Zingatio: Wala Msichupe Mipaka

 

Zingatio: Wala Msichupe Mipaka

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Maisha ya Muislam hapa duniani hayahitaji kujiumiza kichwa na kupata homa kwenye mambo yasiyo na maana. Siyrah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) haioneshi kwamba alikuwa ni mwenye maisha ya fakhari. Zinaposimuliwa Taariykh zake waweza ghafla moja kububujikwa na machozi.

 

Huyo ndiye Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam), ambaye ubora wake haukupata kuchomoza kabla yake wala baada yake. Kila mwanaadamu anastahiki kumuiga hata kwa asiye Muislam kdhaalika. Hiyari yageuka sharti kwa sisi tunaojiita Waislam. Kwani nguzo kuu ya Uislamu ni kumkubali kwamba yeye ndiye Nabiy wa mwisho.

 

Mama wa Waumini Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa), mke wa Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) anasimulia: "...Tuliweza kuona miezi mitatu pasi na kuwasha moto (kwa ajili ya kupika chakula) katika nyumba za Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam)". [Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim, Na. 2972, na Swahiyh Al-Bukhaariy, Na. 2567]

 

Kwenye Hadiyth nyengine, Mama wa Waumini 'Aaishah (Radhwiya Allaahu ‘Anhaa) anasimulia: "Mto wa Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aliokuwa akiulalia ulitengenezwa kwa ngozi ya mnyama iliyojazwa nyuzinyuzi za mtende." [Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Muslim, Na. 2082, na Swahiyh Al-Bukhaariy, Na. 6456]

 

Naye ‘Amr bin al-Haarith, mmojawapo miongoni mwa Swahaba wa Nabiy(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alisema kuwa pindi Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alipofariki, hakuacha mali wala kitu chochote isipokuwa nyumbu wake mweupe wa kupanda, ngao na kipande cha ardhi alichokiacha kwa ajili ya Sadaka. [Imesimuliwa ndani ya Swahiyh Al-Bukhaariy, Na. 2739, na Musnad Ahmad, Na. 17990]

 

Hiyo mifano iliyopo juu ndio tunayohitajia sisi kuiweka mbele na kuiiga. Lil asafin shadiyd – kwa masikitiko makubwa ni kwamba tumeyatupa nyuma mafunzo hayo na tunaangalia matamanio yetu zaidi.

 

Tumekosa muelekeo na muongozo hata kwenye shughuli zetu muhimu. Harusi tunazozisherehekea sasa zimejaa fujo, ubadhirifu, israfu na uzushi uliochupa mpaka. Wenye shughuli watavuka mipaka hadi kupigisha dansi, kunywesha ulevi na kufanya mikusanyiko baina ya wanawake na wanaume kuwa ni halali kabisa.

 

Iweje basi ndugu yangu Muislam uumize kichwa na kupata usumbufu kwa kuifikiria harusi? Michango ya mamilioni ni ya nini zaidi ya kuwalisha walioshiba? Nyumba utakayojenga utaiacha hapa hapa na kitanda chako kitarithiwa na mume atakayemuoa kizuka chako.

 

Halikadhalika, mambo ya kutolewa Bibi na Bwana Harusi katika masteji, kupambwa, kulishana keki na hadi kupigana mabusu hadharani na kupatiwa waalikwa zawadi za bei mbaya hayana mnasaba wowote ndani ya Uislamu. Haya ni mambo yasiyokubalika katika Uislam na yanayopoteza fedha nyingi kwa kuyafanya, na yanasumbua akili pamoja na kupoteza wakati. Ni shughuli hizi zinazowafanya vijana kuona ugumu wa kuoa. Kwani wanaelewa kuwa masumbufu haya ndio sharti za ndoa.

 

Ni nasaha kwa vijana na wazee kuikumbuka ile amri katika Qur-aan inayosema: 

 

وَأَنكِحُوا الْأَيَامَىٰ مِنكُمْ وَالصَّالِحِينَ مِنْ عِبَادِكُمْ وَإِمَائِكُمْ ۚ إِن يَكُونُوا فُقَرَاءَ يُغْنِهِمُ اللَّـهُ مِن فَضْلِهِ ۗ وَاللَّـهُ وَاسِعٌ عَلِيمٌ ﴿٣٢﴾

Na waozesheni wajane miongoni mwenu na walio Swalihina kati ya watumwa wenu wanaume na wajakazi wenu. Wakiwa mafakiri Allaah Atawatajirisha katika fadhila Zake. Na Allaah Mwenye Wasaa, Mjuzi wa yote. [An-Nuwr: 32]

 

Allaah Ndie Mtoaji wa rizki sio mwanaadamu. Yahitaji utulivu wa nafsi kuyafanya masuala ya harusi. Na lililo kubwa ni kumtegemea Mola pamoja na kutambuwa kwamba hakuna utajiri duniani kuliko qana’ah.

 

Tuangalie kwa upande wa maisha ya Sayyidna 'Aliy pamoja na mkewe Bibi Faatwimah binti RasuuliLlaah (Radhwiya Allaahu ‘Anhuma) walipoingia kwenye ndoa. Anasimulia Sayyidna 'Aliy:

 

"Nilipomuoa Faatwimah hatukuwa tukimiliki zaidi ya ngozi ya kondoo tuliyokuwa tukiitandika wakati wa usiku na kulala juu yake, na wakati wa mchana tulikuwa tukiikalia, na hatukuwa na mfanyakazi wa kutusaidia shughuli za nyumba, na (Faatwimah) alipoletwa nyumbani, Rasuli wa Allaah (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) alimpa mtungi wa maji na gilasi mbili pamoja na kitambaa na mito miwili iliyojazwa ndani yake majani ya mtende."

 

Ni nasaha kwa kila Muislam kuchunga mali yake. Kwani mwanzo wa kufanya israfu ni kuacha kuchunga kile unachochuma. Hii ni kwa sababu ya kukosa kumbukumbu kwamba kila neema itaulizwa: 

مَّ لَتُسْأَلُنَّ يَوْمَئِذٍ عَنِ النَّعِيمِ ﴿٨﴾

Kisha bila shaka mtaulizwa Siku hiyo kuhusu neema. [At-Takaathur: 8]

 

Tumuogope Allaah na tuelewe kuwa kila shari au kheri italipwa hata iwe ni ndogo mfano wa mdudu chungu.

Share