Zingatio: Kizuri Tunakiacha Kibaya Tunakifukuzia
Zingatio: Kizuri Tunakiacha Kibaya Tunakifukizia
Imetayarishwa Na: Naaswir Hamid
Dunia ni kubwa lakini sio kwa Rabb Muumba. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Ametuongoza njia njema ili tupate kuifuata. Qur-aani Ametuletea ili iwe ndio sababu ya kufuzu kwetu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) tukaletewa awe ni fundisho kwetu. Badala yake tumeacha, tumeasi na tunafanya maasi kwa kujua, kwa kejeli au kwa dharau.
Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Yupo na daima Atakuwepo, Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ameacha Sunnah yake na Kitabu Kitukufu Qur-aan; kuwa ndio muongozo sahihi kabisa.
Enyi Waislamu, basi hatukumbuki vyakula na vinywaji halali vya kuvifuata na kuvitumia? Tunafanana na Mayahudi walioshushiwa kulla aina ya vyakula bado wakaasi? Tunaacha vinywaji halali chungu nzima na kufukuzia pombe yenye madhara na iliyoharamishwa kwa kila Muislamu. Qauli ya Rabb Wetu Mlezi yafaa kunukuliwa:
يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا إِنَّمَا الْخَمْرُ وَالْمَيْسِرُ وَالْأَنصَابُ وَالْأَزْلَامُ رِجْسٌ مِّنْ عَمَلِ الشَّيْطَانِ فَاجْتَنِبُوهُ لَعَلَّكُمْ تُفْلِحُونَ ﴿٩٠﴾
Enyi walioamini! Hakika pombe na kamari na masanamu na kutazamia kwa mishale ya kupigia ramli; ni najisi na chukizo kutokana na kitendo cha shaytwaan; basi jiepusheni navyo, mpate kufaulu. [Al-Maaidah: 90]
Wahenga walinena “Asiyesikia la Mkuu huvunjika Mguu’. Rabb tumemuasi na bado tunalilia wembe uzidi kutuchinja. Heshima zinavunjika, maadili yanapotea, Uislamu tunamuachia Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na kadhalika.
Pombe ndio mama wa maasi yote, kwani kwayo hiyo pombe tumeshuhudia mauaji, ubakaji, liwaati, uvutaji wa kokeni na bangi, uzinifu, wizi, utovu wa adabu na kadhalika. Ulimwengu wa leo umejikubalisha kwamba kuna pombe halali na haramu. Ni yale maneno ya vijana kunena “Mbwa kumuita Jibwa”. Na haya yamethibishwa na Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) miaka alfu mia nne iliyopita kwamba watu watalewa na kuipa jina jengine hiyo pombe:
“Watu katika Ummah wangu watakunywa pombe wakiipa jina jengine lisilokuwa hilo…” [Ibn Maajah na Shaykh Al-Albaaniy ameipa daraja ya Swahiyh]
Halikadhalika, tuelewe ya kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amebainisha kuanguka laana za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) juu ya pombe na kwa kila mtu:
1) Mwenye kuukamua (kuutengeneza).
2) Mwenye kutengenezewa.
3) Mnywaji.
4) Mbebaji.
5) Anayebebewa.
6) Anayeendesha (kuupeleka ulevi).
7) Muuzaji.
8) Anayekula thamani yake.
9) Anayenunua na
10) Anayeuza.
[Imepokewa na At-Tirmidhiy na Ibn Maajah]
Tumeshuhudia ushiriki wa vyombo vya habari nchini vikitangaza pombe kwa kunadi “klabu fulani itapigisha taarabu…” hiyo klabu hapo ni ya pombe. Ni mbwa mwitu kujivalisha ngozi ya kondoo tu. Baadhi ya vijana wenye ushabiki mkubwa tena uliochupa mipaka, wanavaa fulana za timu ya mpira yenye kutangazia pombe. Ukizingatia wanaovaa wengi katika timu hizo za mpira ni Waislamu! Na viongozi wa timu hizo ni Waislam na ndio wa kwanza kuweka mkataba wa kuvaa matangazo hayo ya pombe. Isitoshe hata ligi hizo za mpira zinadhaminiwa na mashirika ya pombe na kwa masharti yao! Je, tamaa hizo za vijipesa vidogo vinavyotolewa na makampuni hayo ya pombe vinaweza kweli kumfanya Muislam kupingana na Rabb wake? Hali hiyo inachangiwa zaidi na vijana wengi wa Kiislam kukosa misingi ya Dini na hatimaye kuwaondoshea khofu kabisa ya Muumba wa mbingu na ardhi na vilivyomo ndani ya viwili hivyo.
Ubaya zaidi ni kwamba mpaka sikukuu za Kiislamu zinashirikishwa kwenye matangazo hayo. Hata Jumuiya za Kiislamu zikitoa kauli ya kukemea tabia hiyo hakuna linalotekelezwa wala japo watu kukhofia.
Tutambue kwa mujibu wa Hadiyth ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kwamba mtangazaji, mbebaji na wote wanaofanana nao wapo kundi moja. Tusiwe tunamnyooshea kidole mnywaji pombe tu. Huku tukiwasahau ndugu zetu wanaobeba pombe kwenye gari zao na wakati huo huo kipindi cha Swalah wanakwenda kumsujudia Yule Aliyewakataza na kuwaharamishia hayo wayafanyayo! Kwa maana nyingine, ni kama wanamfanyia istihizai.
Enyi vijana na wazee wa Kiislamu. Tuelewe ya kwamba kiini cha kusimama Uislamu ni ndani ya familia zetu. Na ulevi ndio kiini cha kuporomoka kwake. Historia ya Kiislamu yaonesha kwamba Andalus (Spain) ilikuwa ni nchi iliyoendelea mno katika nyanja za maadili ya Kiislamu. Hawakupelekewa vifaru, mizinga wala ndege za vita kuuporomosha Uislamu. Ila Makafiri waliwafungulia mlango wa pombe na kuwapumbaza kwa wanawake na starehe za kipuuzi wakaacha mafundisho yao na maadili yao na mwishowe ukawa ndio mwanzo wa kuporomoka dola za Kiislam zenye nguvu hadi leo hii.