aan” [al-Bukhaariy, Muslim na at-Tirmidhiy]

.

9.       Na imepokewa kwa Ibn Mas‘uud (Radhwiya Allaahu ‘anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Mwenye kusoma herufi kutoka kwa Kitabu cha Allaah atapata ujira mmoja, na ujira huu ni sawa na kumi mfano wake. Wala sisemi kuwa Alif Laam Miym ni herufi moja lakini Alif ni herufi na Laam ni herufi na Miym ni herufi” (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh na ameipokea ad-Daarimiy nayo ni Sahihi).

 

10.   Na imepokewa kwa Ibn ‘Abbaas (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Hakika yule ambaye kwamba hana moyoni mwake (yaani hakuhifadhi) chochote katika Qur-aan ni kama nyumba iliyohamwa” (At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadiyth Hasan Swahiyh na ameipokea Ahmad, al-Haakim na ad-Daarimiy). 

 

11.   Na imepokewa kwa ‘Abdullaah bin ‘Amru bin al-‘Aasw (Radhwiya Allaahu ‘anhuma) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Ataitwa Swahibu (msomi) wa Qur-aan Siku ya Qiyaama na ataambiwa: ‘Soma Qur-aan na upande kuelekea (mbingu za juu) na usome kama ulivyokuwa ukisoma duniani kwani daraja yako itakuwa ni kwa ile Aayah ya mwisho utakayosoma’ [Abu Daawuud na At-Tirmidhiy, na akasema ni Hadityh Hasan Swahiyh na imepokewa na Ahmad na Isnadi yake ni Hasan]”.

 

Hizi ni baadhi ya fadhila kutoka katika Sunnah zilizo sahihi. Bila shaka zipo fadhila za kusoma Aayah na surah Fulani zilizomo katika Qur-aan. Hata hivyo, wapo watu ambao wamebuni Hadiyth ili kuonyesha utukufu ambao haumo kabisa katika Qur-aan. Mfano ni ile inayosemekana ni Hadiyth lakini ni ya kubuni: “Msomaji wa Qur-aan hawi mzulufu”.

 

Ama fadhila hii kwa mwenye kuhifadhi Qur-aan kuwa hataoza haijapatikana katika Hadiyth zilizo sahihi. Hakika wale ambao miili yao haitaoza kwa Hadiyth sahihi ni Rusuli. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: 

 

"Allaah Aliyetukuka, Ameiharamisha ardhi kula miili ya Manabii" [Muslim, Abu Daawuud, an-Nasaaiy na Ibn Maajah kutoka kwa Aws bin Aws (Radhwiya Allaahu ‘anhu)].

 

Na katika Hadiyth nyingine Abu Dardaa’ (Radhwiya Allaahu ‘anhu) amesema kuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: “Niswalieni Ijumaa kwani kufanya hivyo kunashuhudiwa. Malaika wapo kwayo, na hakuna atakayeniswalia bila Swaalah yake hiyo kuletwa kwangu mpaka anakaposimama. Nikamuuliza: ‘Je, hayo pia yatakuwa baada ya kuaga dunia kwako?’ Akasema: ‘Allaah Ameiharamisha ardhi kuila miili ya Manabii’. Hivyo, Rasuli wa Allaah yu hai (uhai wa maisha ya Barzakh) na anaruzukiwa sana” [at-Tirmidhiy na Ibn Maajah].

 

Kuhifadhi Qur-aan kuna fadhila zake lakini pamoja na kufuata maagizo yaliyomo ndani yake na kukatazika na maharamisho. Kuhifadhi bila kufuata inakuwa haina fadhila kwani Qur-aan yenyewe itakuwa inakulaani nawe huna hata habari kwa yale matendo unayoyafanya.

 

 

Na Allaah Anajua zaidi.

 

 

 

 

 

Share