Zingatio: Je, Majina 99 Ya Allaah Kazi Yake Ndio Hii?
Zingatio: Je, Majina 99 Ya Allaah Kazi Yake Ndio Hii
Naaswir Haamid
Ni jambo la kushangaza kuona ndugu wa Kiislamu wakitumia mambo yenye kushabihiana na itikadi zisizo sahihi, ambayo hayana msingi thabiti wa itikadi sahihi anazotakiwa kuzifuata Muislamu.
Tukumbuke kwamba kutumia mambo ya uzushi ni kuwasaidia wengine kupenyeza itizadi zisizo sahihi na hili Rabb wetu Hatutaki kusaidiana katika madhambi na uadui. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
وَتَعَاوَنُوا عَلَى الْبِرِّ وَالتَّقْوَىٰ ۖ وَلَا تَعَاوَنُوا عَلَى الْإِثْمِ وَالْعُدْوَانِ ۚ وَاتَّقُوا اللَّـهَ ۖ إِنَّ اللَّـهَ شَدِيدُ الْعِقَابِ ﴿٢﴾
Na shirikianeni katika wema na taqwa, na wala msishirikiane katika dhambi na uadui. Na Mcheni Allaah; hakika Allaah ni Mkali wa kuakibu. [Al-Maidah, 2]
Miongoni mwa mambo yanayofanywa kuwa ni ya fadhila, ni kutumia majina 99 ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) yenye kuenezwa kwenye mtandao na hata kutungiwa vitabu vidogo kwa lugha kadhaa yenye kumuhakikishia Muislamu kuwa akisoma jina fulani atapata jambo fulani, kama mtoto, utajiri, umaarufu, kupendwa n.k. Hili lafaa kuchungwa, kwani hakuna njia ya kuhakikishiwa ghaibu. Kwa sababu funguo za siri ya ghaibu Anazo Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) peke Yake:
وَعِندَهُ مَفَاتِحُ الْغَيْبِ لَا يَعْلَمُهَا إِلَّا هُوَ ۚ
Na Kwake (Allaah) zipo funguo za ghayb; hakuna azijuaye ila Yeye tu. [Al-An'aam, 59]
Utakapoziangalia vyema fadhila nyingi zilizotajwa ndani ya majina 99, utagundua kuwa zinapingana na Diyn. Hizo fadhila hazipo katika Qur-aan wala Sunnah, ni mambo ya kudanganya watu wasio na hima ya kusoma Diyn yao wala kujiongezea elimu, na haswa zaidi wale wenye kupenda mkato (shortcut) kwenye Diyn na wanaotaka wapate thawabu bure bure kwa mambo yasiyofaa kama hayo. Utakuta wengine hata kuswali hawaswali, lakini du'aa du'aa na maombi kama hayo yanayoenezwa kuhusiana na maajabu yanayofanywa na majina 99 hawayaachi kwenye siku zao.
Ajiulize Muislamu, iwapo atashikamana na nyiradi kama hizo, huo wakati wa kuipitia Qur-aan na Sunnah atakuwa nao? achilia mbali huo mzigo mzito wa kuzipitia nyiradi hizo. Hili bila ya shaka ni taklifu na Diyn yetu haijatuletea mambo ya uzito kama haya.
Kuna vitu ambavyo Muislamu anatakiwa kuwa makini navyo mno, ama si hivyo atajikuta anatumbukia kwenye ukafiri, shirki ama upotofu mwengine. Mifano ifuatayo yaweza kutupatia mwangaza juu ya upotofu unaofanywa kwa kutumia majina hayo 99 ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):
Mtu akiandika Al-'Adl baada ya kula mkate tena wakati wa usiku atapata jambo fulani, hili ni shirki.
Anayetamka jina la Al-'Aziyz kwa siku 40 ataacha kuhitaji kwa watu, hili Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hajatufunza isipokuwa ametutaka kufanya kazi na hata yeye mwenyewe alikuwa muhitaji kwa watu wengine.
Tamko la Al-Baatwin mara tatu kwa siku ataona ukweli wa mambo, hii ni ghaibu na hakuna wa kumhakikishia kuelewa ukweli wa jambo fulani.
Tamko la Al-Haafidhw mara 70,000 baada ya kufunga siku tatu, ataepushwa na adui, Nabiy na jeshi lake walikuwa wakijinoa kwa ucha Mungu na mbinu za vita, nyiradi hiyo ni batili.
Tamko la Al-Khaaliq wakati wa usiku itawezesha kuumba malaika, uumbaji wa viumbe ni uwezo wa Rabb wetu pekee, kinyume cha imani hii ni ukafiri.
Fafanuzi nyengine za uzushi ndani ya majina hayo ni tamko la Ar-Rahmaan mara mia moja ambalo lasemekana linaongeza akili, mbona tunawajua wanaosoma lakini bado akili zao nzito kabisa?
Pia yasemekana kwamba mwenye kusema An-Naafil siku nne mfululizo ataepushwa na madhara, njia sahihi ya kuomba kuepushwa na madhara ni kuomba dua'a sahihi wala sio kupitia njia za uzushi kama hizi.
Au kusoma Al-Ahad mara 1000 inafungua siri kadhaa. Lakini juu ya kuisoma, bado yanabaki mambo zaidi ya 10000 asiyoyajua.
Hayo yaliyotajwa hapo juu ni majina manane tu ya Allaah, ni baadhi tu ya uzushi uliomo ndani ya barua pepe hizo na vijitabu hivyo, lakini bado yamebaki majina 91 ya kuyatolea ufafanuzi, kibarua ambacho ni kipevu chenye kuhitaji muda na nguvu zaidi kufafanua uovu uliomo humo. Hata hivyo, makala hii imshajiishe Muislamu kuacha kudanganywa na kutapeliwa, tena mchana kupe kupe!
Ni vyema ieleweke kwamba hatupingi uwezo wa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) katika jambo lolote, isipokuwa kinachopingwa hapa ni fafanuzi zilizomo ndani ya majina hayo, zenye kumuhakikishia Muislamu fadhila zisizokuwa za kweli ambazo hazikuelezwa na Allaah wala Nabiy Wake!
Tunawakumbusha na kuwahimiza Waislamu pamoja na nafsi zetu kushikamana na Kitabu cha Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) nacho ni Qur-aan pamoja na Sunnah ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Nayo haipatikani kwa kuangalia TV pamoja na kufuatilia ratiba za mechi za mpira. Bali ni kuisaka elimu ya Kiislamu ndani ya madarsa mbali mbali. Kwa uchache Muislam anaweza kujinufaisha kwa elimu katika www.alhidaaya.com huku akihudhuria madarsa na kukaa na Waalimu wa Diyn waliobobea wenye kuaminika elimu yao na uchaji.