Ukisahau Rakaa Au Kitendo Kisha Ukasahau Pia Kutoa Sajdatus-Sahw Ufanyeje?

 

SWALI:

 je wakati bado uko katika Swalah na ukitanabahi kuwa umesahau kitendo (sio rakaa kamili) na ukawekea nia ya kuwa ukimaliza rakaa zako utafanya "Sijdatus-sahw" kable au baada ya Salaam na ikawa bahti mbaya umeshatoa Salaam na ukanyanyuka bila ya kufanya " Sijdatus-sahw, utafanya nini?  

je ukiwa umesahau rakaa kamili, utafanya nini?

 

 


 

JIBU:

Sifa zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola  wa walimwengu wote, Swalah na Salaam zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu ‘anhum) na watangu wema mpaka Siku ya Mwisho

Kusahau katika Swalah ni jambo ambalo limemtokea Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) jambo ambalo linatupa funzo kwamba yeye ni binaadamu kama sisi. Na kawaida yetu kusahau na ndio maana tukaitwa Insaan, neno lenye asili ya kusahau. Naye Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa alihi wa sallam) aliposahau katika Swalah alitukumbusha hivyo kwa kusema:

 

((إنما أنا بشر مثلكم أنسى كما تنسون ، فإذا نسيت فذكروني)) . رواه البخاري ومسلم

((Mimi ni binaadamu kama nyinyi husahau kama mnavyosahau, hivyo nnaposahau nikumbusheni)) [al-Bukhaariy na Muslim]

Kusahau kwake katika Swalah ni Rahma kwetu kwa kujua hukumu pale tutakapokutana na hayo, na pia kuwa tumeondoshewa mashaka ya kurudia Swalah nzima, na badala yake ni kurudia tu kitendo ikiwa ni cha fardhi na kufanya Sajdatus-Sahw badala yake.

Kwa hiyo Ikiwa umesahau kitendo ambacho ni nguzo ‘rukn’ katika Swalah kama Takbiyra ya kwanza ‘Takbiyratul-Ihraam, au kusimama, au kusoma Suratul-Faatihah au kurukuu, au kuinuka katika rukuu, au kusujudu, au kuinuka katika kusujudu au Tashahhud ya pili au kutoa Salaam upande wa kulia itabidi urudie kitendo hicho ili Swalah yako iwe imekamilika. Tazama Swali la: Vipi Vitendo vya Fardhi na Vya Sunnah Katika Swalah”

Na ikiwa umesahau rakaa kamili ikiwa ni moja au mbili ukakakumbuka wakati bado umo katika Swalah, utainuka kutimiza hiyo rakaa uliyosahau. Na ikiwa umekumbuka baada ya kutoa Salaam basi pia utainuka kuzirudia hizo rakaa kisha utatoa Salaam kisha utafanya Sajdatus-Sahw mbili, kisha utatoa Salaam tena kama ilivyo katika usimulizi ufuatao: 

Na hii inatokana na Hadiyth iliyopokelewa kutoka kwa Ibn Siriyn kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) kuwa amesema:

عَنْ أَبِي هُرَيْرَةَ رضي الله عنه قَالَ : " صَلَّى بِنَا رَسُولُ اللَّهِ صَلَّى اللَّهُ عَلَيْهِ وَسَلَّمَ إِحْدَى صَلَاتَيِ الْعَشِيِّ ـ أي الظهر أو العصر ـ قَالَ ابْنُ سِيرِينَ سَمَّاهَا أَبُو هُرَيْرَةَ وَلَكِنْ نَسِيتُ أَنَا . قَالَ : فَصَلَّى بِنَا رَكْعَتَيْنِ ثُمَّ سَلَّمَ ، فَقَامَ إِلَى خَشَبَةٍ مَعْرُوضَةٍ فِي الْمَسْجِدِ فَاتَّكَأَ عَلَيْهَا كَأَنَّه غَضْبَانُ ، وَوَضَعَ يَدَهُ الْيُمْنَى عَلَى الْيُسْرَى وَشَبَّكَ بَيْنَ أَصَابِعِهِ ، وَوَضَعَ خَدَّهُ الْأَيْمَنَ عَلَى ظَهْرِ كَفِّهِ الْيُسْرَى ، وَخَرَجَتِ السَّرَعَانُ مِنْ أَبْوَابِ الْمَسْجِدِ فَقَالُوا قَصُرَتِ الصَّلَاةُ ، وَفِي الْقَوْمِ أَبُو بَكْرٍ وَعُمَرُ فَهَابَا أَنْ يُكَلِّمَاهُ ، وَفِي الْقَوْمِ رَجُلٌ فِي يَدَيْهِ طُولٌ يُقَالُ لَهُ ذُو الْيَدَيْنِ قَالَ : يَا رَسُولَ اللَّهِ أَنَسِيتَ أَمْ قَصُرَتِ الصَّلَاةُ ؟ قَالَ :(( لَمْ أَنْسَ وَلَمْ تُقْصَرْ)) . فَقَالَ : ((أَكَمَا يَقُولُ ذُو الْيَدَيْنِ؟))  فَقَالُوا : نَعَمْ . فَتَقَدَّمَ فَصَلَّى مَا تَرَكَ ، ثُمَّ سَلَّمَ ، ثُمَّ كَبَّرَ وَسَجَدَ مِثْلَ سُجُودِهِ أَوْ أَطْوَلَ ، ثُمَّ رَفَعَ رَأْسَهُ وَكَبَّرَ ، ثُمَّ كَبَّرَ وَسَجَدَ مِثْلَ سُجُودِهِ أَوْ أَطْوَلَ ، ثُمَّ رَفَعَ رَأْسَهُ وَكَبَّرَ . فَرُبَّمَا سَأَلُوهُ ـ أي محمد بن سيرين ـ :ثُمَّ سَلَّمَ ؟ فَيَقُولُ : نُبِّئْتُ أَنَّ عِمْرَانَ بْنَ حُصَيْنٍ قَالَ : ثُمَّ سَلَّمَ " متفق عليه.

Kutoka kwa Abu Hurayrah (Radhiya Allaahu ‘anhu) ambaye amesema: "Alituswalisha Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) Swalah mojawapo za mchana, (Adhuhuri au ‘Alasiri) [kasema Ibn Siriyn ametaja Abu Hurayrah lakini nimesahau mimi]. Akasema: akaswali rakaa mbili kisha akatoa Salaam kisha akainuka na kukaa akiwa ameegemea nguzo akionyesha dalili ya kughadhibika. Akaweka mkono wake wa kulia juu ya mkono wa kushoto akapachanisha Vidole vyake. Akaweka shavu lake la kulia juu ya upande wa juu wa kiganja chake cha kushoto na akatoka kwa haraka kupitia milango ya msikiti, wakasema (Maswahaba), Swalah imepunguzwa, na miongoni mwao alikuwepo Abu Bakr na ‘Umar (Radhiya Allaahu ‘anhuma) ambao walijizuia wasimsemeshe, na miongoni mwao alikuwepo mtu mwenye mikono mirefu aliyekuwa anayejulikana kwa jina la 'Dhul-Yadayni' aliyeuliza: "Ewe Mjumbe wa Allaah, umesahau au umefupisha?" Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akasema: ((Sijasahau wala haijafupishwa)) kisha Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akauliza: ((Ni kweli maneno anayosema Dhul-Yadayni?)) Wakamwambia: "Ndiyo." Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akainuka, akatangulia mbele (mahali aliposimama alipokuwa akiswalisha), kisha akakamilisha rakaa mbili alizozisahau, kisha akatoa Salaam, kisha akasema: ((Allaahu Akbar)), kisha akasujudu sajda kama ya kawaida au ndefu zaidi kidogo, kisha akakaa, kisha akasema tena: ((Allaahu Akbar)) kisha akasujudu tena kama alivyosujudu mwanzo kisha akakaa. Na huenda walimuuliza – yaani Muhammad bin Siyriyn – kisha akatoa Salaam? Akajibu, nimearifiwa kuwa ‘Imraan bin Huswayn alisema: Kisha alitoa Salaam. [Al-Bukhaariy na Muslim]

Na katika Hadiyth nyingine:

Kutoka kwa ‘Atwaa amesema: "Mwana wa Az-Zubayr (Radhiya Allaahu ‘anhu) aliswalisha Swalah ya Maghribi kisha akatoa Salaam baada ya kuswali rakaa mbili, na aliponyanyuka kutaka kulibusu jiwe (la Al-Ka’abah) watu wakasema: "SubhaanaLlaah!", akarudi na kuwauliza: "Mna nini?" Anasema ‘Atwaa: "Akakamilsha rakaa aliyoiacha kisha akasujudu sajda mbili." [Atw- Twabaraaniy]

Na Allaah Anajua zaidi

Share