Zingatio: Uislam Ni Mwepesi

 

Zingatio: Uislam Ni Mwepesi

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Kila mwanaadamu anapojaaliwa kupambazukiwa siku mpya huwa na malengo mapya ambayo yatamsaidia kwenye maisha yake. Malengo ambayo mengine ni mazuri na wakati huo huo yapo maovu. Na hayo malengo yote yaweza kufanikiwa kwa njia zilizo mbaya au nzuri.

 

Anasema Hasan Al-Baswriy (Rahimahu Allaahu) ya kwamba siku inapochomoza hunadi kwa mwanaadamu kumtaka aitendee haki siku hiyo pamoja na nafsi yake:

 

Hakuna siku ichomozayo alfajiri yake isipokuwa huita; Ee Mwanaadamu, mimi ni kiumbe kipya, na nitakuwa shahidi wa matendo yako, basi nitumie kwa kufanya matendo mema, kwani mimi sitarudi mpaka siku ya Qiyaamah.”

 

Wapo ambao hujaribu kuimiliki dunia ndani ya mikono yao na hufanya kila liwezalo kuhakikisha wanafanikiwa. Wanatengeneza zana wanazoita za usalama kumulika harakati zote zifanywazo duniani. Hao wakajiwekea mipaka yao ya vita, na wanapowapiga wenzao kwa vifaru husema kwamba wao ndio wanaovamiwa ilhali wao ndio walianza ukorofi.

 

Inadhihirika ndani ya maisha ya baadhi ya Waislam ya kwamba, huamka asubuhi wakiwa na bendera ya Shaytwaan wakielekea kutafuta riziki bila ya kujali mipaka ya Rabb Mlezi. Hujiingiza kwenye mashaka asubuhi na mchana wakijilazimisha kufanikiwa malengo. Mashaka hayo sio tu katika kupata riziki, bali pia yanapenyezwa (mashaka haya) kwenye sherehe zilizosuniwa na Nabiy wetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam). Zipo pia shughuli nyengine (zinazoitwa za Kiislam) zisizo na miguu wala kichwa zaidi ya kumpotezea Muislam wakati wake ulio ghali mno.  Nazo ndio zimejaa chungu nzima hata kusababisha Waislam kukhitilafiana na wengine kupata maradhi ya moyo na presha kwa matatizo ya kujitakia.

 

Waislam sasa wanajiingiza kwenye migogoro ndani ya misikiti, mirathi haifuatwi na kila mmoja anataka asilimia yote mia ya urithi iingie kwenye mkono wake, wengine wanadai kumiliki ardhi zisizo zao kwa viapo vya uongo! Sio hayo tu, bali dada zangu wa kike watatafuta kwa hali zote kuuharibu mwili wake ili aende kujikumbia dhambi kwenye kumbi za starehe na akitoka hapo ameshalewa, ameshazini na ameshagonganisha ndoa za watu chungu nzima.

 

Tuelewe ya kuwa maisha hayo yote kwetu ni mazito, Uislam haujafika kuja kutufanyia mambo kuwa mazito. Haya mashaka na tabu yote tunajitakia sisi wenyewe: 

 

يُرِيدُ اللَّـهُ بِكُمُ الْيُسْرَ وَلَا يُرِيدُ بِكُمُ الْعُسْرَ

Allaah Anakutakieni mepesi na wala Hakutakieni magumu.. [Al-Baqarah:185]

 

Uislamu haumuamrishi mfuasi wake kujiingiza kwenye shughuli zisizo na manufaa. Haya yote yanatokana na kukosa khofu, hata ibada zetu tunaziingiza mambo ya fedheha na kashfa kubwa. Wakati kama wa Ramadhwaan unahitaji matayarisho ya kutenda mema na kuazimia kuingia kwenye khayr nyingi ndani ya mwezi huu. Badala yake Waislam wanajitayarisha kuupokea kwa vunja jungu na kuumizana kichwa kwa kufanya shopping pamoja na kupandisha vyakula bei za juu kabisa.

 

Ni vyema tukaelewa ya kwamba Uislam unaharamisha yale ambayo yanaleta ufisadi na kuyawacha yale ambayo watu hawana budi nayo, na kuyachukia yale yasiyofaa na kuyapenda yale yenye maslaha zaidi. Anasema Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

قُلْ إِنَّمَا حَرَّمَ رَبِّيَ الْفَوَاحِشَ مَا ظَهَرَ مِنْهَا وَمَا بَطَنَ

Sema: Hakika Rabb wangu Ameharamisha machafu yaliyodhihirika na yaliyofichika" [Al-A’raaf: 33]

 

Na mwenye kupendwa mbele ya Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) sio yule mwenye mali nyingi au sura nzuri; vitu ambavyo sisi wanaadamu ndio tunaviweka mbele katika kumuheshimu mtu. Amesema Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam):

 

"Hakika Allaah Haangalii sura zenu na mali zenu, lakini huangalia nyoyo zenu na matendo yenu" [Muslim]

 

Hakika aliye mbora mbele ya Rabb Mlezi ni anayemcha Allaah(Subhaanahu wa Ta’aalaa):

 

Kutoka kwa Abu Umaamah (Radhwiya Allaahu ‘Anhu) kwamba Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) amesema:

 

"Allaah Amesema: Kwa kweli katika wale wanaoniabudu, Ninayempenda zaidi ni yule muumini lofa, mwenye Swalaah nyingi mwenye kujitahidi kumuabudu Rabb wake kwa siri, ambaye si maarufu kwa watu, na wala hatajiki, na ambaye hali yake ya maisha ni duni lakini anaistahamili hali hiyo…"  [At-Tirmidhiy]

 

Na kwa hakika mwenye kumukhofu Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kwa kufanya matendo mema, hujaaliwa mambo yake kuwa mepesi:

 

وَأَمَّا مَنْ آمَنَ وَعَمِلَ صَالِحًا فَلَهُ جَزَاءً الْحُسْنَىٰ ۖ وَسَنَقُولُ لَهُ مِنْ أَمْرِنَا يُسْرًا ﴿٨٨﴾

Na ama aliyeamini na akatenda mema, basi atapata jazaa nzuri. Na Tutamwambia yaliyo mepesi katika amri Yetu. [Al-Kahf: 88]

 

Tunamuomba Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Atujaalie kupata yaliyo mepesi na wala Asitufanye kuwa miongoni mwa wenye kushughulishwa na dunia hii iliyojaa mitihani:

 

“Ee Allaah hakuna jepesi ila Ulilolifanya jepesi, Nawe Unalifanya gumu jepesi ukitaka.”

 

Share