Ufafanuzi wa Aayah 'Oeni Wawili…'
Ufafanuzi wa Aayah 'Oeni Wawili…'
SWALI:
Naomba kuuliza suala moja. Katika suala la ndoa Allaah (S.W) ameanza kwa kusema oeni wawili,........ Sasa kwa aya hii kuna taawili gani kwa kuanzia wawili na mujibu wa qurani hisabu huanza na moja lakini hapa moja imekuja mwisho, Jee hii ya wawili inawiana na ile ya mirathi ambayo mwanamme hupata mara mbili ya mwanamke? Nadhani nitafahamika. Ahasante
JIBU:
AlhamduliLLaah - Himidi Anastahiki Allaah (Subhaanahu wa Ta’aala) Rabb wa walimwengu, Swalaah na Salaam zimshukie Nabiy Muhammad (Swalla Allaahu 'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhwiya Allaahu 'anhum) na waliowafuata kwa wema mpaka Siku ya Mwisho
Qur-aan kwa hakika ina mtindo wake wa pekee katika mambo tofauti. Si lazima kuwa Qur-aan katika mas-ala ya hesabu ianze moja kwani zipo Aayah nyingine ambazo pia hazikuanza hesabu na moja. Mfano mzuri ni Aayah ifuatayo:
الْحَمْدُ لِلَّـهِ فَاطِرِ السَّمَاوَاتِ وَالْأَرْضِ جَاعِلِ الْمَلَائِكَةِ رُسُلًا أُولِي أَجْنِحَةٍ مَّثْنَىٰ وَثُلَاثَ وَرُبَاعَ ۚ يَزِيدُ فِي الْخَلْقِ مَا يَشَاءُ ۚ
AlhamduliLLahi, Muanzilishi wa mbingu na ardhi, Mwenye kuwafanya Malaika kuwa wajumbe wenye mbawa mbili-mbili, na tatu-tatu na nne-nne. Huzidisha katika uumbaji Atakavyo. [Faatwir: 1]
Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) haulizwi kwa Afanyalo bali sisi ndio tutakaoulizwa kwa yale tuliyoyafanya hapa duniani mema au mabaya. Hakika ni kuwa hesabu hii na ile ya mirathi ni vitu viwili tofauti kabisa. Maelezo ambayo tunaweza kuyatoa ni kuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘aalaa) ndiye Muumba na ndiye mjuzi wa maumbile ya mwanaadamu. Maumbile ya mwanadamu (mwanamme) ni kutotosheka na mke mmoja na hivyo Akaanza na agizo la oeni katika muwapendao wawili, au watatu, au wanne. Hili la kuoa mmoja limekuja mwisho kwa wale ambao hawataweza kufanya uadilifu baina ya wake wengi. Kwa hivyo asli ya mwanamme ni kuwa na wake wengi na udhru wa mmoja ni kutoweza kuwa na wengi.
Na Allaah Anajua zaidi