Kusoma Khitma Inafaa?

 

Kusoma Khitma Inafaa?

 

 Alhidaaya.com

 

SWALI:

 

Assalamu Alaykum

 Je Sheghe Inafaa kusoma Hitma kwa kukusanya watu. Na hii ni wajibu-[lazima]

 

 

JIBU:

 

Kwanza tunapenda na sisi kutoa shukurani kwa Du’aa zenu nzuri mnazotuombea nyote mnaotuma maswali yenu pamoja na wengineo wanaoingia ALHIDAAYA kutafuta faida mbali mbali. Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atutakabalie hizo Du’aa na Atuzidishie uwezo wa kuelemishana kwa kadiri Anavyotujaalia. Aamiyn.

 

 

Tunashukuru kwa kuuliza Swali hili muhimu la kuhusu kusoma khitmah, jambo ambalo linatendeka katika jamii nyingi za Kiislamu kwa kudhani kwamba ni jambo linalofaa bila ya kuwa dalili yoyote. Na lengo linalokusudiwa la kusoma khitmah ni kuwa thawabu za kusoma Qur-aan zimfikie maiti wakati Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema kuwa hii Qur-aan imeletwa kwa ajili ya kumlingania binaadamu aliye hai na siye alikwishafariki:

 

وَمَا عَلَّمْنَاهُ الشِّعْرَ وَمَا يَنبَغِي لَهُ ۚ إِنْ هُوَ إِلَّا ذِكْرٌ وَقُرْآنٌ مُّبِينٌ ﴿٦٩﴾لِّيُنذِرَ مَن كَانَ حَيًّا 

Na hatukumfunza (Nabiy Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) mashairi, na wala haipasi kwake, hii si chochote isipokuwa ni ukumbusho na Qur-aan bayana. Ili imuonye yule aliyekuwa hai.. [Yaasiyn: 69-70]

 

 

Binaadamu akishafariki, 'amali zake zote huwa zimekatika ila kwa mambo matatu yaliyotajwa katika Hadiyth ifuatayo:

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

 ((إذا مات إبن آدم إنقطع عمله إلا من ثلاث, صدقة جارية , أو علم ينتفع به, أو ولدٌ صالح يدعوا له))  مسلم

"Anapokufa mja hukatika ‘amali zake zote isipokuwa mambo matatu, Swadaqah inayoendelea, au elimu yenye manufaa kwayo, au mtoto mwema anayemuombea". [Muslim]

 

 

Hayo ndiyo mambo yanayomnufaisha maiti ikiwa atayaacha duniani. Na zifuatazo ni Du’aa katika Qur’aan na Sunnah ambazo mtoto anaweza kumuomba mzazi wake, na nyinginezo pia anaweza maiti kuombewana waislam wenzake: 

 

رَبَّنَا اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ وَلِلْمُؤْمِنِينَ يَوْمَ يَقُومُ الْحِسَابُ ﴿٤١﴾ 

"Rabb wetu! Unighufirie mimi na wazazi wangu wote wawili, na Waumini, siku ya kusimama hisabu".  [Ibraahiym: 41]

 

رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا

Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni.  [Al-Israa: 24]

 

...رَبَّنَا اغْفِرْ لَنَا وَلِإِخْوَانِنَا الَّذِينَ سَبَقُونَا بِالْإِيمَانِ وَلَا تَجْعَلْ فِي قُلُوبِنَا غِلًّا لِّلَّذِينَ آمَنُوا رَبَّنَا إِنَّكَ رَءُوفٌ رَّحِيمٌ﴿١٠﴾ 

Rabb wetu! Tughufurie na ndugu zetu ambao wametutangulia kwa iymaan na wala Usijaalie katika nyoyo zetu mafundo ya chuki kwa wale walioamini; Rabb wetu! Hakika Wewe ni Mwenye huruma mno, Mwenye kurehemu. [Al-Hashr: 10]

 رَبِّ اغْفِرْ لِي وَلِوَالِدَيَّ  

Rabb wangu! Nighufurie, na wazazi wangu wawili, [Nuwh: 28]

 

 

Vile vile unaweza kusema:

 

اَللَّهُمَّ اغْفِرْ لِلْمُؤمِنِينَ وَاْلمُؤمِنات وَالْمُسْلِمِينَ وَالْمُسْلِمات اَلأَحْيَاءِ مِنْهُمْ وَالأَمْوَات

Ee Allaah Waghufurie Waumini wanaume na Waumini wanawake, Na Waislamu Wanaume na Waislamu wanawake, Waliohai miongoni mwao na waliokufa.

 

 

Na hii ni Du’aa iliyothibiti katika Sunnah ya kumuombea maiti anaposwaliwa au hata wakati wowote mwingine unaweza kumuombea.

 

اللهُـمِّ اغْفِـرْ لَهُ وَارْحَمْـه ، وَعافِهِ وَاعْفُ عَنْـه ، وَأَكْـرِمْ نُزُلَـه ، وَوَسِّـعْ مُدْخَـلَه ، وَاغْسِلْـهُ بِالْمـاءِ وَالثَّـلْجِ وَالْبَـرَدْ ، وَنَقِّـهِ مِنَ الْخطـايا كَما نَـقّيْتَ الـثَّوْبُ الأَبْيَـضُ مِنَ الدَّنَـسْ ، وَأَبْـدِلْهُ داراً خَـيْراً مِنْ دارِه ، وَأَهْلاً خَـيْراً مِنْ أَهْلِـه ، وَزَوْجَـاً خَـيْراً مِنْ زَوْجِه،  وَأَدْخِـلْهُ الْجَـنَّة ، وَأَعِـذْهُ مِنْ عَذابِ القَـبْر وَعَذابِ النّـار

"Ee Allaah Msamehe na Umrehemu na Umuafu na Msamehe na Mtukuze kushuka kwake (kaburini) na Upanue kuingia kwake, na Muoshe na maji na kwa theluji na barafu na Mtakase na makosa kama Unavyoitakasa  nguo nyeupe kutokana na uchafu, na Mbadilishie nyumba bora kuliko nyumba yake, na jamaa bora kuliko jamaa zake, na mke bora kuliko mke wake, na Muingize Peponi na Mkinge na adhabu ya kaburi (na adhabu ya moto".

 

 

Vile vile kumtolea Swadaqah na kumwendea Hajj au 'Umrah ikiwa hakuwahi kufanya hivyo wakati wa uhai wake.

 

 

Kwa kupata maelezo zaidi yanayohusu uzushi wa jambo hili, tafadhali soma mada inayopatikana katika kiungo kifuatacho:

 

 

Khitmah Kutokufaa Na Madhara Yake

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

Share