Mke Anayo Haki Kukataa Kufanya Kazi Za Nyumba?
Mke Anayo Haki Kukataa Kufanya Kazi Za Nyumba?
Alhidaaya.com
Swali La Kwanza:
Naomba kuuliza swali kuhusu haki ya mke. Nimeolewa kwa kipindi cha miaka miwili na hutokezea matatizo mengi kuhusu ufanya kazi nyumbani kama kupika, kuosha kumpijia pasi mume n.k, je kama sikufanya hivo na mume anataka hayo kwa sababu yoyote ile je itakuwa nimekosea na kama sijakosea je hiyo imeandikwa wapi na nnaomba kama itakuwa vizuri kupata japo maandishi ya quran au hadith.
Asanteni.
Swali La Pili:
Naomba kuuliza swali. Mwanamkwe kumpikia mumewe na shughuli za nyumbani kwa ujumla ni wajibu wake au kufanya hivyo ni sehemu ya mapenzi kwa mumewe? Na
kama ni mapenzi ni nani anayestahili kufanya hayo? Allaah awape kila la kheri leo na kesho Aakhirah In shaa Allaah
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Japo dada yetu ameyagawa haya maswali na kuyafanya mawili lakini ni moja tu kwani yanafanana kabisa. Suala hili lina maoni tofauti baina ya wanazuoni mbalimbali.
Maswahabiyaat (Swahaba wa kike) [Radhwiya Allaahu ‘anhunna] walikuwa msitari wa mbele katika kuwahudumikia waume zao. Mfano mzuri ni Faatwimah binti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliyekuwa akimhudumikia mumewe kwa kufanya kazi zote za nyumbani mpaka akamshitakia Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwa aliyokuwa akikumbana nayo mikononi mwake katika kusaga ngano na shayiri [Al-Bukhariy na Muslim].
Na Asmaa’ bint Abi Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhumaa) amesema: "Nilikuwa nikimhudumikia az-Zubayr bin al-‘Awwaam (mumewe - Radhwiya Allaahu ‘anhu) kazi zote za nyumbani. Az-Zubayr alikuwa na farasi niliyekuwa nikimtazama, nikimpatia nyasi na kumsimamia. Alikuwa akimlisha farasi wake na kumnywesha maji, kukanda na kubeba mbegu kichwani mwake kutoka sehemu iliyo na umbali wa maili mbili (kutoka nyumbani kwake)” [al-Bukhariy na Muslim].
Shaykh al-Islaam, Ibn Taymiyah anatuarifu: “Wanazuoni wamezozana (wametofautiana): Je, ni juu ya mke kumhudumikia mumewe kwa mfano kwa kutandika nyumba, kupika chakula, kinywaji, mkate na chakula cha wanyama pamoja na kuwatazama na mfano wake? Wapo wanaosema kuwa si wajibu wake lakini kauli hii ni dhaifu kama udhaifu kwa wanaosema: Si wajibu kuishi na kujamiiana, kwani huku si kuishi nao kwa wema. Panasemwa, na hii ndio kauli sahihi, wajibu wa kumhudumikia, kwani mume ni bwanake (Sayyid) katika Kitabu cha Allaah, naye ni mwenye kuwa na hamu na kunyenyekea kwake katika Sunnah ya Mtume wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Ni juu ya mwenye kunyenyekea (mfungwa) na mtumwa kuhudumu, kwani huo ndio wema. Kisha wapo wanaosema: Ni wajibu wake kuhudumikia kwa kazi nyepesi. Na wengine wanasema: Ni wajibu kuhudumu kwa wema, na hii ndiyo iliyo sahihi. Ni juu ya mke kumhudumikia mumewe kwa wema kwa mfano wao (wanandoa). Hiyo khidmah (huduma) inakuwa tofauti kwa kubadilika hali. Khidmah ya jangwani si kama ya kijijini, na ya kijijini si kama ya aliye dhaifu” (Al-Fataawaa, Mj, 34: uk. 90 -91).
Hivyo, rai ya wanazuoni wa Imaam Ahmad kama Abu Thawr, Abubakar ash-Shaybaaniy na Abu Ishaaq wanaosema ni wajibu wake. Hata hivyo, jamhuri ya wanazuoni wanasema si wajibu wa mke kumhudumikia mumewe na ni juu ya mume kumpatia mkewe msaidizi wa kumsaidia kazi zake.
Muhtasari wa maneno ni kuwa ‘Urf (ada na desturi) za watu ambazo haziendi kinyume na kanuni za Uislamu zinacheza duru kubwa na muhimu katika suala hili. ‘Urf kwa baadhi ya madhehebu ya Ahlus Sunnah ni chimbuko la sheria. Ndio tukaona kuwa Maswahabiyah (Radhiya Allaahu ‘anhunna) wakiwahudumikia waume zao kama mifano tuliyotoa ya Faatwimah binti ya Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na Asmaa’ bint Abi Bakr (Radhwiya Allaahu ‘anhaa) na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakusema wanadhulumiwa. Katika sehemu ya Afrika Mashariki tunayoishi ni ‘Urf kwa mke kumhudumikia mumewe kwa kumpikia, kumpigia pasi na kumfanyia mambo mengineo. Mbali na kuwa kabla ya Nikaah mke ana haki kuweka masharti kama kumtaka mume amuwekee mfanyakazi wa nyumbani ili amsaidie. Au pia mume mwenyewe awe anamsaidia anaporudi kazini.
Hapana shaka kuwa wanandoa wanatakiwa wasaidiane kwa wema kwani Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) Anasema:
وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ
Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah;.. [Al-Maaidah: 2].
Hivyo, mume anatakiwa amsaidie mkewe kama alivyokuwa akifanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). ‘Aaishah amesema: Alikuwa Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akiwasaidia watu wake (wa nyumbani), yaani akiwahudumikia, lakini kipindi cha Swaalah kinapofika alikuwa anatoka kwenda kuswali [Al-Bukhaariy]. Ni juu ya mume kutazama hali ya mkewe na kutombebesha asiyoweza.
Mume anatakiwa atazame mazingira na hali ya mkewe kwani ameamuriwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) pale Aliposema:
وَعَاشِرُوهُنَّ بِالْمَعْرُوفِ ۚ
Na kaeni nao kwa wema.. [An-Nisaa: 19].
Na Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema: "Mcheni Allaah kuhusiana na wanawake kwani wao ni wasaidizi walio kwenu" [Muslim].
Na tena: "Mbora wenu ni mbora wenu kwa familia yake, nami ni mbora wenu kwa familia yangu" [at-Tirmidhiy, Ibn Maajah, ad-Daarimiy na atw-Twabaraaniy].
Kwa hiyo, mume akiwa na wasaa kwa kifedha ni vyema amwekee mkewe msaidizi wa kumsaidia kazi na mke naye anafaa pia asaidie katika baadhi ya kazi na nyumbani kama vile mume naye anafaa kufanya hivyo ili mapenzi yazidi baina yao.
Kwa maelezo zaidi ingia katika kiungo kifuatacho upate maelezo zaidi:
43 Wajibu Wa Mwanamke Kumhudumia Mumewe
Na Allaah Anajua zaidi.
Alhidaaya.com