Radhi Ya Mama Inapasa Katika Hali Gani?
Radhi Ya Mama Inapasa Katika Hali Gani?
SWALI:
Asalaam alaikum, Swali langu radhi ya mzazi inatolewa vipi? Na kwa sababu gani haswa? Mzazi anakutishia kukutolea radhi kila mara ina maana gani? Napenda nipate majibu ya haya mswali halafu nitaelezea historia vipi ilivyo mpaka kufikia kiwango hichi za mzazi, naomba majibu upesi.
Ndugu yenu katika uislamu.
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na salamu zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho.
Hakika inatakiwa ifahamike kwa kila mmoja kuwa wazazi wana haki kwa watoto wao. Hivyo, wanafaa watiiwe katika mema na mazuri na wasiasiwe kabisa katika hilo. Haki hiyo inakuja tu baada ya kumuabudu Allaah Aliyetukuka. Allaah Aliyetukuka Amekariri hilo mara kadhaa katika Qur-aan Yake, mfano ni, Allaah Aliyetukuka Anatuambia yafuatayo:
وَقَضَىٰ رَبُّكَ أَلَّا تَعْبُدُوا إِلَّا إِيَّاهُ وَبِالْوَالِدَيْنِ إِحْسَانًا ۚ إِمَّا يَبْلُغَنَّ عِندَكَ الْكِبَرَ أَحَدُهُمَا أَوْ كِلَاهُمَا فَلَا تَقُل لَّهُمَا أُفٍّ وَلَا تَنْهَرْهُمَا وَقُل لَّهُمَا قَوْلًا كَرِيمًا ﴿٢٣﴾وَاخْفِضْ لَهُمَا جَنَاحَ الذُّلِّ مِنَ الرَّحْمَةِ وَقُل رَّبِّ ارْحَمْهُمَا كَمَا رَبَّيَانِي صَغِيرًا ﴿٢٤﴾
Na Rabb wako Amehukumu kwamba: Msiabudu isipokuwa Yeye Pekee na (Ameamrisha) kuwafanyia ihsaan wazazi wawili. Kama mmoja wao akifikia uzee naye yuko pamoja nawe, au wote wawili basi usiwaambie, Uff! Na wala usiwakemee; na waambie maneno ya heshima.Na wainamishie bawa la unyenyekevu kwa huruma, na useme: Rabb wangu! Warehemu kama walivyonilea udogoni. [Al-Israa: 2324].
Ni maumbile ya mwanadamu anapokuwa ni mzazi kutekeleza majukumu kwa watoto wake – majukumu ya msingi. Hata hivyo, watoto mara nyingi hujitazama wao wenyewe bila kujali kama mzazi anacho au hana. Mwanadamu kimaumbile anapopata watoto hamu yake kubwa ni watoto wake na sio wazazi ambao ndio sababu ya kuja kwao. Kwa ajili hii Allaah Aliyetukuka Akatoa ufafanuzi mrefu kuhusu majukumu ya watoto kwa wazazi wao. Ukumbusho huu umekaririwa mara kadhaa ili kumpatia hisia mtoto atekeleza majukumu yake kwa mzazi wake.
Kiislamu sio hivyo bali kila wazazi wanapokuwa wazee ni nafuu kwetu kwa kiasi kikubwa. Imepokewa kwa Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu 'anhu) kwamba Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Amekhasirika, kisha amekhasirika, kisha amekhasirika yule ambaye atawakuta wazazi wake wawili wakiwa wazee, mmoja au wote kisha asiingie Peponi?" [Muslim]
Hakika wazazi kuwa wazee ni neema na ni mlango wa mtu kuingia Peponi.
Na hakika ni kuwa kumuasi mzazi au kumpenda mtu mwingine kama mke kuliko wao kunakupelekea katika madhambi na pia huenda ukaingia Motoni.
Utiifu kwa wazazi unakuja baada ya utiifu kwa Allaah Aliyetukuka lakini utiifu kwa wazazi una mipaka. Ipo hali moja ambayo mtoto hafai kumtii mzazi wake nayo tumefahamishwa na Allaah katika Qur-aan. Allaah Anasema:
وَإِن جَاهَدَاكَ عَلَىٰ أَن تُشْرِكَ بِي مَا لَيْسَ لَكَ بِهِ عِلْمٌ فَلَا تُطِعْهُمَا ۖ وَصَاحِبْهُمَا فِي الدُّنْيَا مَعْرُوفًا ۖ
Lakini wakikushikilia kuwa Unishirikishe na ambayo huna elimu nayo, basi usiwatii. Na suhubiana nao kwa wema duniani,.. [Luqmaan: 15]
Hii ni hali ambayo hufai kuwatii kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
"Hakuna utiifu kwa kiumbe katika kumuasi Muumba".
Hata hivyo, katika hali yoyote ile ni lazima uwatii na hata wakikuamrisha mabaya wewe hufai kuwatii tu lakini unatakiwa usuhubiane nao kwa wema hapa duniani. Sababu ni kuwa haki yao ya uzazi haipomoki (haiondoki) kwa wao kufanya ubaya au kuamrisha mabaya.
Tatizo tulilo nalo sisi ni kuwa huwa tunakaidi amri zao katika mema kwa sababu tu tumekuwa sisi tunajiweza kutekeleza ya kwetu na hilo sio sawa kwetu. Ikiwa tutakosa kuwatii katika mema basi wakitoa radhi zao huwa Allaah Aliyetukuka Anawaitikia hivyo kukuweka wewe mahali pabaya.
Wakati mwengine wazazi nao huwa wana makosa wanataka watoto wao wawatii katika maasi na maovu na wakikosa kutiiwa basi huwa wakali na kutishia kutoa radhi zao. Katika hili la pili hata wakitoa radhi zao huwa bado wewe uko katika radhi za Allaah Aliyetukuka.
Tunamuomba Allaah Aliyetukuka Atupe masikilizano na wazazi na Atufishe hali wakiwa radhi nasi, nasi pia tuweze kuwatimizia katika mema wanaotuamrisha.
Na Allaah Anajua zaidi