Zingatio: Dunia Imeponywa Kwa Kuja Nabiy (صلى الله عليه وآله وسلم)

 

Zingatio: Dunia Imeponywa Kwa Kuja Nabiy

(Swalla Allaahu ‘Alayhi Waalihi Wa Sallam

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Iwapo miujiza ya 'Iysa (‘Alayhis-salaam) ilikuwa ni kuwarudisha wafu kuwa wahai na kuwaponya wagonjwa kuwa wazima na vipofu kuweza kuona, basi hakika muujiza wa Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ulikuwa ni mkubwa na bora kuliko hiyo.

 

 

Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliurudisha ulimwengu na mataifa yake katika uhai wake, aliwaponya watu kutokana na maradhi yao ya kijahili na matatizo ya moyo pamoja na jamii. Sio tu kuwaponya watu kwa nje tu, bali kuwaongoza katika uongofu wa moyo na macho.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

 

أَوَمَن كَانَ مَيْتًا فَأَحْيَيْنَاهُ وَجَعَلْنَا لَهُ نُورًا يَمْشِي بِهِ فِي النَّاسِ كَمَن مَّثَلُهُ فِي الظُّلُمَاتِ لَيْسَ بِخَارِجٍ مِّنْهَا ۚ كَذَٰلِكَ زُيِّنَ لِلْكَافِرِينَ مَا كَانُوا يَعْمَلُونَ ﴿١٢٢﴾

Je, aliyekuwa maiti kisha Tukamhuisha na Tukamjaalia nuru anatembea kwayo kati ya watu, ni sawa na yule ambaye yumo katika viza si mwenye kutoka humo? Hivyo ndivyo walivyopambiwa makafiri yale waliyokuwa wakiyatenda. [Al-An’aam: 122]

 

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakika amefikia hadhi ya juu ya ucha wa Allaah na ukamilifu. Kiongozi wetu huyu bila ya shaka ni rahmah kwa ulimwengu huu. Hatuna budi kwa mapenzi yetu kufuata yale aliyotuamrisha na kuacha yale aliyotutaka kuyaepuka.

 

 

Siri zilizokuwepo nyuma ya ukweli wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) hakika Anazitambua Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) basi, wala hakuna mwengine wa kueleza uhalisia wa Nabiy wetu. Tabia, matamshi, uongozi, subira na ukarimu wake havikupata kuchomoza katika ulimwengu huu. Hii sio sababu ya kumfanya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) kuwa ni muumba wetu au kumtukuza kinyume na alivyoamrisha. Hakuna haja ya kumsifu kupindukia au kuelezea sifa zake ambazo Muumba wetu pekee Anazitambua. Kwani Anayeelewa siri zote za uumbaji ni Bwana wa Muhammad, Bwana wa viumbe na Bwana wa kufanya Alitakalo.

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’ala) Ndiye mwenye elimu ya kiongozi huyu wa dunia, Muhammad mtoto wa 'AbduLlaah, kwasababu Yeye Ndiye Aliyemuumba kama Alivyotaka, kumlea kama Alivyopenda, kumfanya kiumbe bora na kumpa Ujumbe pamoja na kumfanya kuwa ni rahmah kwa viumbe wote.

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anasema:

وَمَا أَرْسَلْنَاكَ إِلَّا رَحْمَةً لِّلْعَالَمِينَ ﴿١٠٧﴾

Na Hatukukutuma (ee Muhammad صلى الله عليه وآله وسلم) isipokuwa ni rahmah kwa walimwengu. [Al-Anbiyaa: 107]

 

 

Huyu ndiye Nabiy ambaye watu wanampenda pasi na kumuona, alikuwa ni mfano bora kwa dunia. Aliutengeneza Ummah huu na kuupamba kwa kila zuri na kuondosha kila lenye kwenda kinyume na maumbile ya mwanaadamu.

 

 

Kwa namna hii ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), hakuna haja ya kuwa na mshangao wa namna Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) walivyokuwa wakipigana kugombea maji yake aliyotilia wudhuu ama kumwiga katika mwenendo wake wote n.k.. Hawa ndio Swahaba ambao katu hatutawafikia kwa mapenzi yao juu ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), waliitoa miili yao, roho zao na watoto wao kwa ajili yake tu.

 

 

Utiifu ambao Swahaba (Radhwiya Allaahu ‘Anhum) ulitimia kwa kufuata mwenendo wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) na sio kuzua yale yanayokwenda kinyume na mafundisho yake au kumsherehekea kwa mwaka mara moja na kumsahau kila siku katika matendo na maagizo yake aliyokuja nayo kutoka kwa Rabb wake.

 

Share