Zingatio: Hii Sio Njia Ya Uislam
Zingatio: Hii Sio Njia Ya Uislam
Naaswir Haamid
Ndege yu angani, anaruka huru bila ya bughudha wala ya vikwazo. Mwanaadamu yupo chini akimwangalia kwa uwezo aliopewa wa kuwa na mbawa. Mwengine anaangalia mwezi ulivyo mbali na kuwa na ndoto za kuufikia. Ndipo uvumbuzi wa ndege zilizotengenezwa na mwanaadamu zikaibuka hadi kutufikia sisi, tukipelekwa mji mmoja kwenda mwengine.
Haya yote yametokana na uwigo wa mwanaadamu kwa kuwaza na kujiuliza: “mbona kaweza mimi nishindwe?” Maendeleo ya teknolojia hayakukomaa hapo tu bali yakachukua mkondo namna ya uyoga utambaavyo. Hadi sasa tunashuhudia mengi kupitia kwenye runinga, mtandao, redio na magazeti. Bahati mbaya, teknolojia imeleta mengi ya uzushi na yasiyoendana na utamaduni wa Uislamu.
Magharibi wakaweka vipindi vyenye kuonesha na kushajiisha utamaduni usiojulikana asili yake. Humo tunawaona wanaadamu wakiwa na wigi kichwani, wengine wametiwa blichi au kuchongwa nyusi, nguo za utupu kabisa, wamevaa suruali karibu ya kuvuka, mikato isiyoeleweka na mengi mengineyo.
Dada zandu ndani ya Uislamu wakaanza kuyaiga hayo yote bila ya kupima. Anaweka rungu la rasta kichwani mwake na anapotaka kujikuna kichwani ni lazima atafute kilipo kijiti. Nguo za “mini skirt” zina wenyewe na kwa mazingira wanayoyaelewa. Dada zangu wanazivaa hadi uswahilini kwenye masoko au ndani ya daladala. Ole wake atake kuketi au kuokota kitu kilichomdondoka! Mikono yake itaitafuta sketi hali ya kuwa inamalizia juu ya mapaja. Viatu vya kisigino au vya mapande mithili ya tofali vinavaliwa, na miguu inapomuuma asingizie nini?! Mwili wa mwanamke ni stara iliyostiriwa ndani ya Uislamu. Dada zangu wanatoka na “jeans” au suruali sawa na miili yao, utaipata wapi stara zinapokukuta siku zako ghafla moja?
Kaka zangu ndani ya Uislamu nao wapo bega kwa bega ndani ya maasi hayo. Suruali zinazoburura mfano wa gari linalozoa taka ndizo “style” ya wengi. Kuna mtindo wa uvaaji unaotambulika kwa jina la “kukata K” ambapo suruali hufungwa chini ya makalio au karibu ya kuvuka kabisa. Hizi ndizo zinazovaliwa, utawaona wavulana wameshughulika kuziweka sawa sururali zilizovaliwa hivyo, mara anataka kuadhirika kwa kukaribia kuonekana nguo yake ya ndani. Kwa vile wameona kwenye runinga “bradhameni” amevaa vidani, bangili na herini, basi nao watataka kuiga kwa kuweka kilo za macheni katika vifua vyao. Anapotokezea Muumini anakatisha chochoro kujificha asipate kupatiwa da’awah.
Bado sielewi mantiki ya dada na kaka zangu kufanya mambo hayo; ikiwa ni kwa biashara au ni wigo tu? Naamini haitakuwa makosa kuwajibu; ni ulimbwembwe wa uwigo wa mwanaadamu na kuonekana “wanakwenda na wakati”. Wanaofanza haya sio Joni wala Eliza! Bali ni hao kina Ali na Fatuma. Ingawa yanashushiwa heshima yake na yanakosewa lafdhi yake, asili ya majina haya ni yenye taariykh tukufu.
Ni vyema tukawauliza ndugu zetu wanaosema ni Waislamu; je hiyo ndio njia aliyotuchagulia kuifuata Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)? Bali sivyo! Mila za Uislamu hazipo hivyo kwa kujitia mashakani na tabu. Kwani Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametufundisha tabia bora kabisa kwa kutumia kivazi kuwa ni stara na amesema:
“Kwa hakika nimeletwa kuja kukamilisha (kufundisha) tabia njema.” [Imesimuliwa na Abu Hurayrah (Radhwiya Allaahu ‘Anhu]. Al-Haythamiy, Majmaa az-zawaaid, Al-Albaaniy, Silsilatul Ahaadiyth Asw-Swahiyhah na Swahiyhul Jaami’.
Nayo Qur-aan inatuambia kwamba:
وَمَن يُشَاقِقِ الرَّسُولَ مِن بَعْدِ مَا تَبَيَّنَ لَهُ الْهُدَىٰ وَيَتَّبِعْ غَيْرَ سَبِيلِ الْمُؤْمِنِينَ نُوَلِّهِ مَا تَوَلَّىٰ وَنُصْلِهِ جَهَنَّمَ ۖ وَسَاءَتْ مَصِيرًا ﴿١١٥﴾
Na atakayempinga Rasuli baada ya kuwa imeshambainikia uongofu na akaifuata njia isiyokuwa ya Waumini; Tutamgeuza alikogeukia na Tutamuingiza Jahannam. Na uovu ulioje mahali pa kuishia. [An-Nisaa: 115]
Ni haramu kuchanganya kivazi baina ya mwanamke na mwanamme. Kwani kila mmoja baina yao kapewa umbile lakekwa vile maisha yake yanavyokwenda. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):
“Allaah kamlaani mwanamme mwenye kuvaa vazi la kike, na mwanamke mwenye kuvaa vazi la kiume. Kama alivyowalaani wale wanaume wenye kujifananisha na wanawake, na wanawake wenye kujifananisha na wanaume.” [Imepokewa na Bukhaariy]
Kwa kila hatua tunayoipiga, ni lazima tuzingatie kwamba kuna Uislamu wetu ambao ndio kigezo chetu. Haitakuwa busara wala jambo linaloingia akilini kuona Waislamu wakifuata nyendo za Magharibi. Vigezo vya kuiga “fashion show” au “kwenda na wakati” havina mnasaba ndani ya masuala Aliyokwishatuhukumia Rabb.