Zingatio: Kila Mmoja Ni Mchunga

 

Zingatio: Kila Mmoja Ni Mchunga

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

Ni kawaida ya mwanaadamu kukamata mambo kwa njia nyepesi na ya haraka kabisa tokea anapozaliwa. Kutokana na kipaji hichi ndio huweza kuvumbua mambo kwa sababu tu ya kuona na kuwaza kwake. Bila ya shaka walio wengi watakubaliana nami ya kwamba mtoto ni sumaku ya kukamata mambo kwa haraka mno kuliko kifuu tundu cha mtu mzima. Ndio maana hata Salafus Swaalih walitilia mkazo kuwahifadhisha watoto wao Qur-aan na Sunnah tokea awali.

 

Kwa hakika Muislamu anapoingia ndani ya ndoa ana azma ya kupata kizazi. Kikubwa ambacho kinacholengwa ni kurithiwa mali ili isiende nje ya mstari wa mzazi. Lakini anasahau kabisa kumrithisha elimu ya Uislamu ambayo itamsaidia hapa duniani na Aakhirah. Elimu ambayo itamjenga kuwa na tabia njema, muadilifu mbele ya jamii inayomzunguka na kiongozi wa kupigiwa mfano wala asiyependa majivuno. Badala yake wazee wanatilia mkazo kulipa alfu za dola kila mwaka kwa elimu ya Magharibi ndani ya shule za chekechea, sijui hali inakuwaje kwa shule za msingi na sekondari? Basi na tukumbuke ya kwamba sote ni wachunga na sote tutaulizwa kuhusu tunavyovichunga. Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

“... Mume ni mchungaji wa familia yake, naye atapaswa kuulizwa juu ya anaowachunga. Na mke ni mchungaji wa nyumba ya mumewe, naye pia atapaswa kuulizwa juu ya anachokichunga.” [Al-Bukhaariy na Muslim].

 

Masikitiko makubwa ni kwamba tunaacha nyuma mafundisho yetu ya Uislamu kwa kujitumbukiza ndani ya dimbwi la Magharibi, ingawa hao watu wa Magharibi kwa kiwango kikubwa wanajilaumu juu ya mila zao na wana hamu kubwa ya kuwa na misimamo ya Kiislamu.

 

Tunawaona wazee wakiwapa uhuru mkubwa watoto wao hadi kuwa na runinga au internet ndani ya vyumba vyao bila ya usimamizi na uangalizi wa mzazi. Mbali ya runinga ya mtoto, ukumbini nako kuna seti ya movie theatre na music system. Tuelewe ya kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Hapendi mambo ya upuuzi na hupenda ya maana. Ni uhuru huu wanaotumia vizazi vyetu kuangalia mambo ya anasa pamoja na kufuata mila za ki-Magharibi. Kwani kwa kiwango kikubwa Magharibi wamefanikiwa kuweka anasa chungu nzima za kuhamasisha maingiliano ya kinyama.

 

Muwekee mkazo mwanao ahifadhi Qur-aan pamoja na Sunnah ya Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), na sio kumfanyia sherehe za birthdays kila mwaka ukipoteza pesa na huku ukijichumia madhambi ya gharama. Maasi yote haya yanafanyika kutokana na kukosa khofu ya kumtii Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa). Tuisome na tuizingatie Hadityh ifuatayo ya Nabiy wetu (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

 “Fanyeni amali katika kumtii Allaah na ogopeni kumuasi Allaah, waamrisheni watoto wenu kufuata amri na kuacha makatazo, kwani hilo litawakinga watoto wenu na nyinyi na moto” [Ibn Jariyr na Ibn al-Mundhir].

 

“Kuzaa si kazi, kulea ndio kazi” Ndivyo wanavyosema Waswahili. Kwani kuna mikasa aina wa aina ya uashareti yametokea juu ya kukosa ulezi na muongozo wa kufuata amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa).

 

Tunasikia kesi za kupandishwa kizimbani kwa mzazi wa miaka 50 kutokana na kumlawiti mwanawe wa kiume. Walimu wanapelekewa malalamiko ya wanafunzi wao walio chini ya umri wa miaka 10 kulaliana wakiwa utupu kabisa! Watoto ambao wamekubali kabisa kutenda hayo matendo, na ili kuwaangalia kama wanaelewa kuwa ni kosa wakaambiwa warudie hicho kitendo ndani ya chumba kilicho faragha. Wapi? Hawakuweza kufanya kwa sababu walielewa kuwa ni kosa, hivyo wanahitaji kujificha na wasijulikane sio wakati kama huo ambao watajulikana wanafanya nini. Mkasa mwengine ni wa mwanamme aliye baina ya miaka 10 hadi 13 kuwachukua nduguze wa kiume na kwenda kuwanajisi. Wapi wameona watoto hawa mambo hayo?!

 

Bado hawana shahawa za kuzalisha mbegu za uzazi wanafanza mambo hayo, wakiingia balehe watafanya nini hawa jamani? Yaa Allaah! Yote haya yametokea na yanaendelea kutendeka ndugu zangu wa Kiislamu. Wamefunzwa na nani haya kama sio wazazi/jamii kuwapatia uhuru mkubwa na kutojali maisha yao?!

 

Tukumbuke ya kwamba adhabu za Rabb ni kubwa na huo Moto Alioumba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuni zake ni watu na mawe. Moto ambao hauna usimamizi wa askari atakayepokea rushwa, bali unasimamiwa na Malaika wasiocheka, walio wakali na wenye nguvu. Tuielewe na tuifanyie kazi amri ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ya kujikinga pamoja na jamaa zetu kutokana na adhabu Zake: 

 

يَا أَيُّهَا الَّذِينَ آمَنُوا قُوا أَنفُسَكُمْ وَأَهْلِيكُمْ نَارًا وَقُودُهَا النَّاسُ وَالْحِجَارَةُ عَلَيْهَا مَلَائِكَةٌ غِلَاظٌ شِدَادٌ لَّا يَعْصُونَ اللَّـهَ مَا أَمَرَهُمْ وَيَفْعَلُونَ مَا يُؤْمَرُونَ﴿٦﴾

Enyi walioamini! Jikingeni nafsi zenu na ahli zenu na moto ambao kuni zake ni watu na mawe; juu yake wako Malaika washupavu hawana huruma, shadidi, hawamuasi Allaah kwa yale Anayowaamrisha na wanafanya yale wanayoamrishwa. [At-Tahriym: 6]

 

Shime tujihimize juu ya amri za Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) ambazo tumewekewa kwa maslahi yetu wenyewe. Tunaweza kuwachunga watoto wetu ingawa ni vigumu kwa hali ilivyo, lakini Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Anamhukumu mja kutokana na juhudi yake. Hivyo timiza wajibu na umuombe Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amuongoze mwanao.

 

Share