Zingatio: Tambua Kwamba Muziki Ni Haramu

 

Zingatio: Tambua Kwamba Muziki Ni Haramu

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Kwa maisha ya leo yalivyo, ustaarabu ambao unafanana na wa mnyama, utaonekana ni mtu wa maajabu kutoa kauli ya kwamba muziki haufai kabisa kabisa. Badala yake, ndio kwanza wanatengeneza matamasha na kuyaita: "Save The Music" yaani "Linda/Hifadhi Muziki (usipotee)". Na si wengine wenye kuyaandaa hayo isipokuwa wanaojiita Waislamu!

 

Kwa hakika Qur-aan na Sunnah yake Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) vyote kwa pamoja vimetoa makemeo makali juu ya muziki na ala zake zote. Hii ni amali ambayo inamtia Muislamu uziwi wa masikio na upofu wa kuifuata dini yake.

 

Kwa hakika itachukua kurasa kwa kurasa kuwasilisha mbele yenu dalili za kwamba muziki ni haramu. Hiyo yote yaonesha kuwa muziki umepigwa marufuku ndani ya Uislamu. Baadhi tu ya uthibitisho huo ni kama zifuatazo:

 

وَمِنَ النَّاسِ مَن يَشْتَرِي لَهْوَ الْحَدِيثِ لِيُضِلَّ عَن سَبِيلِ اللَّـهِ بِغَيْرِ عِلْمٍ وَيَتَّخِذَهَا هُزُوًا ۚ أُولَـٰئِكَ لَهُمْ عَذَابٌ مُّهِينٌ ﴿٦﴾

Na miongoni mwa watu, yuko ambaye hununua maneno ya upuuzi ili apoteze (watu) njia ya Allaah bila elimu, na huichukulia mzaha. Hao watapata adhabu ya kudhalilisha.  [Luqmaan: 6]. Kwa tafsiri ya Swahaba na Maimaam, ‘maneno ya upuuzi’ ni Muziki.

 

Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) yaonesha kwamba uharamu wa zinaa na pombe unakwenda sambamba na muziki. Akaendelea kueleza kuwa ipo siku hao wenye kukumbatia vitendo vichafu hivyo watageuzwa manyani na manguruwe:

 

"Watakuweko watu katika Ummah wangu watakaojaribu kuhalilisha zinaa, uvaaji wa hariri, pombe na muziki. Baadhi ya watu watakuwa pembeni mwa mlima na mchungaji wao atawajia jioni na kuwaomba haja (fulani). Watasema: "Rudi kesho". Allaah Atawaangamiza usiku, Atawaangushia milima kisha Atawabadilisha waliobakia wawe nyani na nguruwe na watabakia hivyo hadi siku ya Qiyaamah." [Al-Bukhaariy]

 

Basi tambua na elewa kwamba muziki na vionjo vyake vyote ni haramu. Zingatia vizuri namna ulimwengu wa leo ulivyojaa muziki ambao Muislamu asipokuwa makini ataona ni halali. Muziki ndani ya idhaa za redio, TV, matangazo ya biashara, michango ya huduma za jamii kunafanyika matembezi ya hisani lakini yakiongozwa na ibilisi (ngoma), ufunguzi wa majengo na kwenye masherehe ndio hakusemeki.

 

Sio hayo tu, baadhi ya Waislamu wanadiriki hadi kupiga miziki kwenye misiba wakisema huu mziki wa kuomboleza! Na masikitiko makubwa ni kuona ndugu wa Kiislamu wafanyao kazi kwenye idhaa zenye kuchangiwa na Waislamu wakizipiga vilivyo ala zote za muziki. Wanapoambiwa wanajibu kwamba huo sio muziki bali ni kasida au Nashiyd na madufu tu. Kwani piano, gita, mazumari, yamegeuzwa jina na sasa kuitwa madufu!?

 

Waislamu nyoyo zetu zimelala fofofo, tumegubikwa na wingu kubwa la ujahili ambao unatusababisha kuwa ni wenye kutawaliwa karne kwa karne sasa. Michezo ya sinema, michezo ya watoto na kila aina ya starehe hainogi bila ya kuwa na muziki. Umefika wakati Waislamu wakatafuta ya maana badala ya kutawaliwa na muziki katika kila pembe ya maisha yao.

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa) Aturuzuku khatima njema na tunatumai kuwa ndugu zetu ambao bado wako katika maasi haya, watakaposoma makala hii, itakuwa ni zingatio kwao na kumkhofu Rabb wao Mtukufu kwa kujiepusha na uharamu huu na kubaki katika Radhi Zake Allaah (Subhaanahu wa Ta'aalaa).

 

Share