Zingatio: Kwa Wenye Akili

 

Zingatio: Kwa Wenye Akili

 

Naaswir Haamid

 

 

Alhidaaya.com

 

 

Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) Amemuumba mwanaadamu ni mwenye matamanio na akili. Tofauti na Malaika ambao wamepewa akili bila ya matamanio au wanyama waliopewa matamanio bila ya akili. Na ndio maana Qur-aan haikuteremshwa kwa Malaika wala wanyama. Imeteremshwa kwa wanaadamu ambao wanazo akili za kufahamu ili kutekeleza matamanio yao kwenye njia sahihi.

 

Kwa hakika inakuwa ni vigumu kuelewa ya kwamba mwanasayansi anashindwa kuingia kwenye Uislamu kidhati kabisa. Kwani Qur-aan imejaa sayansi aina kwa aina za kumuacha mdomo wazi huyo mwanasayansi. Na wala Hakukosea Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) kuumba Moto kwa nafsi zisizotaka kutanabahi ukweli uliomo ndani ya Qur-aan ulio wazi kabisa.

 

Ni wajibu wa kila mwanaadamu kuutafuta ukweli wa kuumbwa kwake na lengo la kuwepo kwake hapa ulimwenguni. Hata Nabiy Ibraahiym (‘Alayhis-salaam) aliangalia mwezi na jua akijaribu kuvuta fikra kwamba huwenda vitu hivi vikawa ni Rabb wake, lakini hakufikia huko akamalizia kwa qawl ya:

 

إِنِّي وَجَّهْتُ وَجْهِيَ لِلَّذِي فَطَرَ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضَ حَنِيفًا ۖ وَمَا أَنَا مِنَ الْمُشْرِكِينَ ﴿٧٩﴾

Hakika mimi nimeelekeza uso wangu kwa Ambaye Ameanzisha mbingu na ardhi nimeelemea haki, nami si katika washirikina. [Al-An’aam: 79]

 

Mara kadha wa kadhaa Aayah za Qur-aan zinamalizia na qawl za 'wenye akili', 'wenye kutanabahi', 'uongofu kwa wamchao' na kadhalika. Haingii akilini kuona kwamba Muislamu anayedai kuisadiki Qur-aan akimshirikisha Rabb Mlezi. Na anapoambiwa hukaidi akiona kuwa ni haki yake kufanya mambo ya ushirikina.

 

إِنَّ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ وَاخْتِلَافِ اللَّيْلِ وَالنَّهَارِ لَآيَاتٍ لِّأُولِي الْأَلْبَابِ ﴿١٩٠﴾ الَّذِينَ يَذْكُرُونَ اللَّـهَ قِيَامًا وَقُعُودًا وَعَلَىٰ جُنُوبِهِمْ وَيَتَفَكَّرُونَ فِي خَلْقِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ رَبَّنَا مَا خَلَقْتَ هَـٰذَا بَاطِلًا سُبْحَانَكَ فَقِنَا عَذَابَ النَّارِ ﴿١٩١﴾ 

Hakika katika kuumbwa mbingu na ardhi, na mabadiliko ya mfuatano wa usiku na mchana; bila shaka ni Aayaat (ishara, zingatio) kwa wenye akili. Ambao wanamdhukuru Allaah kwa kusimama  na kwa kukaa na kwa kulala ubavuni mwao na wanatafakari katika kuumbwa mbingu na ardhi (wakisema): Rabb wetu, Hukuumba haya bure, Utakasifu ni Wako tukinge na adhabu ya moto. [Al-‘Imraan: 190-191]

 

Aayah namna hizo ziliposhushwa kwa kipenzi chetu Muhammad (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) uso wake ulipiga wekundu na machozi yakaanza kumbubujika hadi ndevu zake zikaroana. Hiyo sio hali inayozikuta nafsi zetu kwa Rabb wetu, nafsi ambazo zinazidi kurudi hatua nyuma badala ya kwenda mbele. Tunaenziwa na Allaah (Subhaanahu wa Ta’aalaa) na tukafunzwa na Sunnah ya Nabiy (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) lakini bado hatuhitaji kutanabahi. Eeh nafsi… Wataka niambia kwamba moto ndio utakaokwenda kuwa ni gereza lako?

 

Basi elewa ewe nafsi kwamba wamekwenda kombo waliorukwa na akili mfano wa kuku, wakadonoa ulimwenguni vingi vizuri na mabaya wakazidi kuyatafuna, dunia kwao ilivamiwa kwa anasa za kila aina uijuayo na dhambi za fitna, wakapumbazika na kilevi hichi kibaya wasielewe usiku wala mchana,kwao halali na haramu zilikuwa ni kauli za ajabu wakazidi kukana, sasa wameshatangulia kaburini na waovu wengine wamepangana,malipo ya utovu wa akili zao Ayajua Jalaali Rabbana.

 

Basi tunatamka na tunakuomba kama ulivyotufunza:

 

رَبَّنَا إِنَّكَ مَن تُدْخِلِ النَّارَ فَقَدْ أَخْزَيْتَهُ ۖ وَمَا لِلظَّالِمِينَ مِنْ أَنصَارٍ ﴿١٩٢﴾ رَّبَّنَا إِنَّنَا سَمِعْنَا مُنَادِيًا يُنَادِي لِلْإِيمَانِ أَنْ آمِنُوا بِرَبِّكُمْ فَآمَنَّا ۚ رَبَّنَا فَاغْفِرْ لَنَا ذُنُوبَنَا وَكَفِّرْ عَنَّا سَيِّئَاتِنَا وَتَوَفَّنَا مَعَ الْأَبْرَارِ ﴿١٩٣﴾ رَبَّنَا وَآتِنَا مَا وَعَدتَّنَا عَلَىٰ رُسُلِكَ وَلَا تُخْزِنَا يَوْمَ الْقِيَامَةِ ۗ إِنَّكَ لَا تُخْلِفُ الْمِيعَادَ ﴿١٩٤﴾

Rabb wetu, hakika Umuingizaye motoni, kwa yakini Umemhizi. Na madhalimu hawana yeyote mwenye kuwanusuru. Rabb wetu, hakika sisi tumemsikia mwitaji anaita kwenye iymaan kwamba ‘mwaminini Rabb wenu’ basi tukaamini.  Rabb wetu, Tughufurie madhambi yetu na Tufutie makosa yetu na Tufishe pamoja na Waumini wema. Rabb wetu na Tupe Uliyotuahidi kupitia Rusuli Wako, wala Usituhizi Siku ya Qiyaamah; hakika Wewe Huendi kinyume na miadi. [Al-‘Imraan: 192-194]

 

 

Share