Zingatio 1: Ramadhwaan Inabisha Hodi

 

Zingatio 1:  Ramadhwaan Inabisha Hodi

 

Naaswir Haamid

 

Alhidaaya.com

 

 

 

Enyi makundi ya Waislamu, vijana kwa wazee, wanawake kwa wanaume, matajiri na masikini, weusi na weupe, wagonjwa kwa wazima; basi haujafika tu wakati wa kukaa kitako na kuipangia mikakati Ramadhwaan iliyopo njiani? Imeshafika mlangoni na yabisha hodi kwa nguvu zote, basi ifungulieni mlango na muitandikie zulia la upendo na ukarimu.

 

Huo ndio mwezi wa Ramadhwaan ambao ndani yake kuna fadhila nyingi na matunda yake mutakuja kuyaona mbele ya Muumba. Kuna mazingatio makubwa katika Swawm hapa duniani kama vile kujua hali za mafakiri na masikini, kulikausha tumbo na kulifanya kuwa na afya zaidi na mengineyo zaidi.

 

Halikadhalika, kuna mazingatio ya kwamba tendo hili halijulikani malipo yake hata kwa Malaaikah, kwani Rabb Amewahakikishia kwamba ni Yeye tu Ndiye Atayekwenda kuilipa kwa haki inayotakiwa kulipwa. Kwa sababu funga ni ‘ibaadah ya siri kabisa baina ya mja na Rabb wake, hakuna mwanaadamu anayeweza kututhibitishia kwamba fulani amefunga au vyenginevyo. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Kila amali njema anayoifanya mwanaadamu italipwa mara kumi … Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) amesema: Ila kufunga kwa sababu funga ni kwa ajili Yangu, na ni Mimi mwenyewe Nitakayeilipa…" [Imesimuliwa na Abu Hurayrah na kupokewa na Al-Bukhaariy na Muslim]

 

Tena kwa utaratibu na ustaarabu wake, mgeni huyu hafiki kwako kuigonga milango yenu bila ya kuwaletea taarifa. Daima anawaletea ujumbe wake kwamba atakuja kukutembelea, anazielewa silka na tamaduni za ugeni. Ameshaondoka tarishi wake Rajab na karibuni ataondoka mjumbe mwenziwe Sha’abaan, ili kumpisha mgeni karimu Ramadhwaan. Basi ninawanasihi mumfungulie mlango kwa tabasamu kubwa na huku mioyo yenu ikiwa wazi kwa faraja pamoja na kupokea mafunzo yote atakayokuachia nayo.

 

Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) ametuelezea kuhusu fadhila za mwezi huu: "Umekujieni mwezi wa Ramadhwaan, ni mwezi wa Baraka.  Imefanywa Swawm kwenu kuwa ni Fardh, milango ya Jannah hufunguliwa na milango ya moto hufungwa na Mashaytwaan hufungwa. Umo katika mwezi huu usiku ulio bora kuliko miezi alfu. Atakayenyimwa kheri zake hakika kanyimwa [yote ya kheri]." [Imepokewa na Imaam Ahmad]

 

Unadhifu wa matendo ya Ramadhwaan ni kuitimiza amri ya Swawm bila ya kutafuta hoja. Kwani Waumini wa kweli husema:

سَمِعْنَا وَأَطَعْنَا ۖ 

Tumesikia na tumetii [Al-Baqarah: 285]

 

Itakuwa ni hasara kubwa kumkimbia Ramadhwaan, ukajitia shughuli na uziwi hadi kushindwa hata kumfungulia mlango nyumbani kwako na moyoni mwako. Hivyo, jitahidini kwa ukarimu wake Ramadhwaan kuwa ni sababu ya kuondolewa katika usajili wa watu wa Motoni. Allaah Atukinge na adhabu hiyo.

 

 

Share