Sajdatus-Sahw Ni Moja Au Mbili?

 

SWALI:

 je "Sijdatus-sahw ni moja au mbili?

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na Salaam zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Tunashukuru kwa swali lako hili, hakika Sajdat as-Sahw ni: Sijda mbili ambazo zinazotekelezwa na mwenye kuswali kwa ajili ya kufidia au kurekebisha makosa yatokeayo akiwa ndani ya Swalah kutokana na kusahau (Sahw). Kuitekeleza sijda hii kunasababishwa na mambo matatu: Kuzidisha kitu (az-Ziyaadah), Kuacha kitu (an-Naqsw) na kuwa na shaka (ash-Shakk).

Sajda ya kusahau (Sujuud as-Sahw) inasujudiwa mara mbili kabla ya kutoa Salaam au baada yake, na imesihi kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alifanya namna zote mbili.

Katika Hadiythi sahihi, amesema Abu Sa’iyd al Khudriy (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 ((إذا شك أحدكم في صلاته فلم يدِر كم صلى ثلاثا أو أربعاً، فليطرح الشك ليبن على ما استيقن، ثم ليسجد سجدتين قبل أن يسلم)) رواه مسلم،

((Mmoja wetu akitia shaka ndani ya Swalah yake akawa hana uhakika ameswali rakaa tatu au nne, basi aache kutia shaka na ahesabu zile alizo na uhakika nazo, kisha asujudu sajda mbili kabla ya kutoa Salaam))  [Muslim]

Maana ya kauli ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliposema: ((Aache kutia shaka na ahesabu zile alizo na uhakika nazo)) ni kuwa; Mtu anapokuwa ndani ya Swalah akatia shaka iwapo yupo katika rakaa ya tatu au ya nne, huwa na hakika kuwa wakati ule keshaswali rakaa tatu, isipokuwa ile ya nne ndiyo anayoitilia shaka. Kwa ajili hiyo anatakiwa ahesabu zile tatu tu alizo na uhakika nazo – na aswali rakaa moja tu kwa ajili ya kukamilisha rakaa nne, kisha asujudu sijda ya kusahau.

Na Allah Anajua zaidi

 

Share