Zingatio: Homa Ya Urembo
Zingatio: Homa Ya Urembo
Naaswir Haamid
Simulizi ya Fisi kuvizia mkono wa binaadamu akidhani utadondoka ili apate kuula ni afadhali kuitanabahisha ingawa haina usahihi wowote. Ila tutaitumia kuonyesha athari ya kuwa na uchu usio na mipaka.
Waislamu tumekuwa na uchu wa kutafuta mali, pumbazo na anasa mfano wa huyo Fisi kuuvizia mkono akidhani utadondoka. Lakini wapi?! Haudondoki asilani kiurahisi. Tofauti ya Fisi na sisi Waislamu ni kwamba tunaiga sana mila za Kimagharibi tukidhani tutaendelea namna walivyo wao. Khatma yake, hatuna hatua tunayokwenda mbele ila ni kurudi nyuma kimaadili, kitabia na kubwa zaidi ni kuuacha Uislamu wetu.
Uislamu umekuja kumkomboa mwanamke kwa kumpa heshima ‘adhiymu kabisa sio namna Magharibi wanavyomfanya kuwa ni kinyago kwa kumtoa mbele ya matangazo ya biashara huku asilimia 90% ya faida hiyo ikiingia kwao wavulana. Hii yote imetokana na binaadamu kugandana mno na pumbazo za dunia. Hata kama wakipatiwa ukumbusho huukana na kufanana na mbwa ambaye akipigiwa ama asipigiwe kelele, yuhema tu. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:
وَلَوْ شِئْنَا لَرَفَعْنَاهُ بِهَا وَلَـٰكِنَّهُ أَخْلَدَ إِلَى الْأَرْضِ وَاتَّبَعَ هَوَاهُ ۚ فَمَثَلُهُ كَمَثَلِ الْكَلْبِ إِن تَحْمِلْ عَلَيْهِ يَلْهَثْ أَوْ تَتْرُكْهُ يَلْهَث ۚ ذَّٰلِكَ مَثَلُ الْقَوْمِ الَّذِينَ كَذَّبُوا بِآيَاتِنَا ۚ فَاقْصُصِ الْقَصَصَ لَعَلَّهُمْ يَتَفَكَّرُونَ ﴿١٧٦﴾
Na lau Tungelitaka Tungelimnyanyua kwazo (hizo Aayaat), lakini aligandamana na dunia na akafuata hawaa zake. Basi mfano wake ni kama mfano wa mbwa, ukimhujumu ananing’iniza ulimi nje na kuhema, na ukimwacha pia ananing’iniza ulimi nje na kuhema. Hivyo ndiyo mfano wa watu waliokadhibisha Aayaat Zetu. Basi simulia visa huenda wakatafakari. [Al-A’araaf: 176]
Kumekuwa na mitindo ya kutetea haki za wanawake kwa minajili ya kumtoa mbele ya kadamnasi bila ya kuangalia athari zake kimaadili na ubinaadamu. Kwa kisingizio hicho ndio tunapata haya mashindano ya urembo ambayo ni vyema yakafikia kikomo haswa kwa Waislamu.
Ushiriki wa wanawake kwenye nyanja hizi za urembo umeshuhudiwa kuwa na matokeo ya upotofu wa maadili na tabia mbovu kabisa za uzinzi. Ajabu kubwa, wanapohojiwa wanaeleza ya kwamba; mashindano ya urembo ni kipaji tu cha kazi kama zilivyo kazi nyingine! Jibu hilo laenda sambamba na wanamuziki. Wakisema kuwa kazi hizo sio uhuni na yafaa kwa vijana kushiriki kwa bidii zote. Jee, wataka tueleza ya kuwa kuvaa jeans/miniskirt kwa mwanamke na kusokota rasta kwa mwanamume sio uhuni? Mwanamume aliye jamadari mzima akivaa vidani na mapete mithili ya mwanamke ni sawa? Iwapi tofauti yao ya jinsia?
Mwanamke wa Kiislamu ametukuzwa kwa kuwekewa kanuni maalum za kivazi ili asipotoshwe na jamii. Mwanamke wa Kiislamu hatakikani kuwa na uchu wa urembo nje ya kuta za mumewe na Mahariym wake. Badala yake, mwanamke anasukumwa mbele ya kioo cha saluni kwa dakika zisizopungua 30 huku ameridhika kuumbuliwa kwa kutolewa nyusi na kuchongwa meno. Baada ya hapo, kinachofuatia si chengine ila ni fitnah kwa wavulana waliopo vibarazani na kuwaingiza kwenye dimbwi la zinaa. Wanawake wengine wanaotoa miguu hapo saluni hupata hasara ya kuvutwa kushiriki kwenye mashindano ya urembo akidhani ni bahati nzuri kwake. Atatolewa mbele ya kadamnasi amevaa mithili ya mtu aliyekosa akili. Lengo kuu la kushiriki hayo mashindano sio chochote ila ni kupata macho ya watu, kujiuza kwa bei rahisi, umaarufu na tunuku.
Huenda huyo mshiriki asiwe na athari za moja kwa moja, lakini jamii inaachiwa kovu baya kabisa na mabomu ya kuwapotoza vijana kujiingiza kwenye dimbwi hilo huku wakisaka hizo fedha na bahati mbaya ni wachache mno wenye kufikia huko aliyeshinda mshindi. Athari ya mambo haya sio ngeni kuziorodhesha kwa jamii yetu. Kwani tunashuhudia ongezeko la mimba zilizo nje ya ndoa, utoaji wa mimba kwa wanafunzi, ubakaji, wizi na mengineyo.
Dawaam wa dawaam tuelewe kwamba, tutakuwa ni wenye kukhasirika kwa kukosa miongozo ya diyn yetu ya Kiislamu.