Zingatio: Bado Mali Haijaisha…Endelea Kuitafuta!
Zingatio: Bado Mali Haijaisha….Endelea Kuitafuta!
Naaswir Haamid
Nafasi ya kumuabudia Rabb wetu tumeiondosha na kuifanya mali ndio bendera yetu ya iymaan. Hali ya kuwa hiyo mali si kitu mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Je, hatuoni namna mali inavyokimbia? ukiipata inakuwa mtihani na kuikosa halikadhalika. Matumizi hayeshi ila wakati unakwisha.
Yareti Waislamu wote wangeliitikia wito wa Qawl ya Rabb Aliposema: ‘Iqra-a’ pamoja na mahimizo ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) juu ya kuitafuta elimu, tusingelifikia hali ya kuwa sawa na wendawazimu katika kuitafuta mali. Tuipitie pamoja Hadiyth ifuatayo:
Kutokana na Mahmuud bin Lubayd (Radhwiya Allaahu ‘Anhu), amesema kwamba, amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) “Mambo mawili binaadamu anayachukia: anachukia mauti na mauti ni kheri kwake kutokana na fitnah, anachukia uchache wa mali, na uchache wa mali ni uchache wa hisabu” [Imepokewa na Ahmad]
Tuelewe ya kwamba vyote tunavyovichuma hapa duniani tutaenda kuulizwa mbele ya Muumba, na ndio sababu Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) akatuambia kuwa uchache wa mali ni uchache wa hisabu. Tukumbuke kwamba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atakwenda kutuuliza juu ya kila neema Aliyotupatia kwa Qawl Yake:
ثُمَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ ﴿٨﴾
Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema. [At-Takaathur: 8]
Tunadhani ya kwamba nafsi itakinai mbele ya mali? Na haikuwa nafsi ila ni yenye kuamrisha maovu. Kila kukicha tunaendelea kuwa na uchu wa mali hali ya kuwa hiyo mali haina mwisho abadan! Ni vyema tukaelewa kwamba Allaah Hana haja ya kuangalia wingi wa mali wa mtu wala sura yake. Anachokiangalia ni a’maal ambazo wingi wetu tumeacha kutekeleza. Kama tunategemea mali kuwa ni muokozi wetu hapa duniani, tujiweke tayari na Moto unaoitwa Hut wamah ambao hakuna miongoni mwetu anayeweza kuuvumilia. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
الَّذِي جَمَعَ مَالًا وَعَدَّدَهُ ﴿٢﴾ يَحْسَبُ أَنَّ مَالَهُ أَخْلَدَهُ ﴿٣﴾ كَلَّاۖ لَيُنبَذَنَّ فِي الْحُطَمَةِ ﴿٤﴾
Ambaye amekusanya mali na kuyahesabu. Anadhani kwamba mali yake itamdumisha milele. Laa hasha! Atavurumishwa katika Al-Hutwamah (moto mkali unaonyambua nyambua). [Al-Humazah: 2-4]
Na ukoje huo moto uitwao Hutwamah? Huo ni moto uliowashwa ukawa mkali usio na mfano wa moto wowote unaoufahamu hapa duniani. Na moto huo utamchoma mtu nje na ndani ya mwili wake ukapita na kuingia hadi kwenye moyo na wakiwa wamefungwa kwa magogo marefu mrefu pasiwe na upenyo wa kutokea.
Hakuna masikhara mbele ya Rabb Mtukufu, kwani kubwa litaingizwa kwenye mizani na dogo halitatoka. Yote yatakuwa na hisabu yake kamili, wala hakuna ambaye uvumbuzi wake wa teknolojia utayafanya matendo yake yasiwekwe katika Miyzaan. Mali haina mwisho hadi Qiyaamah, ila tambua ya kuwa rizki ya kila mmoja imeshaandikwa!