Zingatio: Simu Zitatuangamiza
Zingatio: Simu Zitatuangamiza
Naaswir Haamid
Kwa vile tupo kwenye “utandawazi” wa ukafiri ndani ya jamii zetu, imekuwa ni vigumu kuepukana na usawa wa maadili ya Magharibi. Hata hivyo, bado tuna nafasi ya kushindana na ukafiri kwa vitendo na kauli zetu. Ni vyema kila mmoja akachukua hadhi yake aliyonayo kukomesha maadili potofu angalau kwa kukemea na kuachana nayo. Kwani hakuna anayelazimishwa kuyafuata kwa mtutu wa bunduki.
Uislamu wetu ni njia maridhawa ya kuifuata kwa kila hatua tunayopiga. Ni njia isiyokubali mfumo wowote wa kuhamasisha muziki, ikiwa ni kwa kuimba, kutia miziki, kununua, kubeba au vyenginevyo. Vivyo hivyo, haifai kwa Muislamu kuwa na yale mawazo ya watu wa Magharibi wanaosema: “When You Are In Rome, Do As The Romans Do” – Unapokuwa Roma Fanya Kama Warumi Wafanyavyo. Bila ya kuona hayaa, Waswahili nao wameanzisha msemo unaofanana nao “Liingialo Mjini Si Haramu”. Yote haya ni maneno ya uzushi yasiyolingana na mafunzo ya Uislamu na yanafaa kupigwa vita kwa vitendo na kauli.
Ni kutokana na misemo hiyo, tunaona vijana kwa wazee wakibeba simu zenye kushehena kila aina ya muziki, sio tu majumbani bali mpaka misikitini Subhaana Allaah! Wengine wanakwenda mbali hadi kuingiza ndani ya simu zao mambo ya kuchefua roho kama vile picha au michezo ya kuhamasisha uasharati. Hapa ndipo tunapojiangamiza kwa kujua au wengine kwa ujinga wetu tu.
Je! Kuna tofauti ya Muislamu aliyeingia msikitini akiwa amebeba seti nzima ya redio na yule ambaye amebeba simu yake yenye miziki ya waimbaji wa kila namna? Waislamu tutafakari kwa kutumia kanuni za Kiislamu katika kila hatua ya maamuzi tunayofanya juu ya maisha yetu. Ama si hivyo, tutageuza misikiti yetu sawa na makanisa yaliyojaa kila aina ya ala za muziki. Huenda Waislamu wakawashinda hata Wakristo kwa kuingia na sinema zenye uasharati ndani ya misikiti yao.
Sio vyema kuvamia kila aina ya teknolojia na kuitaka kuitumia hata kama ikiwa ni yenye kupelekea kwenye maadili potofu. Tunachohitaji kuzingatia hapa; sio kwenda msikitini bila ya simu, kuitoa sauti au kuizima simu pale tu unapoingia msikitini. Laa hasha! Lengo ni kuondosha huu uovu kwa kufuta aina zote ya maadili maovu ndani ya simu zetu na kuachana kabisa kuweka miziki ndani ya simu zetu.
Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema kwamba:
“Kutakuwa na watu miongoni mwa ummah wangu watakaofanya kuwa ni ruhusa uzinifu, Hariri, ulevi na ala za muziki...” [Imesimuliwa na al-Bukhaariy, 5590].
Hadiyth hii inaonesha kwamba ala za muziki ni haramu kwa njia mbili. Kwanza, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:
“watakaofanya kuwa ni ruhusa,”
Ambayo inaonesha wazi kwamba vitu vilivyoainishwa – vikiwemo ala za muziki – haviruhusiwi ndani ya Shari’ah, lakini watu watavifanya kuwa ni vyenye kuruhusiwa. Pili, ala za muziki zinatajwa pamoja na vitu vyengine ambavyo haviruhusiwi, navyo ni uzinifu na ulevi. Kama ala za muziki zisingelikuwa ni haramu, zisingelitajwa pamoja navyo. (as-Silsilah as-Swahiyhah ya Imaam al-Albaaniy, 1/140-141)
Hapa ndipo inapoonekana tofauti ya Muislamu na Muumini. Kwani wanapoambiwa waumini husema:
وَقَالُوا سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ
“Tumesikia na tumetii..” [Al-Baqarah:285].
Nasaha zetu kwa Waislamu ni kuweka milio ya kawaida tu isiyo na miziki. Hili litatutofautisha na Makafiri, kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametukataza kujifanananisha nao. Kukosa kufuata maagizo ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ni kujitakia maangamizi ambayo ndio tunayaona kila pembe ya dunia hii. Mara kimbunga, tetemeko la ardhi, mvua kali, ajali za ndege na mengineyo. Maafa ambayo yamechaga kwa ufedhuli wa matendo yetu.