Ramadhwaan: Uzushi Wa Swalaah Ya Ijumaa Ya Mwisho Katika Ramadhwaan Kuwa Inafuta Madhambi

 

 

Uzushi Wa Swalaah Ya Ijumaa Ya Mwisho Katika Ramadhwaan

Kukidhia Swalaah Na Kuwa Inafuta Madhambi

 

Alhidaaya.com

 

 

SWALI:

 

Assalaam alykum ndugu zetu tujulisheni usahihi wa Swalaah unasali sunna baada ya sala ya Ijumaa ya mwisho ya Ramdhwaani  ili kulipa  Swaalah ulizokuwa hujazisali yaani sala za kufutika na kwamba unafutiwa madhambi. Naomba kuongozwa      

Jazaakallahukheir fiamanillah

 

 

JIBU:

 

AlhamduliLLaah Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.

 

 

Hilo ni jambo lilozushwa na watu kuhudhuria Swalaah ya Ijumaa ya mwisho ya Ramadhwaan. Kwa kufanya hilo imezuliwa Hadiyth kuwa hiyo ni Jum’atul-Widaa (Ijumaa ya kuaga). Hakika hii hakuna katika Shariy’ah ya Dini yetu.  Na linalozushwa katika Swalaah hiyo ni kwamba    mwenye kuswali siku hiyo basi madhambi ya mwaka mzima amesamehewa hata madhambi makubwa ambayo hajafanya tawbah ya kisawasawa.

 

 

Sunnah za siku hiyo ni kama za kawaida hakuna kabisa eti unakidhi Swalaah za mwaka mzima. Hili ni jambo geni katika Uislamu ambalo halikuwepo wala halitakuwa. Hakuna dalili kabisa ya kauli ya Nabiy (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) kuhusu jambo hilo.

 

 

Nasaha zetu za dhati ni kuwaomba Waislamu waache kuzua na kufuata uzushi na kuongeza au kuzua katika Dini, kwani ‘ibaadah za uzushi kama hizo hazitakuwa na uzito wowote Siku ya Qiyaamah bali yatamuingiza mtendaji motoni kwa sababu ni kumzulia uongo Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) ambaye amesema:

 

 َمَنْ كَذَبَ عَلَيَّ مُتَعَمِّدًا فَلْيَتَبَوَّأْ مَقْعَدَهُ مِنْ النَّارِ  البخاري

"Mwenye kunizulia uongo kwa makusudi, basi ajiandalie makazi yake motoni."  [Al-Bukhaariy]

 

 

Na Allaah Anajua zaidi

 

 

 

 

Share