Zingatio: Tumesikia na Tunatii

 

Zingatio: Tumesikia Na Tunatii

 

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Kuna njia moja na njia moja tu inayoweza kutuwezesha kupata mafanikio. Imani ya Uislamu! Ni imani ndio iliyowasaidia Waislamu wa kale na bado inabaki kuwa ni nguvu pekee ambayo itakisaidia kizazi cha leo. Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anatuamrisha kufuata njia hiyo:

 

وَأَنَّ هَـٰذَا صِرَاطِي مُسْتَقِيمًا فَاتَّبِعُوهُ ۖ وَلَا تَتَّبِعُوا السُّبُلَ فَتَفَرَّقَ بِكُمْ عَن سَبِيلِهِ ۚ ذَٰلِكُمْ وَصَّاكُم بِهِ لَعَلَّكُمْ تَتَّقُونَ ﴿١٥٣﴾

Na kwamba hii njia Yangu iliyonyooka, basi ifuateni. Na wala msifuate njia nyinginezo zitakufarikisheni na njia Yake. Hivyo ndivyo Alivyokuusieni (Allaah) kwayo mpate kuwa na taqwa. [Al-An’aam: 153]

 

Nafasi na matatizo yetu ya leo sio tofauti na yale yaliyowakuta Waislamu wa kale. Walikuwa ni wachache lakini waliweza kufanikiwa na kuwashinda hata Warumi na Wafursi. Hao Warumi na Wafursi walikuwa na nguvu za kijamii, kisiasa na kiuchumi. Juu ya hivi, muujiza mkubwa ni kwamba waliwashinda Kaizari na Kosroisi sio zaidi ya miaka 50 tu. Yote haya yalifanyikaje? Si chengine ila ni imani yao!

 

Njia iliyonyooka ya Uislamu haipitiki kwa kuwa Muislamu pekee tu. Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anatusisitiza kufanya amali za kumnyenyekea Allaah sio kwetu sisi tu, bali pia kuwahimiza vizazi vyetu kushikamana na njia hii:

 

“Fanyeni amali katika kumtii Allaah na ogopeni kumuasi Allaah, waamrisheni watoto wenu kufuata amri na kuacha makatazo, kwani hilo litawakinga watoto wenu na nyinyi na moto” (Ibn Jariyr na Ibn al-Mundhir).

 

Kwanini hatuna nguvu za kutosha kuuhami Uislamu wetu angalau kwa vitendo vyetu? Ajabu tunasimama na kumuomba Mola wetu mara 17 kwa siku Atuongoze njia iliyonyooka na hali ya kuwa hatujafunua nyoyo zetu kuhitajia huo muongozo. Tunatamka kwamba Yeye Ndiye tunayemuabudia na Yeye tu Ndiye tunayemuomba mara 17 kwa siku. Lakini bado tu, hauonekani uwiano baina ya maombi yetu na wajibu wetu wa kuuhami Uislamu.

 

Tukumbuke kwamba njia ya Uislamu tuliyoichagua haitotupatia mafanikio kiurahisi kwa kuwa tu ni Waislamu huku tukiwa tunacheza miziki, kunywa pombe, kuzini, kula riba na kadhalika. La hasha! Hiyo siyo njia aliyoamrishwa Muislamu ndani ya Uislamu. Muislamu anayezungumzwa na Uislamu ni yule mwenye kumnyenyekea Muumba wa Mbingu na Ardhi pamoja na kufuata maamrisho yote aliyokuja nayo Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).

 

Halikadhalika, tuelewe ya kuwa Dini ya Uislamu tuliyoichagua kwa ridhaa zetu haijatandikiwa maua wala sio njia inayofanana na kitanda cha king size au zulia jekundu red carpet. Isipokuwa Uislamu ni njia inayohitaji kujitolea kwa kujisalimisha mbele ya amri za Muumba. Hivyo Muislamu kwa kujitolea huko awe tayari kutoka majasho na machozi. Kwa hali na mali awe tayari kusema ukweli na kuwa muaminifu maishani mwake mwote. Hatutakiwi kumuabudia Muumba kwa kuchupia chupia tu. Allaah Anasema:

         

وَاعْبُدْ رَبَّكَ حَتَّىٰ يَأْتِيَكَ الْيَقِينُ﴿٩٩﴾

Na mwabudu Rabb wako mpaka ikufikie yakini (mauti). [Al-Hijr: 99]

 

Uislamu unahitaji hamasa, mashaka na kuwa tayari kwa lolote. Lililo jipya hapa ni lipi? Mbona vyama na jumuiya nyengine zinakuwa na mafanikio? Bila ya shaka mafanikio yao yametokana na kujitolea kwao. Iweje sisi tushindwe kuacha kuzini na muziki au kubwiga madawa ya kulevya na mirungi? Hakuna njia ya mkato ya kufanikiwa. Mafanikio ambayo kama tutamuuliza Muislamu yeyote mwenye akili zake timamu atakujibu ni kuipata Jannah. Hiyo Jannah Muislamu mwenzangu haipatikani kwa kutundika mguu ukiangalia TV masaa chungu nzima huku ukiwa umeridhika kwa kuswali na kufunga tu.

 

Ni kipi cha kufanya ili kutambua kwamba Uislamu ni bora kwetu? Tukielewa fika kwamba Uislamu ni mfumo bora kabisa unaoweza kupatikana duniani kote, na kwamba taariykh, jiografia na nafasi yetu kimataifa inaonesha kwamba tunaweza kurudia heshima, uongozi na haki kwenye dunia hii. Basi ni imani ndiyo itakayotufanya kutambua nafasi yetu ndani ya dunia hii. Imani ambayo inapatikana kwa kukaa kitako kusoma Qur-aan na Sunnah pamoja na kuzifanyia kazi kanuni zilizomo humo.

 

Kama kweli tumechagua Uislamu kuwa ni njia yetu ya maisha. Tukatamka kwa ndimi zetu pamoja na kuyakinisha ndani ya mioyo yetu kwamba Qur-aani ni Kitabu chetu na Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ndiye Nabiy wetu, tutamke kwa sauti kali na kauli moja: “Tumesikia na tumetii” [Al-Baqarah: 285]

 

 

Share